Home Michezo Kimataifa VITA NI VITA

VITA NI VITA

1989
0
SHARE

*Rekodi zinaongea, Emery nyumbani, Solskjaer ugenini

LONDON, England

HAKUNA anayependa kuona timu yake inafungwa, haikuwa rahisi kwa Manchester United kupindua matokeo dhidi ya PSG, baada ya kushinda mabao 3-1, huku ikikumbukwa mabingwa hao wa zamani wa England walipoteza mchezo wa kwanza kwa mabao 2-0.

Wakati ambao mashabiki wa Manchester United wamejawa na nyuso za furaha, mambo hayakuwa mazuri kwa Arsenal, ambao walikubali kichapo cha mabao 3-1 dhidi ya Rennes katika mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 bora ya Ligi ya Europa huko nchini Ufaransa.

Arsenal inabidi washinde mabao 2-0 mchezo wa marudiano ambao utafanyika kwenye Uwanja wa Emirates wiki ijayo, lakini kabla ya mechi hiyo, leo watakuwa na kibarua dhidi ya Manchester United katika uwanja huo.

Mara ya mwisho timu hizo zilipokutana kwenye mchezo wa Kombe la FA ndani ya Uwanja wa Emirates, vijana wa Ole Gunnar Solskjaer waliondoka na ushindi wa mabao 3-1 na kuiondosha Arsenal katika michuano hiyo.

Lakini safari hii kocha wa Arsenal, Unai Emery, amesema kuwa atafanya juu chini kuhakikisha timu yake inabakisha pointi tatu ndani ya Uwanja wa Emirates.

Arsenal wameshinda michezo nane ya Ligi Kuu England ya hivi karibuni ambayo imechezwa kwenye Uwanja wa Emirates.

Emery anadai kuwa licha ya Manchester United kuwa kwenye fomu nzuri, hilo halimtishi, ila amepanga mbinu za kukizuia kikosi hicho kilichotoka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya PSG.

“Manchester United wapo kwenye kiwango cha juu mno, wametoka kushinda mchezo mgumu, lakini hilo halifanyi tushindwe kupata ushindi dhidi yao.

“Tupo nyumbani, tutajaribu kucheza kwa mbinu tofauti ili kuweza kushinda mechi hiyo, tunataka kuwafurahisha mashabiki wetu,” alisema kocha huyo.

Arsenal watakosa huduma ya kiungo wao, Lucas Torreira, ambaye alipata kadi nyekundu mchezo uliopita dhidi ya Tottenham ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1.

Nao Manchester United chini ya chini ya Solskjaer hawajafungwa wala kutoa sare mchezo wowote ugenini tangu kocha huyo achukue mikoba ya Jose Mourinho Desemba mwaka jana.

Hata hivyo, kocha huyo raia wa Norway alidai kuwa licha ya kikosi chake kupata ushindi dhidi ya PSG, hawawezi kuidharau Arsenal, ambayo imetoka kupoteza kwa Rennes huko Ufaransa.

Solskjaer alikwenda mbali zaidi kwa kudai kuwa timu yake imekamilika baada ya kurejea kwa baadhi ya wachezaji ambao walikuwa na majeraha na kukosa michezo iliyopita.

“Ukurasa wa PSG umeshafungwa, tuna mchezo mwingine ugenini mgumu na muhimu kwetu dhidi ya Arsenal, wana kikosi kizuri, hatuwezi kudharau kisa walifungwa mechi iliyopita.

“Anthony Martial yupo vizuri na tayari kwa mchezo huo, pia, Nemanja (Matic) na Ander (Herrera) wote wamefanya mazoezi na kuonyesha matumani makubwa kuelekea mechi hiyo,” alisema Solskjaer.

Katika michezo mitano ya hivi karibuni timu hizo zilipokutana, Arsenal wameshinda mara moja, huku Manchester United wakishinda mara tatu na kutoa sare moja.

Lakini rekodi za jumla, wenyeji wa mchezo wa leo kwenye Uwanja wa Emirates wameshinda mara 82, Manchester United mara 99 na kutoa sare 48.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here