Home Makala Afcon 2019: Joto ndio limeanza kuchanganya

Afcon 2019: Joto ndio limeanza kuchanganya

1408
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU

DROO ya makundi michuano ya Kombe la Mataifa Afrika, Afcon, itakayofanyika nchini Misri mwaka huu, hakika imeongeza kiwango cha joto na presha kabla ya kuanza kwa vita kati ya mataifa 24.

Michuano hiyo itaanza kutimua vumbi jijini Cairo, Misri, Juni 21 na kufikia tamati Julai 19, mwaka huu.

Hafla ya upangwaji wa makundi hayo iliyofanyika mwishoni mwa wiki hii huko Giza, Misri, pembezoni mwa sanamu maarufu ya Sphinx, ilimalizika huku makundi yaliyopangwa yakiwaacha wadau wengi na maswali ya kujiuliza.

Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ambayo ilijitutumua vilivyo katika hatua ya kufuzu, imepangwa kundi moja na timu za Algeria, Senegal na Kenya.

Kama ilivyokuwa hatua ya kufuzu, Taifa Stars itatakiwa kusuka mipango madhubuti ya kuzikabili timu hizo imara ilizopangwa nazo.

Kwanza, Taifa Stars inayoongozwa na mfungaji bora wa Ligi Kuu Ubelgiji, straika wa KRC Genk, Mbwana Samatta, itakuwa na kibarua kizito dhidi ya Senegal.

Senegal, katika viwango vya soka Afrika ni taifa linaloongoza kwa sasa, juu ya Tunisia.

Licha ya kuwa moja ya mataifa yaliyokuwa kwenye bakuli la kwanza la mataifa ya juu katika upangwaji wa makundi, Senegal hawana rekodi ya kutisha sana katika michuano ya Afcon.

Senegal hawajawahi kutwaa taji la michuano hiyo ambayo wameshiriki mara 14, wakiwa na rekodi ya kushiriki mfululizo kati ya mwaka 2002 hadi 2008.

Hata hivyo, Senegal ikiwa na staa wake anayekipiga Liverpool, Sadio Mane, watatarajiwa kuweka historia ya kutwaa taji la michuano hiyo kwa mara ya kwanza mwaka huu.

Baada ya Senegal, Taifa Stars itatazamiwa kuweka rekodi ya kuwaangamiza mabingwa wa zamani wa Afcon, Algeria.

Algeria ni moja ya mataifa makubwa ya Kiarabu katika soka barani Afrika, ikiwa na rekodi ya kubeba kombe hilo mara moja, sawa na timu za Morocco, Sudan na Tunisia.

Ikiwajumuisha wachezaji wengi nyota, Algeria itamtegemea zaidi winga wao, Riyad Mahrez, anayekipiga katika klabu ya Man City.

Kikwazo kingine cha Taifa Stars ni Kenya, taifa jirani ambalo lina uzoefu wa kutosha na michuano hiyo, ambapo hii itakuwa ni mara yao ya sita tangu waliposhiriki mara ya mwisho mwaka 2004, mashindano yaliyochezwa Tunisia.

Makundi mengine

Wenyeji wa michuano hiyo na mabingwa wa kihistoria (mataji saba), Misri, wamepangwa Kundi A sambamba na mabingwa mara mbili, DR Congo, Zimbabwe na Uganda.

Misri watatupa karata yao ya kwanza dhidi ya Zimbabwe jijini Cairo.

Kundi F limezijumuisha timu ya pili na ya tatu kwa mafanikio makubwa katika historia ya michuano hiyo, bingwa mtetezi, Cameroon na Ghana.

Timu hizo zinatarajiwa kuonesha ubabe wa kutosha kisoka, kutokana na mafanikio yao hivi karibuni.

Cameroon walinyakua taji lao la tano la Afcon mwaka 2017, watawania nafasi za juu dhidi ya mabingwa mara nne, Ghana, Benin na Guinea-Bissau.

Imezoeleka kuwa kila mashindano lazima yawe na ‘kundi la kifo’ na katika michuano hii, Kundi D ndio lenye balaa. Humo kuna timu za Morocco, Ivory Coast, Afrika Kusini na Namibia.

Nigeria walipangiwa Kundi B na timu za Guinea, Madagascar na Burundi. Huku Tunisia wakijipanga kuchuana dhidi ya Mali, Mauritania na Angola kwenye Kundi E.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here