Home Makala BURE TU!

BURE TU!

1711
0
SHARE

Dirisha la usajili limefungwa, lakini hawa wanaweza kusajiliwa muda wowote

LONDON, England

DIRISHA la usajili Januari limefungwa kwa staili ya aina yake, fedha zimetumika kidogo tofauti na lililopita mwaka jana huku kukiwa hakuna usajili wa kushtua kama ilivyozoeleka.

Pamoja na usajili huo kufanyika, bado kuna wachezaji wenye majina makubwa ambao wanaweza kusajiliwa hivi sasa au mwishoni mwa msimu huu.

Mara nyingi huwa ni ngumu kufanya usajili pindi dirisha linapofungwa, lakini kuna majina ya nyota ambao wako huru wanaweza kusaini kwenye timu mbalimbali nchini England au ligi nyingine bila tatizo.

Makala haya yanakuletea wachezaji watano ambao wanaweza kusajiliwa wakati wowote licha ya dirisha la usajili kufungwa hivi karibuni barani Ulaya.

Yaya Touré

Hana timu tangu alipoamua kuachana na Olympiacos Desemba mwaka jana, lakini kiungo huyo mwenye miaka 35 ameshindwa kuthibitisha kama ataachana na soka hivi karibuni.

“Huu si mwisho, huwezi kujua sababu, ninaweza kucheza katika ligi yoyote hata ikiwa hapa nchini England,” alisema Toure alipohojiwa na kituo cha Sky Sports.

Umri wake ni mkubwa, kasi yake imepungua tangu alipoondoka Manchester City, lakini ana nguvu, akili na kiongozi kwa wengine.

Amefanikiwa kushinda Ligi Kuu England mara tatu, Ligi ya Mabingwa Ulaya mara moja na mengine mengi, uzoefu wake unaweza kuwa msaada mkubwa wa timu zitakazomhitaji.

Misimu nane aliyokuwa nchini England amefanikiwa kufunga mabao 79 na kushinda mataji tangu alipoondoka Barcelona nchini Hispania.

Mkataba wa muda mfupi unaweza kuwa msaada kwa klabu itakayomhitaji mpaka mwisho wa msimu huu sababu bado ni mchezaji huru.

Yohan Cabaye

Wakati mkataba wake unakaribia kumalizika ndani ya Crystal Palace msimu wa 2017/18, Cabaye aliondoka na kusaini mkataba na klabu ya Al-Nasr ya Dubai.

Nyota huyo wa Ufaransa aliyecheza michezo 48 akiwa na jezi ya timu ya Taifa, alisaini miaka miwili na klabu hiyo Dubai, lakini mwezi uliopita ilitangazwa kuwa walifikia makubaliano maalumu ya kuvunja mkataba huo.

Cabaye ambaye aliwahi kutwaa taji la Ligi Kuu Ufaransa, Ligue 1, akiwa na Lile mwaka 2011 anakuwa mchezaji huru, pia aliwahi kucheza Newcastle United na PSG.

Miaka mitatu aliyokuwa Crystal Palace ilidhihirisha kuwa ni mchezaji wa daraja la juu, licha ya mkataba wake kuvunjwa bado anaweza kuwa msaada kwa klabu itakayomhitaji hivi sasa.

Giuseppe Rossi

Alikuwa mmoja wa nyota wenye vipaji vikubwa wakati wanatoka Shule ya Manchester United, lakini alishindwa kupata nafasi kikosi cha kwanza kutokana na ushindani mkubwa uliokuwepo.

Uwepo wa nyota kama Wayne Rooney, Ruud van Nistelrooy na Louis Saha ulimfanya Rossi ajiunge na Villarreal kisha Fiorentina.

Amecheza michezo 30 ya timu ya Taifa ya Italia na kufunga mabao saba, Rossi aliachana na klabu ya Genoa hivi karibuni sababu ya majeraha ya muda mrefu.

Mwezi uliopita alikuwa akifanya mazoezi na kikosi cha Manchester United kwa ajili ya kujiweka sawa lakini bado ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa na anaweza kuwa msaada kwa klabu nyingine.

Patrice Evra

Mchezaji mwingine wa zamani wa Manchester United ambaye yupo huru, Evra, amekuwa nje ya soka tangu alipoachana na West Ham msimu uliopita.

Beki huyo wa kushoto mwenye miaka 37, ni moja ya wachezaji walioshinda mataji mengi miaka 15 ya hivi karibuni, alishinda taji la Ligi ya Mabingwa, Ligi Kuu England mara tano na mawili ya Italia wakati yupo Juventus.

Evra amecheza michezo 81 akiwa na jezi ya timu ya Taifa ya Ufaransa kwa kipindi chote.

Licha ya kushindwa kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara ndani ya West Ham, baadaye anaweza kuwa msaada kwa wengine.

Uzoefu wake, uhamasishaji na ubora ni moja ya mambo anayoweza kuyatoa kwa klabu itakayofanikiwa kupata saini yake kabla ya msimu kumalizika.

Ibrahim Afellay

Moja ya wachezaji walioonyesha uwezo mkubwa wakati wakiwa bado wadogo kiasi cha kuwashawishi Barcelona kumsajili kwa euro milioni 3 kutoka PSV ya Uholanzi.

Lakini wiki iliyopita nyota huyo wa Uholanzi alifikia makubaliano ya kuvunja mkataba na klabu ya Stoke City ambayo ipo Ligi Daraja la Kwanza England.

Chini ya Pep Guardiola wakati huo Barcelona alishindwa kupata nafasi ya kucheza kutoka na uwepo wa wachezaji wenye uwezo mkubwa zaidi.

Mwaka 2015 alijiunga na Stoke City lakini hakuwa kwenye ubora mkubwa kama ilivyotarajiwa na kupelekea kuvunja mkataba huo.

Hiyo inamfanya kuwa mchezaji huru ambaye anaweza kusajiliwa wakati wowote kipindi hiki ambacho usajili umefungwa tangu wiki iliyopita.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here