SHARE

NA AYOUB HINJO

Baada ya timu ya Taifa ya Tanzania kufungwa mabao 3-0 na Cape Verde, kila mtu anaonekana kuongea chake juu ya mchezo huo, huku wengine wakienda mbali wakihitaji kocha wa timu hiyo, Emmanuel Amunike, aondoke.

Naomba niwakumbushe kidogo, huo ulikuwa mchezo wa pili kwa Amunike tangu aichukue timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, bado anaendelea na ujenzi wa kile anachokihitaji.

Ni mapema sana kuanza kutoa lawama kwa kocha, ukizingatia ni mchezo wa pili tu kwake, kwa haraka hakuwa na kingine zaidi ya kuingia kwa falsafa ile ya kujilinda, kisha kushambulia kwa kushtukiza.

Ni njia rahisi zaidi ambayo aliamua kuitumia ili kutambua na kuusoma ubora wa wapinzani wake aliokutana nao kabla ya kucheza michezo ya marudiano.

Unapozuia maana yake wapinzani wako wanakuwa wanafunguka na kulisogelea lango lako kwa urahisi zaidi na unaweza kufungwa kama utafanya makosa ya kushindwa kuziba nafasi au utaadhibiwa kwa makosa binafsi ya wachezaji.

Mchezo dhidi ya Uganda, kila kitu kilionekana kwenda sawa, sababu wachezaji wote walitambua cha kufanya ili kuwabana wapinzani wao, huku wachezaji hao wakicheza kwa mawasiliano mazuri yaliyosaidia kuondoka Kampala na pointi moja.

Kwa mara nyingine, kocha wetu, Amunike alitumia falsafa ile dhidi ya Cape Verde, lakini mambo hayakuwa sawa kama alivyohitaji.

Kwa kiasi kikubwa wachezaji wa Taifa Stars walikosa mawasiliano mazuri na kupelekea kufungwa mabao mawili kipindi cha kwanza, hapo ndipo ukawa mwisho wa mchezo huo.

Cape Verde, ambao walikuwa wenyeji wa mchezo huo, walirudi kipindi cha pili wakitambua Taifa Stars itarudi kivingine ili kutafuta nafasi za kufunga mabao.

Ni kweli hicho kilitokea, walichokifanya wenyeji hao ni kushusha hali ya Taifa Stars kila walipokuwa na mpira kwa kucheza soka la taratibu bila presha sababu walikuwa na faida ya mabao mawili yaliyopatikana kipindi cha kwanza.

Kwa kiasi kikubwa, ili uweze kupata matokeo ya ushindi kwa aina ya michezo hiyo, inakuhitaji uwe na uhakika wa kutumia vizuri nafasi unazozitengeneza, lakini haikuwa hivyo kwa Taifa Stars, ambao walishindwa kufunga bao.

Kipindi cha kwanza, wachezaji saba walicheza nyuma ya mpira, kwa aina ya mchezo huo huwezi kuona ubora wa washambuliaji wako sababu timu inakuwa inashambuliwa.

Kwa aina ya wachezaji waliosimama mbele huonekana bora na wenye msaada kama timu inatengeneza nafasi za kutosha, kila mmoja anafahamu ubora wa Mbwana Samatta, Simon Msuva na Thomas Ulimwengu ulipo.

Mpaka sasa, tumecheza michezo mitatu katika Kundi L, huku tukivuna pointi mbili tu kwa kutoa sare ya bao 1-1 na Lesotho na suluhu dhidi ya Uganda, kabla kukubali kichapo cha mabao 3-0 juzi mbele ya Cape Verde.

Kufungwa mchezo huo inazidi kutuweka katika nafasi ngumu ya kufuzu katika hatua inayofuata ili kupata nafasi ya kushiriki ya michuano ya Mataifa ya Afrika mwakani nchini Cameroon.

Labda mchezo wa kesho kutwa wa marudiano dhidi ya Cape Verde katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, unaweza kufufua matumaini ya Tanzania kusonga mbele, lakini kama tutafanikiwa kupata matokeo ya ushindi.

Kwa namna moja au nyingine, michezo miwili ambayo itapigwa nyumbani kuanzia na huo wa keshokutwa inabidi Taifa Stars wapate matokeo ya ushindi, lakini ikiwa kinyume na hapo giza litazidi na hatutoweza kuona mbele.

Huu si muda wa kutoa lawama sijui mchezaji fulani angekuwepo timu isingefungwa, kipindi hiki kuelekea michezo iliyobaki kocha na wachezaji wanahitaji kuungwa mkono ili kuwapa moyo wa kuipigania bendera ya Tanzania.

Muda ndio huu wa kila Mtanzania kusimama imara na kujivunia timu ya Taifa, hatuna wakati mwingine mzuri wa kuunganisha nguvu zetu na kupaza sauti za umoja kama hivi sasa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here