Home Michezo Kimataifa Allardyce amtaka John Terry timu ya taifa

Allardyce amtaka John Terry timu ya taifa

505
0
SHARE

LONDON, ENGLAND

KOCHA mpya wa timu ya taifa ya England, Sam Allardyce, anatarajia kumuita kikosini beki wa zamani wa timu hiyo, John Terry, ambaye alijiuzulu kuitumikia timu hiyo miaka minne iliyopita.

Nyota huyo alichukua maamuzi ya kustaafu soka tangu mwaka 2012, baada ya mgogoro wake na Anton Ferdinand katika mchezo dhidi ya QPR ambao ulipigwa Oktoba 2011, kutokana na hali hiyo Chama cha Soka nchini England kilimshtaki beki huyo kabla ya kuchukua maamuzi ya kujiuzulu.

Mchezo wa mwisho nyota huyo kukipiga huku akiwa na timu hiyo ya taifa, ilikuwa Septemba 2012 dhidi Moldova na akaja kutangaza kujiuzulu timu hiyo mwezi mmoja baadaye. Hata hivyo, mchezaji huyo alitakiwa kulipa faini ya pauni 22,000 kutokana na tukio hilo.

Terry aliendelea kuwa na kiwango bora katika safu ya ulinzi, huku akiwa anakipiga katika klabu yake ya Chelsea na kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu nchini England katika msimu wa 2014-15.

Kocha huyo mpya wa timu ya taifa ya England, Allardyce amedai kwamba hadi sasa tangu mchezaji huyo ajiuzulu timu hiyo imekuwa na wakati mgumu katika safu ya ulinzi, hivyo amepanga kumrudisha mchezaji huyo kikosini kwa ajili ya kurudisha heshima ya taifa.

“Najua kikosi kina matatizo, hasa katika nafasi ya ulinzi, hivyo ninatarajia kufanya mazungumzo na John Terry kwa ajili ya kuona kama kuna uwezekano wa kurudi katika kikosi cha taifa.

“Bado mchezaji huyo ana nafasi ya kufanya kazi na mimi katika kikosi cha England, lakini tunatakiwa kusubiri. Sijui kama kuna mambo ya kisiasa yanaendelea na kama hakuna mambo hayo basi nitampa nafasi katika kikosi changu,” alisema Allardyce.

Kocha huyo anatarajia kukiita kikosi chake mwishoni mwa wiki hii kwa ajili ya kuwania kufuzu michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2018, mchezo wa kwanza utapigwa dhidi ya Slovakia.

Kwa upande wa klabu ya Chelsea, Kocha wa Klabu hiyo, Anton Conte, amedai kuwa John Terry ni mchezaji ambaye anaweza kutoa mchango kwa safu yake ya ulinzi, hivyo mchezaji huyo ana nafasi ya kuendelea kuitumikia klabu hiyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here