SHARE

NA MWANDISHI WETU, LUBUMBASHI

LICHA ya kuruhusu kufungwa mabao 4-1 kutoka kwa TP Mazembe, lakini kipa wa Simba, Aishi Manula, amekuwa gumzo katika Mji wa Lubumbashi kutokana na kazi kubwa aliyoifanya.

Simba walikubali kichapo hicho mchezo wa Ligi ya Mabingwa hatua ya robo fainali uliochezwa Uwanja wa Stade TP Mazembe, jana nchini DR Congo.

Matokeo hayo yanaifanya Simba kutupwa nje ya michuano hiyo kwani katika mchezo wa kwanza uliochezwa nyumbani Jumamosi ya wiki iliyopita, timu hizo zilitoka suluhu ya 0-0.

Katika mchezo huo wa jana, Manula alifanya kazi ya ziada ambapo kama isingekuwa juhudi zake huenda Simba wangepokea kipigo kikubwa zaidi ya hicho.

Kipa huyo ambaye pia ni namba moja timu ya Taifa, Taifa Stars, aliokoa michomo hatari dakika ya 36, 42, 43, 49, 52, 73, 85 pamoja na 88 na kuacha gumzo kubwa.

Wakizungumza baada ya mchezo huo, baadhi ya mashabiki wa Mazembe walisikika wakisema inabidi Simba wamshukuru sana kipa wao kwani wangeondoka na kapu la mabao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here