Home Michezo Kimataifa AJAX V MAN UNITED… NI FAINALI YA VIJANA WA SOKA LA BURUDANI...

AJAX V MAN UNITED… NI FAINALI YA VIJANA WA SOKA LA BURUDANI DHIDI YA WAPAMBANAJI

464
0
SHARE

STOCKHOLM, Sweden

NI fainali ya Ligi ya Europa msimu huu baina ya Ajax Amsterdam na Manchester United.

Fainali ni neno jepesi. Hii ni zaidi ya fainali, ni dhambi kwa mdau wa soka kuikosa fainali hiyo itakayochezwa usiku wa leo nchini Sweden.

Ugumu wa pambano la leo unachagizwa kwa kiasi kikubwa na lengo la Man United la kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, sambamba na kuongeza taji jingine kabatini msimu huu, lakini cha kuzingatiwa ni kwamba Ajax ina kikosi cha vijana wadogo wanaojiamini na kusakata soka la kiwango cha hali ya juu kutokana na falsafa ya ‘Total Football’ iliyoanzia nchini Uholanzi.

Aidha, si rahisi kwa kocha wa United, Jose Mourinho, kukubali kichapo leo kutokana na hatari ya kukosa mkataba mpya na ongezeko la mshahara iwapo atashindwa kuipa timu taji la Europa.

Hii fainali ina maana kubwa kwa United kuliko inavyofikiriwa. Masuala ya mkataba wa jezi na kampuni ya Adidas, mapato ya msimu ujao na mishahara kwa wachezaji wao, kila kitu kitaathiriwa na kama watafanikiwa kubeba Kombe la Europa au la.

Wastani wa kiasi watakachovuna Man United kwenye fainali hii ni pauni milioni 70, zaidi ya pauni milioni 20 kutoka Adidas na 50 kwa kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini suala la fedha huenda lisiwe na maana kubwa kwa United zaidi ya kushiriki ligi ya mabingwa.

Ajax nao hawatakuwa na la kujitetea iwapo wataharibu leo. Licha ya kwamba wameshajikatia tiketi yao ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, wakishinda leo watafuzu moja kwa moja hatua ya makundi.

Vijana hao wameonesha uwezo mkubwa msimu huu, wataalamu wa soka wakisema ni wazi sasa Ajax imerudi kwenye falsafa zenyewe za mkongwe wa zamani wa Ajax na Barcelona, Johan Cruyff.

Kwanini wanasema hivyo? Ni baada ya kutinga fainali ya kombe la pili kwa ukubwa linalosimamiwa na Shirikisho la Soka barani Ulaya, kazi nzuri ya kocha Peter Bosz.

Kikwazo kikubwa kwao leo ni uwepo wa Mourinho pale United, mmoja wa makocha bora duniani. Wataweza kuhimili presha? Tujongee kibanda umiza tukashuhudie burudani ya soka la Ulaya.

NONDO MUHIMU

  1. Ajax na Manchester United zimekutana mara nne kwenye michuano ya Ulaya. Zote zikishinda mechi mbili (mechi mbili katika raundi ya kwanza ya Kombe la UEFA 1976/77 na mechi mbili za nyumbani na ugenini kwenye raundi ya 32 katika michuano ya Europa msimu wa 2011/12).
  2. Ajax imetwaa mataji sita katika fainali nane za mwisho za michuano ya Ulaya, ambazo waliwahi kucheza huku Red Devils wakifanya hivyo mara nne katika fainali sita.

iii. Ajax imepoteza fainali mbili za Ligi ya Europa kati ya tatu walizocheza hivi karibuni, wakiruhusu mabao saba kwenye mechi hizo.

Vikosi:

Man United: Romero; Valencia, Darmian, Blind, Jones; Fellaini, Herrera, Pogba; Lingard, Mkhitaryan, Rashford.

Ajax: Onana; Veltman, Sanchez, De Light, Sinkgraven; Klaasen, Schone, Ziyech; Younes, Dolberg, Traore.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here