Home Habari YANGA SC YATUPWA NJE NA ZANACO, YAANGUKIA SHIRIKISHO

YANGA SC YATUPWA NJE NA ZANACO, YAANGUKIA SHIRIKISHO

445
0
SHARE

NA CLARA ALPHONCE,

WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga, jana ilikua kama bahati mbaya kwao baada ya kutolewa na Zanaco kwenye michuano hiyo na kujikuta ikiangukia kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, licha ya kucheza kandanda safi na lakuvutia.

Yanga walitolewa kwenye michuano hiyo baada ya kutoa suluhu ugenini katika Uwanja wa Mashujaa uliopo jijini Lusaka nchini Zambia.

Katika mchezo wa awali uliochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, timu hizo zilitoa sare ya 1-1.

Kwa matokeo hayo, Zanaco sasa wanaingia hatua ya robo fainali ya michuano hiyo kwa jumla ya mabao 1-1 lakini wakiwa na bao la ugenini lililowapa faida ya kusonga mbele.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara walianza mpira huo kwa kasi na kufanikiwa kumiliki mpira kwa kiasi kikubwa katika vipindi vyote lakini juhudi zao hazikuwawezesha kupata bao.

Kipindi cha kwanza wachezaji; Hassan Kessy, Goefrey Mwashiuya na Haji Mwinyi, kama wangekuwa makini wangeweza kupata bao la mapema baada ya kugongeana hadi golini mwa Zanaco lakini wakashindwa kumalizia.

Zanaco ambao walionekana kuitafuta sare kwa kucheza kwa kujihami zaidi katika mchezo huo walikuwa wakifanya mashambulizi ya kushtukiza na kupelekea kipindi cha kwanza kufanya mashambulizi makubwa matatu ambayo hayakuzaa matunda.

Kipindi cha pili Yanga walifanya mabadiliko kwa kumtoa Mwashiuya na kumwingiza Emmanuel Martin ambaye aliongeza uhai katika timu na kufanya mashambulizi mengi zaidi langoni mwa Zanaco lakini hakuna bao lililopatikana.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi, aliliambia Dimba kwamba, katika mchezo huo walijaribu kubadili mbinu tofauti na zile walizotumia katika mechi ya awali lakini kwa bahati mbaya hawakuweza kufanikiwa.

“Tulipocheza nao mara ya kwanza tuliwasoma vizuri na kukaamua kubadili mfumo wetu, tulifanikiwa kwa kiasi pia tuliweza kumiliki mpira na kucheza vizuri zaidi na tulijiamini, lakini ndio hivyo tumeshindwa kupata bao,” alisema Mwambusi.

Ushindi huu unaifanya Zanaco iendeleze rekodi ya kuitupa nje Yanga kwenye michuano ya Afrika, baada ya mwaka 2006 pia kuwatoa katika hatua kama hii ya Ligi ya Mabingwa kwa jumla ya mabao 3-2, wakishinda 2-0 Lusaka baada ya kufungwa 2-1 Dar es Salaam.

Yanga sasa itamenyana na timu iliyofuzu hatua ya 32 Bora ya Kombe la Shirikisho kuwania tiketi ya kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo, wakati Zanaco inakwenda moja kwa moja hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa.

Kikosi cha Yanga leo kilikuwa; Deo Munishi ëDidaí, Hassan Kessy, Mwinyi Hajji, Kevin Yondan, Vincent Bossou, Justin Zulu, Thabani Kamusoko, Haruna Niyonzima, Simon Msuva, Obrey Chirwa na Geoffrey Mwashiuya/ Emmanuel Martin dk62. Zanaco; Toster Sambata, Ziyo Tembo, George Kilufya, Zimeselema Moyo/, Chongo Chirwa, Saith Sakala, Taonga Bwembya, Ernest Mbewe, Boyd Musonda, Attram Kwame na Augustine Mulenga.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here