Home Makala Ajib hajaitwa Stars, haishtui sana

Ajib hajaitwa Stars, haishtui sana

1631
0
SHARE

NA ABDULAH MKEYENGE

NIMESOMA orodha ya majina ya wachezaji wa timu ya taifa Tanzania, jina la rafiki yangu, Ibrahim Ajib, limekosekana katika orodha hayo. Haijanishtua sana. Orodha hiyo ya wachezaji itaingia kambini hivi punde kujiandaa na mchezo wa Uganda.

Inavyoonekana kocha wa Stars, Emmanuel Amunike, kipindi hiki alichokuwa akiandaa majina ya wachezaji kuja kuyaweka wazi mbele ya wanahabari, hajapata presha na jina la Ajib.

Miezi kadhaa iliyopita angeweza kulikata jina la Ajib, lakini asingekuwa na amani moyoni mwake. Kuna sehemu angejibishia mwenyewe. Lakini sasa hajakutana na hali hii.

Kama nchi tuliamini mechi mbili za Cape Verde na mechi ya mwisho dhidi ya Lesotho, zilimhusu Ajib. Wakati ule alikuwa katika kilele cha ubora wake. Namba hazikudanganya.

Katikati ya michezo ya Cape Verde na Lesotho ndani ya Ligi Kuu Bara, Ajib Alisha ‘assist’ mara tisa. Hapa nchi ilimhitaji, lakini Amunike aliweka pamba masikioni na kupuuza.

Lakini tangu umalizike mchezo wa Lesotho na Stars kulala kwa bao 1-0, ndani ya Yanga Ajib ame’assist mara mbili tu. Mara moja ikiwemo juzi Jumapili kwenye mchezo na KMC.

Ukweli mchungu ni kwamba, rafiki yangu amepiga hatua nyingi za nyuma. Ndiyo maana hata Amunike hajakutana na wakati mgumu wa kushindana na moyo wake hivi sasa kama wakati ule alipomwacha na kila mtu kumshangaa.

Hata wakosoaji wanaomkosoa Amunike hivi sasa juu ya uteuzi huo, ni wachache wanaomkosoa kuhusu Ajib, lakini wengi wanamkosoa kwa kutowaita Paul Godfrey ‘Boxer’ na Salim Aiyee.

Amunike ana sababu nyingi za kujitetea kutomuita Ajib kipindi hiki. Kitendo cha Ajib kuingia na kutoka katika kikosi cha kwanza cha Yanga, ni sehemu inayompa Amunike kiburi na utetezi. Anajiona yuko sahihi.

Njia pekee ya ‘kumsuta’ Amunike ni Ajib kurudisha makali yake. Ni lazima afanye hivyo. Ifike muda Amunike atajiona anabishana na ukweli kama wakati ule. Lakini kwa ilivyo sasa, yote anayoambiwa Amunike kuhusu Ajib, yataingia sikio la kushoto, yanatokea sikio la kulia. Hawezi kumsikiliza mtu.

Naufahamu vyema uwezo wa Ajib. Kinachomtokea sasa ni mapito. Kuna siku ataamka tena katika ubora mkubwa na hizi ndoto za kila mmoja kumwona akitamba na jezi za timu ya taifa kama Yanga zitafika tu. Lakini pia, ni wakati wake kuamka usingizini kutupa shuka, kuchukua vifaa vyake na kukimbilia uwanja wa mazoezi. Ni hiki tu cha kufanya.

Lazima awe na malengo makuu matatu. Moja afanye mazoezi magumu. Pili afanye mazoezi magumu. Tatu afanye mazoezi magumu. Akifanya hivyo atarudi tena vinywani mwa watu na wengi watataka awepo Stars. Lakini kwa sasa Amunike ni mshindi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here