SHARE
LONDON, England

MWENYEKITI wa zamani wa klabu ya Arsenal, Peter Hill-Wood, anaamini kuwa huu ndio wakati sahihi kwa kocha wa klabu hiyo, Arsene Wenger, kubwaga manyanga baada ya kudumu kwa miaka 22.

Hill-Wood, 82, aliamua kuachia majukumu kwa wengine mwaka 2013 na ndiye aliyemwajiri Wenger kuinoa Arsenal mwaka 1996.

Wenger amejikuta katika wakati mgumu zaidi msimu huu, hasa baada ya kubamizwa na Man City mara mbili ndani ya wiki moja, vichapo vyote vikiwa ni vya mabao 3-0.

Vipigo hivyo vilisababisha mtafaruku baina ya mashabiki huku bodi ya klabu ya Arsenal nayo ikionesha dhamira ya kusitisha ushirikiano wa kikazi na kocha huyo ifikapo mwisho wa msimu huu.

“Niwe muwazi, sipendezwi na kinachoendelea. Nafikiri kuna mabadiliko ya lazima yanayotakiwa kuchukuliwa. Wenger amefanya kazi nzuri sana ila naona muda wake wa kupumzika umewadia,” alisema Hill-Wood.

“Inasikitisha kuona mambo yanamwendea hivi, alikuwa anapendwa na wengi lakini kwa kukaa muda mrefu huku mambo yakiwa ovyo, imesababisha chuki kwa waliompenda,” aliongeza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here