Home Habari AJIB ATENGEWA DAU NONO MISRI

AJIB ATENGEWA DAU NONO MISRI

2872
0
SHARE

NA SALMA MPELI

KLABU ya Zamalek ya Misri imeanza harakati za kuimarisha kikosi chake, huku ikionyesha nia ya kuhitaji saini ya mshambuliaji tegemeo wa klabu ya Yanga na timu ya Taifa ya Tanzania, Ibrahim Ajib.

Taarifa ambazo DIMBA Jumatano ilizipata jana kutoka nchini Misri kutoka kwa wakala wa klabu hiyo aitwaye Misfer Al-Farhan, zinadai kwamba wamekuwa wakimfuatilia Ajib kwa muda mrefu tangu msimu wa mwaka jana akiwa na kikosi cha Simba, ambapo sasa dawati la ufundi limeona anaweza kuwepo kwenye mipango yao.

Moja ya kazi kubwa ambayo Zamalek wanahitaji kumpa Ajib ni kwa ajili ya michuano ya kimataifa kwa maana ya Kombe la Shirikisho ambapo timu hiyo inashiriki, huku Misri ikiwa imeingiza timu mbili nyingine ikiwa ni Al-Masry.

“Idara ya ufundi imeridhika na kiwango chake lakini kama unavyojua ni mchezaji mwenye mkataba na Yanga, kwa hiyo kuna taratibu zinafanyika ambazo zikiwa tayari mtazifahamu kwa maana ya klabu husika ila kwa sasa hatuwezi kusema sana.

“Mimi kama mtu ninayesimama kwa upande wa Zamalek, yapo majukumu ambayo nitayakamilisha ndani ya muda mfupi, ikiwemo kuja Tanzania kuanza mazungumzo na klabu yake ingawa kwa sasa nipo Dubai (Umoja wa Falme za Kiarabu).

“Nikirudi Misri nitakutana na uongozi wa Zamalek kisha kuendelea na hatua nyingine zinazokubalika kisheria na kitaratibu, imani yetu kama klabu ni kuona jambo hilo linafanikiwa mapema kadiri inavyowezekana kwa kuamini kwamba, menejimenti ya Ajib nayo itafanya sehemu yake,” alisema Al-Farhan.

Kuhusu kiasi cha fedha alichotengewa kama ada ya usajili, Al-Farhan alisema kwamba bajeti ya klabu ni Euro 50,000 (zaidi ya shilingi 131,000,000 za Kitanzania).

“Bajeti ya klabu ni Euro 50,000 ambazo ni fedha kwa ajili ya usajili wake pekee ila hapo haihusu fedha ya kumnunua kutoka Yanga kuja Zamalek,” aliongeza Al-Farhan.

Iwapo dili hilo litafanikiwa, Ajib atakuwa ameingia kwenye moja ya timu kubwa lakini timu yenye mafanikio katika bara la Afrika baada ya kufanikiwa kukusanya mataji 48, yakiwemo ya Misri kwenyewe na Afrika.

Mataji hayo ni pamoja na Ubingwa wa Misri ambapo imetwaa mara 12, Kombe la Misri (mara 25), Kombe la Mabingwa Misri (mara tatu), huku mataji mengine yakiwa ni Ligi ya Mabingwa Afrika mataji matano na Kombe la Shirikisho mataji matatu na sasa ikiwa na kikosi kipana chenye wachezaji 35.

DIMBA lilimtafuta Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa, kwa ajili ya kuzungumzia suala hilo lakini hakuweza kupatikana kwa wakati.

Kwa upande wake Ajib mwenyewe alipoulizwa juu ya ofa hiyo, alisema yeye binafsi hafahamu suala hilo na kama lipo pengine uongozi wa klabu yake watakuwa na taarifa.

“Sina taarifa juu ya suala hilo labda waulizwe viongozi wa Yanga,” alisema Ajib ambaye amesajiliwa na Yanga msimu huu akitokea kwa mahasimu wao Simba.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here