Home Makala RONALDO, ICARDI, FYEKELEA MBALI, PIATEK BABA LAO

RONALDO, ICARDI, FYEKELEA MBALI, PIATEK BABA LAO

7521
0
SHARE

MILAN, Italia

KRZYSZTOF Piatek. Hili jina umelisikia wapi? Hujawahi? Basi sikulaumu.

Kwa sababu gani haupaswi kulaumiwa kutomjua Piatek ni kwamba, si wewe tu ambaye humfahamu vyema huyu ‘muuaji’ na adui namba moja wa makipa Serie A, aliyetua Genoa, Juni mwaka huu.

Hata hivyo, lazima utakuwa umeliona tu sehemu jina lake kutokana na makali yake ya kuzifumania nyavu anayoyaonesha. Na huu huenda usiwe mwisho wake.

Straika huyo alifanikiwa kuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao katika mechi saba mfululizo za kwanza Serie A, hiyo ilikuwa ni wikiendi iliyopita, na alirudia tu kile alichokifanya Gabriel Batistuta msimu wa 1994/95.

Kwa sasa jamaa anaongoza kwa mabao Barani Ulaya, akiwa na mabao 13 aliyofunga katika mechi nane ambazo amecheza msimu huu, yakiwemo manne peke yake wakati Genoa ilipochuana na Lecce, kwenye Coppa Italia.

Ni nani hasa huyu Piatek?

Genoa ilimnasa Piatek, 23, kutoka timu ya Cracovia iliyopo Poland, kwa kitita cha pauni milioni 3.5, baada ya kuvutiwa na takwimu yake ya kufunga mabao 32 katika mechi 65.

Mshambuliaji huyo aliwahi kuitwa katika kikosi cha awali cha Poland kilichokuwa na wachezaji 35 kwa ajili ya kushiriki Kombe la Dunia mwaka huu, lakini alishindwa kupata nafasi ya mwisho.

Lakini kiwango cha kuzifumania nyavu alichokionesha akiwa Genoa, kilifanikisha Piatek aitwe timu ya taifa mwezi uliopita na kucheza dhidi ya Jamhuri ya Ireland.

Straika huyo amekuwa na wastani mzuri sana wa kufunga mabao, akimpita mpinzani wake wa karibu, Lorenzo Insigne kwa tofauti ya mabao matatu.

Anacheza soka la aina gani?

Makali yake asogeapo langoni mwa mpinzani msimu huu, yameshindwa kuelezeka. Imeelezwa kuwa, nyota huyo mwenye mabao tisa kwenye Ligi msimu huu, hana haja ya kuugusa mpira zaidi ya mara tatu ndio atikise nyavu.

Wikiendi iliyopita wakati kikosi chake kikibamizwa 3-1 na Parma, ni yeye aliyefunga bao la kufutia machozi, na alikaribia kufunga lingine ambalo lingemfanya afikishe mabao 10.

‘Unyama’ wake huo mbele ya makipa umetokana na kwamba Piatek alivyokuwa mdogo alivutiwa sana na straika wa zamani wa AC Milan, Filippo Inzaghi, na ni kweli wanafanana namna ya kutengeneza nafasi na kuwatoroka mabeki katika muda sahihi.

Wengine tayari wameshamfananisha na Harry Kane, kama mshambuliaji ambaye si hatari peke yake, pia ni mfungaji wa uhakika na anajua kujitenga kwenye nafasi muhimu.

Kocha wake katika timu ya Genoa, Davide Ballardini, anapendezwa sana na uchezaji wa Piatek, akieleza kwamba nyota wake huyo si tu mfungaji mzuri, bali anajituma, ana ushirikiano na pia haoni shida kurudi nyuma kukaba.

Lakini, kocha huyo anasema haoni kama huu ni muda sahihi wa kukaribisha presha nyingi kwa staa wake huyo, ingawa anaamini atakuwa mchezaji bora zaidi.

Barcelona, Piatek? Kuna kitu

Siku hizi tetesi za usajili huibuka na mchezaji anayefanya vizuri kwa wakati huo, kama alivyo Piatek.

Piatek anahusishwa na timu za Barcelona ya Hispania pamoja na Bayern Munich, ambayo inasaka mrithi wa Robert Lewandowski.

Ni wazi Piatek anataka kutua kwa miamba mikubwa ya soka duniani, kwani hivi karibuni alihojiwa kuhusu Barcelona, lakini alidai haamini kama tetesi hizo ni za kweli, ingawa alizisikia.

Kwa upande wa Genoa, wao wameonekana kukerwa na taarifa hizo, lakini kwa jinsi Piatek anavyozitikisa nyavu kwa moto wa dizeli, itakuwa ngumu tetesi hizo kupotea.

Kama bado hujamtazama Piatek, hebu zisubiri mechi za Poland dhidi ya Ureno na Italia zitakazochezwa hivi karibuni.

Usisahau, jina lake ni Krzysztof Piatek.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here