Home Makala Kamati za TFF zinashusha thamani ya ligi

Kamati za TFF zinashusha thamani ya ligi

1663
0
SHARE

NA EZEKIEL TENDWA

JUMAPILI iliyopita Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ilikutana kupitia mashauri mbalimbali yaliyofikishwa kwenye kamati hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Wakili Kiomoni Kibamba.

Baada ya kukutana kwa Kamati hiyo kesho yake yaani Jumatatu wiki hii, ikajitokeza hadharani mbele ya kamera za waandishi wa habari na kutangaza matokeo ya kikao hicho kizito.

Lilikuwa jambo jema kabisa Kamati hiyo kukaa na kutoa adhabu kwa wale wote walioonekana kufanya vitendo visivyo vya kiuungwana kwenye mchezo wa soka kwani michezo ni furaha na wala si ugomvi.

Hata hivyo, bado kuna tatizo kwenye Kamati hiyo kwani yapo makosa yaliyofanyika muda mrefu ambayo kwa hali ya kawaida ilikuwa maamuzi yawe yameshatolewa na wahusika kumaliza kabisa adhabu zao.

Kwa mfano, shauri namba moja lililokuwa likimhusu beki wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ ambaye alimpiga kiwiko mchezaji wa Coastal Union mchezo uliochezwa Februari 3, 2019.

Kutoka Februari 3 hadi Machi 11 ambapo Kamati wanatoka hadharani na kutoa adhabu, ni sawa na mwezi mmoja na siku nane. Yani mpaka hata yule aliyetendewa kosa ameshasahau kilichotokea.

Kama Kamati hiyo ya nidhamu ingetoa adhabu mapema inamaanisha kwamba Ninja angekuwa ameshakosa michezo yake hiyo mitatu na sasa angekuwa anaitumikia timu yake kama kawaida.

Sasa achana na hiyo, kuna kesi nyingine namba saba inayomhusu Meneja wa timu ya Transit Camp, John Mchemba. Huyu alifanya kosa Novemba 10, 2018 katika mechi namba 31, kundi B dhidi ya Green Warriors iliyofanyika Azam Complex.

Huyu amekutwa na kosa la kuanzisha vurugu na kusababisha mchezo kusimamishwa na hata alipopelekwa jukwaa kuu lakini aliendelea na vurugu hizo hivyo amesimamishwa kujihusisha na mpira wa miguu kwa miezi mitatu na faini ya Sh laki mbili (200,000).

Hii inashangaza kidogo kwani kosa ambalo lilifanyikaa mwaka jana ilitakiwa maamuzi yangechukuliwa mapema mwaka huohuo au mapema Januari mwaka huu, lakini inasubiriwa mpaka mwezi wa tatu! Inafikirisha kidogo.

Yani kosa la kusababisha vurugu uwanjani mtu anakaa miezi minne ndipo wenye mamlaka wanaibuka na kutoa adhabu? Kweli tupo siriazi na mpira wetu? Tuna dhamira ya dhati kuupeleka mpira wetu mbele? Sidhani.

Kuna vitu ambavyo tuliviona kwenye utawala uliopita wa Jamal Malinzi tukadhani utawala huu wa Wallace Karia, ni mwendo wa viwango lakini tunaona uendeshaji wa soka letu unazidi kudidimia badala ya kwenda mbele.

Kuna ile Kamati ya Saa 72 mbona haionekani kufanya kazi yake ipasavyo? Saa 72 ni sawa na siku tatu sasa kama tunasubiri mpaka miezi miwili hadi mitatu ikatike ndio maamuzi yatoke, hakuna sababu ya kuwa na kamati hiyo.

Kama Kamati hiyo itaendelea kuwepo nashauri hilo jina la saa 72 libadilishwe tu kwani haliendani na hali halisi ya kile linachotokea badala yake tunaona ubabaishaji tu.

Vitu hivi vinaonekana ni vidogo lakini vinachangia kwa kiasi kikubwa kuporomosha soka letu. Viongozi hawasimami vema kwenye nafasi zao ndiyo maana kila kitu kinakwenda vululuvululu.

TFF hii ya Karia imekuwa na mapungufu mengi tofauti na ilivyokuwa imetarajiwa. Hiyo tu ya ligi kukosa mdhamini mkuu mpaka sasa inaonyesha dhahiri kuna kosa lilifanywa na wakubwa.

Ratiba kupinduliwapinduliwa kila mara huku baadhi ya timu zikiwa na viporo zaidi ya nane wakati ligi ikiwa inaelekea ukingoni, ni ishara kwamba soka letu linaendeshwa kwa mfumo wa bora liende.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here