Home Makala Makocha wana kazi kubwa na ngumu!

Makocha wana kazi kubwa na ngumu!

3199
0
SHARE

NA EZEKIEL TENDWA

BAADA ya Simba kutangaza kwamba inasafiri na kikosi chake kamili kwenda kushiriki michuano ya Mapinduzi, idadi kubwa ya wadau wa soka walimsifu kocha mkuu, Patrick Aussems, kwamba ameona mbali.

Walisema ameona mbali kwa maana kwamba mwishoni mwa wiki hii Simba wanakabiliwa na mchezo mgumu wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Saoura ya Algeria, hivyo isingekuwa busara kikosi kikakosa mechi za kujiweka sawa.

Walipofika Zanzibar wakaanza kucheza dhidi ya Chipukizi ya Pemba na kushinda mabao 4-1 kocha akitumia zaidi wachezaji wanaoanzia benchi isipokuwa Meddie Kagere, Nicholas Gyan pamoja na John Bocco ambaye aliingia kipindi cha pili.

Mchezo uliofuata yaani Jumapili iliyopita dhidi ya KMKM, kocha akaamua kuweka kikosi chake kamili mchezo ukamalizika kwa ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Rashid Juma na kutinga moja kwa moja hatua ya nusu fainali.

Hata hivyo, mchezo huo ni kama ulimalizika huku mashabiki wa Simba wakiwa na simanzi baada ya beki wao kisiki, Erasto Nyoni, kupata majeraha ambayo bila shaka yatamweka nje ya uwanja kwa muda usiopungua wiki tatu.

Ni ukweli ulio dhahiri kwamba hilo ni pigo kwa Simba, kwani Nyoni ni moja ya wachezaji tegemeo ndani ya kikosi hicho kutokana na namna anavyojituma huku akicheza namba zaidi ya moja, kitu ambacho hakiwezi kufanywa na wachezaji walio wengi.

Baada ya kuumia kwa Nyoni, kelele zimeanza huku Aussems akitupiwa lawama na baadhi ya wadau kwamba kutokana na kukabiliwa na michuano migumu ya Ligi ya Mabingwa hasa mchezo wao dhidi ya Saoura, hakutakiwa kuwatumia wachezaji wake muhimu Mapinduzi.

Yani walewale waliokuwa wakimsifu kocha huyo kwamba ana akili sana kwenda kuwapa wachezaji wake mazoezi ya kujiweka sawa, ndio hao hao wanaomponda kisa Nyoni kaumia.

Kama Nyoni asingeumia bado Aussems angesifiwa kwamba ana akili sana kuwaweka vijana wake sawa kwa kuwapanga wote mchezo huo dhidi ya KMKM, lakini kwa sababu mambo yamekwenda tofauti anaangushiwa jumba bovu.

Hivyo ndivyo walimwengu walivyo. Upande mmoja wanakuwa kama watakatifu na upande mwingine wanageuka kuwa maadui, hatuwezi kuukwepa ukweli huu.

Nasema hivyo kwa sababu baada ya lineup kutoka mapema na kuonekana Aussems amepanga kikosi kazi, mashabiki wa Simba walionekana kufurahi sana na kusema ni jambo jema kwani mchezo huo ungeweka utayari wa miili ya wachezaji wao lakini sasa tunasikia mengine.

Kama Nyoni asingeumia na Simba wakaonyesha kandanda maridadi na kuibuka na ushindi mnono, kila mmoja angeendelea kumsifu Aussems kama walivyoanza baada ya kutangazwa kwamba anasafiri na kikosi kamili kushiriki Mapinduzi.

Kuumia kwa mchezaji si lazima akiwa kwenye mechi. Hata kwenye mazoezi mchezaji anaweza akaumia hivyo kilichotokea kwa Nyoni ni kama bahati mbaya na kilichopo ni kuanza kuipa sapoti Simba kuelekea mchezo wao dhidi ya Waarabu, kwani wachezaji waliopo wanaweza wakavaa viatu vyake.

Hakuna shaka kwamba uzoefu wa Jjuuko Murushid unaweza kuwasahaulisha kabisa mashabiki wa Simba pengo la Nyoni, kwani beki huyu amekuwa mhimili mkubwa hasa timu yake ya Taifa ya Uganda.

Ameumia Shomari Kapombe lakini aliowaacha wamefanya vizuri sasa Nyoni naye ameumia, bila shaka aliowaacha wataendelea kumwakilisha vizuri.

Hii ndiyo maana halisi ya kuwa na kikosi kipana, kwamba mmoja akipata matatizo wengine wanapambana kuhakikisha mambo yanakwenda sawa. Haina maana kusema kikosi kipana halafu mchezaji mmoja akiumia wadau wanatafuta pa kwenda kujificha.

mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here