SHARE

LONDON, England


PAMOJA na ukali wake wa kucheka na nyavu, kila unapofika mwezi wa nane, straika Harry Kane ni nyoka wa kibisa. Hana madhara kabisa!

Mkali huyu wa mabao wa Tottenham, aliyebeba kiatu cha ufungaji bora kwenye msimu miwili mfululizo (2015-16 na 2016-17), ana rekodi mbovu ya kutofunga bao katika mechi anazocheza mwezi wa nane.

Unaweza usiamini, lakini ukweli ni kuwa, Kane hana madhara kabisa kwenye Premier League, ndani ya mwezi huu.

Sare ya bao 1-1 waliyoipata Spurs dhidi ya Burnley, wikiendi iliyopita, imemfanya Kane aendeleze mkosi wake wa kutocheza na nyavu mwezi Agosti.

Katika michezo 13 ya Premier League, aliyocheza tangu aanze soka la kulipwa, sawa na dakika 898, Kane hajafanikiwa kutumbukiza mpira kimiani.

Kwenye michezo hiyo, Kane amepiga jumla ya mashuti 44, huku 10 tu yakilenga lango. Mengine yote aliyapeleka kule Juma Mahadhi alipoupeleka mpira wake wa penalti alioupiga dhidi ya Simba.

Msimu huu, kwenye michezo miwili aliyocheza mpaka sasa, amepiga jumla ya mashuti 18. Nane dhidi ya Chelsea na 10 akipiga dhidi ya Burnley. Idadi hiyo imemfanya awe mchezaji wa kwanza kupiga mashuti mengi ndani ya mwezi Agosti, bila kufunga bao.

Lakini baada ya mwezi huu kupita, Kane huwa binadamu tofauti kabisa. Wastani wake wa kufunga huwa mabao matatu kwenda juu.

Na akifika Oktoba, kasi huongezeka maradufu, ambapo hufikisha wastani wa mabao 9 kwa mwezi, kiasi cha kumfanya abebe kiatu cha mfungaji bora mwisho wa msimu.

Kwa wastani huo, takwimu zinaonyesha kuwa, Kane hutumia miezi mitatu kwanza kuseti mitambo yake, kisha kuanza kuifyatua mpaka mwisho wa msimu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here