SHARE

LONDON, England

TANGU kuanza kwa msimu huu, winga wa timu ya Taifa ya Ubelgiji na Chelsea, Eden Hazard, amekuwa katika kiwango kizuri, amefunga mabao 10 na kutoa asisti 10 kwenye michezo 21 ya Ligi Kuu England.

Winga huyo mwenye miaka 27, alijiunga na Chelsea mwaka 2012, akitokea Lille ya Ufaransa na tangu hapo amejitambulisha kama ni mmoja wa wachezaji bora duniani kwa sasa, amecheza jumla ya michezo 229 ya Ligi Kuu England na kufunga mabao 79.

Hazard alishinda tuzo ya Mchezaji Bora wa msimu 2013/14, pia akiingia kwenye kikosi bora cha msimu mara nne kwa vipindi tofauti.

Kiwango chake kimekuwa gumzo Ulaya na kuzivutia baadhi ya timu kama Real Madrid, Barcelona, Juventus, Bayern Munich na PSG kuhitaji saini yake kila dirisha la usajili linapofunguliwa.

Lakini hivi karibuni, Chelsea ilifanikiwa kunasa saini ya Christian Pulisic wa Borrusia Dortmund, huku akielezwa kuwa amesajili ili kuziba pengo la hazard, anayetajwa kuondoka.

Licha ya Pulisic kusajiliwa, bado kuna uwezekano timu hiyo ya London kusajili winga mwingine. Makala haya yanakuletea wachezaji watano ambao wanaweza kuziba nafasi ya Hazard kama ataamua kuondoka Chelsea.

WILFRIED ZAHA

Bila kificho, Zaha ni mmoja wa wachezaji ambao wana uwezo mkubwa sana wanaocheza nje ya timu sita kubwa za Ligi Kuu England, kwa kiwango chake anaweza kuwa mchezaji muhimu ndani ya klabu hizo.

Zaha alicheza mchezo wake wa kwanza na Crystal Palace msimu wa 2009/10 na baadaye alijiunga na Manchester United mwaka 2013, ambako alishindwa kuonyesha kiwango kizuri na kurudi kwa mara nyingine kukipiga na Crystal Palace.

Tangu arejee ndani ya kikosi hicho, amekuwa mmoja wa wachezaji bora na wenye uwezo mkubwa, huku akizivutia timu kubwa kuhitaji saini yake kwa mara nyingine tena.

Kama Hazard akiondoka ndani ya Stamford Bridge, kuna uwezekano mabosi wa Chelsea wasiende mbali zaidi ya kugonga hodi kwa majirani zao kuhitaji saini ya Zaha.

HIRVING LOZANO

Winga huyo raia wa Mexico, amekuwa katika kiwango cha juu tangu msimu uliopita, huku akionyesha kiwango kikubwa kwenye fainali za Kombe la Dunia na klabu yake ya PSV tangu kuanza kwa msimu huu.

Lozano ana kasi kubwa, maarifa na hatari kwenye umaliziaji, msimu uliopita aliisaidia PSV kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Uholanzi, akifanikiwa kufunga mabao 17 na kutoa asisti 11.

Msimu huu tayari amefanikiwa kufunga mabao saba na kutoa asisti moja katika michezo nane ya kwanza ya Ligi Kuu ya Uholanzi.

Winga huyo mwenye miaka 23 alihusishwa kujiunga na Chelsea katika dirisha hili la usajili, kwa hiyo anaweza kuwa mbadala sahihi wa Hazard kama ataondoka Chelsea.

LORENZO INSGINE

Maurizio Sarri aliwatengeneza wachezaji wengi wazuri alipokuwa katika kikosi cha Napoli na Lorenzo Insigne ni mmoja wa wachezaji bora kwenye historia ya kocha huyo.

Insigne ana uwezo wa kukokota mpira, kupiga pasi na huonekana bora zaidi anapocheza nyuma ya straika, japo kuwa ni mchezaji anayeweza kucheza sehemu tofauti uwanjani.

Tayari amefanikiwa kufunga mabao sita na kutoa asisti moja katika michezo nane ya Ligi Kuu Italia msimu huu, uwepo wa Sarri unaweza kuwa msaada mkubwa kwake sababu aliwahi kufanya naye kazi Napoli kwa kipindi cha miaka minne.

Kwa msimu hufunga mabao zaidi ya 10 na kutoa asisti zaidi ya tano, anaweza kuziba nafasi ya Hazard kama Chelsea itamhitaji kiungo huyo raia wa Italia mwenye miaka 26 hivi sasa.

FLORIAN THAUVIN

Winga huyo wa Ufaransa alijiunga na Newcastle mwaka 2015, lakini alishindwa kutamba ndani ya Ligi Kuu England aliyoishia kucheza michezo 13 tu.

Alitumia muda wa miezi sita kwa mkopo ndani ya Magpies kabla ya kurejea kwa mkopo katika klabu yake ya zamani ya Marseille, ambayo ilimsaini jumla mwaka 2017.

Thauvin alifunga mabao 41 katika michezo 94 aliyocheza akiwa na jezi ya Marseille, huku akifanikiwa kushinda tuzo ya Mchezaji Bora wa mwezi mara tatu.

Kiwango chake alichokionyesha akiwa na Marseille kilimshawishi Kocha wa timu ya Taifa ya Ufaransa, Didier Deschamps, kumjumuisha katika kikosi kilichokwenda kushiriki fainali za Kombe la Dunia mwaka huu.

Uwezo wa kupiga pasi, kukokota mpira na kufunga mabao vinaweza kuwashawishi Chelsea kuhitaji saini yke kama Hazard ataamua kuikacha klabu hiyo.

GARETH BALE

Winga huyo wa Wales ni mmoja wa wachezaji bora duniani hivi sasa, tena anaweza kuwa mbadala sahihi wa Hazard bila matatizo yoyote.

Licha ya kutokea Southampton ambayo alijiunga nayo mwaka 1999, wengi walimfahamu winga huyo alipojiunga na Tottenham mwaka 2007 kucheza nafasi ya beki wa kushoto.

Msimu 2012/13 alishinda tuzo ya Mchezaji Bora wa msimu huo, huku kiwango chake kikiwavutia Real Madrid kulipa pauni milioni 85 kupata saini yake mwaka 2013.

Ingawa majeraha yamekuwa yakimrudisha nyuma, lakini anapokuwa katika kilele cha ubora wake, kila mmoja atajua kutokana na kile atakachokifanya uwanjani kama ilivyotokea katika mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Liverpool, alipofunga mabao mawili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here