SHARE

LONDON, England
UNAPOTAJA majina ya walinzi bora wa upande kulia hivi sasa barani ulaya huwezi kulikosa jina la kinda Aaron Wan-Bissaka aliyezaliwa Novemba 26,1997 ambaye ghafla tu amepiga hatua kubwa kutoka Crystal Palace hadi Manchester United.


Wengi watajiuliza Wan-Bissaka ni nani ilikuwaje Man United wakatoa kiasi cha Euro milioni 50 kumnasa kinda huyo ambaye msimu uliopita akiwa na Palace alichukua tuzo za mchezaji bora wa klabu mara nne Machi, Agosti, Septemba na Oktoba .


Nyota huyo alianza safari yake katika soka akiwa na miaka 11 katika kikosi cha vijana cha Crystal Palace ambako amedumu kuanzia mwaka 2016 hadi 2019 alipoamua kuondoka na kutua katika kikosi cha Man United ili apate changamoto mpya.


Beki huyo mwenye umri wa miaka 21 anaevaa jezi namba 29 mgongoni akiwa na kikosi cha wakubwa cha Palace , tangu mwaka 2016 amecheza jumla ya michezo 42 akishindwa kufunga bao lolote.


Katika ngazi ya timu ya taifa, Wan Bissaka, amefanikiwa kucheza mchezo mmoja akiwa na jezi za timu ya taifa ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, chini ya miaka 20 huku akicheza michezo miwili na timu ya vijana ya England chini ya miaka 20 na michezo mitatu kikosi cha chini ya miaka 21.


Yafuatayo ni mambo matano ambayo huyajui kuhusu Aaron Wan Bissaka ambaye amekuwa gumzo katika dili lake la kutua katika kikosi cha Manchester United

Ndoto zake zilikuwa, Chelsea, Arsenal
Akiwa kinda alitamani kucheza katika klabu kubwa kama vile Chelsea na Arsenal huku Palace wakiwa chaguo lake la mwisho lakini kinyume na matarajio yake timu hizo zilimtosa na kujikuta akiangukia kwa Tai hao wa London ambao walimpa nafasi ya kufanya majaribio kwa miezi mitatu.
Aliikacha jezi ya DR Congo akaichagua England


Licha ya kuwa na uraia wa asili wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutokana na wazazi wake kuzaliwa taifa hilo lakini Wan-Bissaka, amegoma kulitumikia taifa hilo na kuamua kuvaa jezi za England, katika kikosi cha vijana chini ya miaka 20 na 21 ambako amecheza michezo mitano huku akiiwakilisha DRC katika mchezo mmoja pekee.
Ni shabiki wa Manchester United tangu utoto


Ni wachezaji wachache sana wanaofanikiwa kucheza timu wanazoshabikia tangu utoto , lakini ni bahati iliyoje kwa Wan-Bissaka ambaye amekuwa shabiki wa Manchester United tangu akiwa mdogo amekuwa akiifuatilia timu hiyo hivyo ni kama vile ameenda kufanya kazi .
Mshahara wake sasa ni mara tisa ya awali


Nyota huyo licha ya kuwa katika kiwango bora akiwa na kikosi na Palace, lakini alikuwa akipokea mshahara wa Euro 10000 kwa wiki, lakini baada ya kutua kwa mashetani wekundu tayari mshahara wake umepanda mara tisa ya ule wa awali na kufikia Euro 90000.
Kutoka straika hadi beki


Kila mtu ana malengo na mipango katika kile anachokiamini ndivyo ilivyo kwa beki huyo wa kulia ambaye alianza kucheza soka katika kikosi cha vijana cha Palace akiwa miaka 11, akicheza nafasi ya winga kabla mambo hayajageuka msimu 2016/17 alipobadilishwa nafasi na kuwa mlinzi wa kulia na kocha Frank der Boer.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here