SHARE

NA SAADA SALIM


NYOTA wa Simba mwenye ufundi mwingi wa kuchezea mipira na kutengeneza mabao, Ibrahim Ajib, amesikia maneno ya chini chini kwamba ana mpango wa kuitosa klabu hiyo, akacheka sana kwa dharau.

Unajua alichosema baada ya hapo? “Nani aondoke Simba? Mimi? Thubutuu! Bado nipo nipo sana tu.”

Kwa kifupi amesisitiza kuwa kamwe hawezi kwenda kokote kwa sasa kama wengi wanavyodhani na badala yake amewaambia mashabiki wa Wekundu hao wa Msimbazi wajiandae kunyanyua kombe msimu huu.

Ajib amelazimika kuyasema hayo baada ya kuenea taarifa kuwa ana mpango wa kuikacha timu hiyo ambayo amekuwa nayo kwa kipindi kirefu, huku akihusishwa na kujiunga na mahasimu wao wakubwa, Yanga.

Akizungumza na DIMBA Jumatano, Ajib, ambaye ni mmoja wa washambuliaji wenye vipaji vya hali ya juu, alisema bado ana mkataba na Simba na mawazo yake kwa sasa ni kuisaidia klabu yake hiyo kutwaa ubingwa msimu huu.

“Bado nina mkataba na Simba kwa sasa, hivyo hizo taarifa nyingine zinazoenea huko mitaani mimi sizijui kabisa, kilichopo kichwani mwangu kwa sasa ni kuipigania timu yangu kutwaa ubingwa msimu huu na kuwafanya mashabiki wetu wafurahi,” alisema.

Akizungumzia mbio za ubingwa, ikizingatiwa kuwa mahasimu wao, Yanga pamoja na Azam wanawafukuzia kimyakimya, alisema licha ya kwamba hawakufanya vizuri katika michezo yao miwili ya mwisho ya mzunguko wa kwanza, hakuna kitakachowazuia kwenye mbio zao hizo za ubingwa.

“Lengo letu ni kutwaa ubingwa msimu huu na sisi hatuangalii nani yupo nyuma yetu, badala yake tunaangalia mbele ambapo tunataka kushinda michezo yetu yote ya mzunguko wa pili na hilo linawezekana kabisa,”  alisema.

Maneno hayo ya Ajib bila shaka yanajibu kiu ya mashabiki wake, ambao wamekuwa roho juu baada ya kuenea taarifa kwamba Yanga wanafanya mipango ya chini kwa chini ya kumchukua.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here