SHARE

NA HENRY PAUL

JINA la beki, Abdallah Zahoro maarufu ‘Babeshi’, si geni masikioni mwa wapenzi wa soka nchini, hususan wa klabu ya Tukuyu Stars, Lipuli ya Iringa na RTC Kagera, kwasababu amezichezea timu hizo ambazo zilikuwa zikishiriki Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (sasa Ligi Kuu Bara) miaka ya 1980 mwishoni hadi 1990.

Beki huyo ambaye alikuwa anacheza safu zote za ulinzi, alisifika kutokana na aina ya uchezaji wake, kwani alikuwa kizingiti kikubwa kwa washambuliaji aliokuwa akikabiliana nao na kuwafanya wapate wakati mgumu kumpita.

Babeshi alistaafu kucheza soka ya ushindani msimu wa 2000/01 akiwa na klabu ya Lipuli ya Iringa.

Hivi karibuni DIMBA Jumatano, lilimtafuta mstaafu huyo wa soka na kufanya naye mahojiano kuhusiana na nafasi ya timu ya Taifa Stars baada ya kufungwa katika mchezo wa kwanza wa Kundi C michuano ya Kombe la Afrika mabao 2-0 na Senegal Jumapili iliyopita nchini Misri.

Katika mahojiano hayo Zahoro anatoa maoni yake akisema Taifa Stars licha ya kufungwa bado wanayo nafasi ya kusonga mbele katika hatua ya 16 bora endapo watajitahidi na kucheza kwa kujituma katika mechi mbili zilizobaki.

“Taifa Stars wanakabiliwa na mechi mbili dhidi ya Kenya na Algeria ambazo zina viwango bora lakini lolote linaweza kutokea kama wachezaji watacheza kwa bidii na kujituma.

“Katika mechi hizi mbili zilizobaki, kila mchezaji anatakiwa kutimiza majukumu yake katika nafasi anayocheza, ili kutowapa nafasi wapinzani kutawala mchezo na kuibuka na ushindi.

“Kwa upande mwingine, itategemea kocha Emmanuel Amunike katika upangaji wa kikosi chake kwasababu anatakiwa kupanga wale wachezaji wenye uzoefu na mechi za kimataifa na kuachana na wale ambao bado wanachipukia.

“Wachezaji kama Erasto Nyoni, Faridi Mussa na Frank Domayo, wana uzoefu mkubwa na mechi za kimataifa, hivyo ni vyema wakawepo katika mechi hizo mbili zilizobaki.

“Kocha Amunike anatakiwa kuchukulia mechi hizo mbili zilizobaki kama fainali na si kupanga kikosi cha wachezaji ambao hawana uzoefu na michuano ya kimataifa.

“Sasa hivi kilichobaki kwa kocha Amunike si kujaribu kila mchezaji kucheza, bali anatakiwa kuwachezesha wachezaji wenye uzoefu na mechi za kimataifa na wanaojituma uwanjani.

“Kama wachezaji watacheza kwa bidii na kujituma na kocha akawachezesha wachezaji wenye uzoefu na michuano ya kimataifa, nina imani kuwa Taifa Stars itashinda na kutinga katika hatua ya 16 bora.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here