Home Funguka/Mapenzi AARON KALAMBO: Nimeshaumizwa sana na mapenzi

AARON KALAMBO: Nimeshaumizwa sana na mapenzi

1979
0
SHARE

NA MWAMVITA MTANDA

KARIBU tena katika ukurasa wetu wa maisha nje ya soka, ambapo leo tunaye kipa wa Maafande wa Tanzania Prisons, Aaron Kalambo, ambaye aliwahi pia kukipiga Polisi Dodoma.

Ukurasa huu unakupa fursa ya kufahamu maisha mengine wanayoishi mastaa wa familia ya soka, ukiachilia mpira ambao umewatambulisha zaidi.

Yafuatayo ni mahojiano ya DIMBA na kipa huyo tegemeo wa Tanzania Prisons.

DIMBA: Watu wangependa kujua uwapo nje ya soka wewe ni mtu wa aina gani?

KALAMBO: Mimi ni mcheshi sana na ninapokuwa na marafiki zangu lazima niwavunje mbavu kwa stori za vichekesho. Nje ya soka mimi hupenda kutumia muda wangu kupumzika baada ya mazoezi na kucheza gemu.

DIMBA: Mashabiki wangependa kujua unaishi wapi na kama unakaa na familia.

KALAMBO: Naishi Mbeya ndani ya kambi ya Jeshi la Magereza na kwa umri wangu bado sijaanzisha familia, ingawa mipango hiyo haiko mbali.

DIMBA: Unapenda mwanamke wa aina gani?

KALAMBO: Mimi ni mgonjwa kwa mwanamke mwenye rangi nyeupe na umbo la wastani. Hata mke nitakayemuoa nadhani hatakosa sifa hizo, ingawa kubwa zaidi ni tabia njema na kuwa mcha Mungu.

DIMBA: Maisha yako ya ndoa ungependa upate watoto wangapi?

KALAMBO: Kwa hali ya maisha ilivyo, nadhani wawili ingependeza zaidi na kama Mungu akipenda nitaomba wa kwanza awe wa kike, ili nimuenzi mama yangu mzazi ambaye alifariki mimi nikiwa mdogo.

DIMBA: Unajua kupika na ulijifunza wapi?

KALAMBO: Najua kupika vizuri sana, nilijifunza tangu nikiwa darasa la tatu na chakula changu cha kwanza kupika ilikuwa ni ugali. Siku ya kwanza nilisonga ugali lakini sikukata tamaa, nikaendelea kujifunza mpaka sasa mimi ni mjuzi mzuri wa mapishi.

DIMBA: Nani alikufundisha kupika?

KALAMBO: Maisha ya kuachwa yatima bila mama nikiwa mdogo yalinilazimu kujifunza kupika ili kufanya maisha yaende.

DIMBA: Ratiba yako ya chakula ikoje kwa siku?

KALAMBO: Mimi napenda kunywa chai na chapati kila asubuhi na supu au mayai ya kukaanga. Msosi wangu wa mchana napenda kula ugali wa dona, dagaa na mboga za majani, lakini usiku napenda sana wali nyama na mboga za majani. Kinywaji changu kikubwa ni juisi ya embe.

DIMBA: Wewe ni mpenzi wa suruali za kitambaa?

KAlAMBO: Daah! Sijawahi kabisa kuvaa suruali za kitambaa. Mimi vazi langu kubwa ni tisheti na jinzi na pensi.

DIMBA: Matumizi makubwa ya mshahara wako ni nini?

KALAMBO: Mimi nimewekeza zaidi kwenye kilimo, kwani ndicho kitu ambacho kimekuwa kikiniongezea mapato.

DIMBA: Kabla ya kuibukia kwenye soka ulipanga uwe nani?

KALAMBO: Ningekuwa daktari, sema tu nilifeli shule.

DIMBA: Umeshawahi kuumizwa na mpenzi wako?

KALAMBO: Daaah! nimeshaumizwa zaidi ya mara sita mpaka nikaanza kuyachukia mahusiano, lakini niliye naye sasa tunaenda sawa.

DIMBA: Ukistaafu soka unataka uwe nani?

KALAMBO: Nitakuwa mfanyabiashara mkubwa wa viazi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here