Home Habari AJIB AWAPELEKEA ‘HAT TRICK’ MAJIMAJI

AJIB AWAPELEKEA ‘HAT TRICK’ MAJIMAJI

977
0
SHARE

ABDUL MKEYENGE

STRAIKA wa Yanga, Ibrahim Ajib, amewapa matumaini makubwa mashabiki na wapenzi wa Yanga kwa kusema kuwa atahakikisha anawapa furaha nyingine wikiendi ijayo kwa kuifunga Majimaji kadiri iwezekanavyo, kwa vile anakwenda huko huku akiwa na kumbukumbu ya kuwafunga ‘hat trick’ Wanalizombe hao msimu wa 2015/2016.

Ajib aliyejiunga Yanga akitokea Simba, alieleza kuwa ana historia nzuri ya kuwafunga Majimaji na ingawa hii haifanyi iwe rahisi kwake kuwafunga tena, lakini amejipanga kufanya hivyo.

“Mechi itakuwa nzuri, lakini nitaingia uwanjani kupambana na Majimaji nikijivunia kuwa niliwahi kuwafunga mabao matatu (Hatrick) misimu miwili iliyopita. Nitaingia uwanjani nikiamini naweza kufanya kitu kingine kizuri, japo nafahamu wapinzani nao wana maandalizi,” alieleza.

Wakati akiwa Simba, Ajib aliwahi kuifunga Majimaji mabao matatu kwa maana ya ‘hat trick’ katika mechi ya mzunguko wa kwanza ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2015/2016, Simba ilipoibuka na ushindi wa mabao 6-1 Novemba, mwaka  2015, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mechi hiyo, Ajib alianza kufunga bao la kwanza dakika ya nane ya kipindi cha kwanza akiunganisha pasi iliyopigwa na beki wa kulia wa timu hiyo Emery Nimubona, baada ya kumtoka Ally Mohamed mlinzi wa kushoto wa Majimaji FC.

Mambo bado yaliendelea kumnyookea Ajib kwani dakika sita baadaye alipachika bao la pili akiunganisha krosi iliyopigwa na Mohamed Hussein Tshabalala. Goli hilo liliamsha kasi ya Ajibu kuanza kuitafuta ‘hat-trick’ kwa uchu.

Ndoto za Ajib kufunga goli la tatu kwenye mchezo huo zilitimia dakika ya 42 kipindi cha kwanza, baada ya kufanikiwa kufunga goli la tatu na kujihakikishia kuondoka na mpira.

Akizungumza na DIMBA Jumatano, Ajib amesema kuwa anaenda kukutana na Majimaji akiwa na morali ya hali ya juu na kuwataka wajiandae kuziacha pointi tatu japo watakuwa uwanjani kwao.

Straika huyo aliyeibuka shujaa wa Yanga katika mchezo uliopita dhidi ya Njombe Mji kwa kufunga bao pekee, alisema ni wakati wa Yanga kutulia na kuamini kuna kitu wanaenda kufanya katika mchezo huo na michezo mingine inayofuata.

Alisema anajisikia vyema kimwili na kiakili kwa ajili ya kuwavaa Majimaji na anaomba kocha wake, George Lwandamina, amwamini ili afanye kazi.

“Kama mchezaji najiona niko vizuri ndio maana unaweza kuona nilifunga bao la ushindi dhidi ya Njombe Mji na hiki ndicho kipindi cha kuwaambia na wapinzani wetu wanaofuata (Majimaji) kuwa nakuja huko nikiwa njema kabisa.

“Timu iko vizuri na kila mchezaji yuko vizuri, hivyo ni jukumu la kocha kumpa nafasi yule anayemuona anaweza kuisaidia timu kwa wakati gani.

“Ndani ya timu kuna ushindani na kila mmoja anataka kumshawishi mwalimu kwa ajili ya kucheza, sasa timu ikishakuwa katika hali hiyo ni lazima ushindi upatikane kwa vyovyote vile,” alisema Ajib.

Mchezo huo wa Ligi Kuu Bara unatarajiwa kuchezwa Jumamosi mwishoni mwa wiki hii kwenye Dimba la Majimaji mkoani Songea.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here