Home Makala Abasirim Chidiebere: Aggrey Morris alitaka kuniua

Abasirim Chidiebere: Aggrey Morris alitaka kuniua

606
0
SHARE
Abasirim Chidiebere

NA ZAINAB IDDY,

SOKA ni mchezo wa furaha, amani na upendo. Pale unapogeuka uadui uwanjani ni jambo la hatari kwa wachezaji. Straika wa kimataifa wa Stand United, Abasirim Chidiebere, kamwe hatamsahau beki shupavu wa Azam FC, Aggrey Morris, kwa kitendo alichomtenda kwa kumfanyia rafu mbaya ambayo imemfanya kuwa nje ya uwanja kwa wiki sita.

Chidiebere ambaye ni raia wa Nigeria, aliumizwa na Aggrey Oktoba 12 mwaka huu wakati wa mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara baina ya Stand United na Azam mchezo uliochezwa Uwanja wa CCM Kambarage na kumalizika kwa ‘Wapiga debe’ hao wa Shinyanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Straika huyo anamtuhumu Aggrey kwa namna alivyomfanyia ukatili wa kumchezea rafu iliyomsababishia kuvunjika taya na kuwekwa nyaya maalumu kuzuia meno yasitoke huku akiendelea kula kwa kutumia mrija.

DIMBA limefanya mazungumzo na straika huyo kujua mwendelezo wa afya yake baada ya kukumbwa na ajali hiyo akielezea masikitiko yake kwa kufanyiwa kitendo hicho alichokiita si cha kiungwana.

DIMBA: Pole kwa majeraha uliyoyapata.

Chidiebere: Asante kikubwa nashukuru bado navuta pumzi.

DIMBA: Unaweza kuelezea tukio la kuumizwa lilikuwaje?

Chidiebere: Naumia sana ninapofikiria  tukio lile kwani sikudhani mchezaji mkubwa mwenye heshima katika soka la Tanzania kama Aggrey Morris angeweza kunifanyia kitu kama kile kwa makusudi wakati sina ugomvi naye.

Ninachokumbuka tulikuwa tunawania mpira kama ilivyo kawaida ya straika na beki lakini ghafla nikashtukia napigwa kiwiko na kuanguka nikiwa nagalagala nikashangaa anainua miguu na kunikanyaga kama njia ya kunikomesha. Baada ya hapo sikujua kilichoendelea kwani nilipoteza fahamu na kujikuta nipo kwenye chumba cha wagonjwa nikipatiwa huduma ya kwanza na madaktari.

DIMBA: Ilikuwaje baada ya hapo?

Chidiebere: Nilipozinduka nakujiona nipo kwenye chumba nikagundua nilikuwa nimepoteza fahamu kwani niliwaona madaktari pamoja na viongozi wakiwa pembeni yangu, baada ya kufumbua macho nilisikia wakiambiwa watoke nje ili matibabu yaendelee, kiukweli namshukuru Mungu kuendelea kuwa hai mpaka leo.

DIMBA: Kabla ya Aggrey kukuchezea rafu ulishawahi kuwa na tatizo lolote ambalo linasababisha kuzimia?

Chidiebere: Hapana, katika maisha yangu sijawahi kuzimia, hii ni mara ya kwanza ndiyo maana mara kwa mara namshukuru Mungu kwani sidhani kama nilitakiwa kuendelea kuvuta pumzi kama si mapenzi yake.

DIMBA: Alichokifanya Aggrey kwako ni mchezo au mlikuwa na ugomvi nje ya uwanja?

Chidiebere: Katika vitu nisivyovipenda katika maisha yangu ni kukwazana na mtu na hata kama kuna nililomkosea anapaswa kuniambia si kunifanyia jambo kama hili lililohatarisha maisha yangu.

DIMBA: Kwa maana hiyo unafikiri Aggrey alikusudia jambo baya kwako?

Chidiebere: Ndiyo, tena naweza kusema alipanga kuniua ila Mungu hakuwa upande wake, nashangaa kwanini hadi sasa hakuna jambo lolote la kisheria lililochukuliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

DIMBA: Unafikiri TFF walipaswa kufanya nini juu ya hili.

Chidiebere: Michezo ya kibabe na rafu zisizo za michezo kwa Aggrey hazikuanza leo, nafikiri unakumbuka yaliyomkuta Okwi, nakumbuka alifungiwa baadhi ya mechi lakini adhabu hiyo haitoshi.

DIMBA: Adhabu gani anastahili?

Chidiebere: Kufungiwa maisha kwani kama ameweza kufanya kwa Okwi aliyepoteza fahamu akaja kwangu nimepoteza fahamu na kunivunja taya ipo siku atakuja kufanya jambo litakalosababisha mchezaji kupoteza  uhai.

DIMBA: Unafikiri kwanini TFF wamekuwa kimya hadi sasa?

Chidiebere: Kwa kuwa sichezi katika timu zenye faida kwao kwa maana Yanga na Simba inakumbukwa yalipomkuta Okwi waliingilia kati na kutoa adhabu, mbona kwangu wapo kimya, je, angekuwa mchezaji wa timu zao wangefanya kama ilivyo sasa.

DIMBA: Kwa upande wa Azam na Aggrey tangu litokee jambo hilo wameshakujulia hali?

Chidiebere: Walikuja kuniona kambini mara baada ya kurejea hospitali na viongozi wa Azam waliahidi kunisaidia lakini hadi hivi sasa hakuna aliyenipigia simu hata kunijulia hali zaidi ya mabosi zangu Stand United wanaogharamia huduma zote za matibabu.

DIMBA: Unatibiwa hospitali gani na kwa mujibu wa daktari utakuwa nje kwa muda gani?

Chidiebere: Napata matibabu katika Hospitali ya Faha dental Clinic na nitakuwa nje ya uwanja kwa wiki sita huku kila siku nikitakiwa kuripoti kwa ajili ya uchunguzi.

DIMBA: Matabibu wanasemaje, taya zikikaa sawa unaweza kurejea uwanjani?

Chidiebere: Walichoniambia zimevunjika vibaya hivyo jibu kamili la kucheza au la litajulikana baada ya muda huo.

DIMBA: Kulingana na tatizo hilo jambo gani unadhani limevurugika?

Chidiebere: Kwanza mfumo wangu wa maisha, nilikuwa naongea lakini hivi sasa siwezi, nilikuwa nakula mwenyewe lakini tatizo hili natumia mirija, kikubwa zaidi nafikiria itakuwaje kama suala hili halitapona si ndio nitakuwa nimepata ulemavu, itakuwaje maisha yangu kwani mpira ndiyo kazi inayofanya familia yangu iweze kuishi vizuri.

DIMBA: Nini unachoweza kumwambia Aggrey kwa hivi sasa?

Chidiebere: Mpira ni mchezo wa furaha si vita, hata kama wachezaji watakuwa na ugomvi basi uishe nje ya uwanja  tunapoingia uwanjani tupo kazini.

Alifanya haya kwa Okwi, kwangu na hivi karibuni amefanya hivyo kwa Simon Msuva na Obrey Chirwa katika mechi yao na Yanga japo hao wawili hawajapata madhara kama sisi.

Siku zote beki bora anaweza kuwa ni yule anayezuia zaidi au kuisaidia timu yake kutofungwa kwa kuokoa au kuvuruga mipango ya wapinzani lakini si kwa sifa nyingi za kuwaumiza wengine.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here