SHARE

NA ABDULAH MKEYENGE

WAKUU wetu wa pale Karume wamepeana mkono wa kwaheri na kocha wa Stars Emmanuel Amunike. Wakuu wameingia msakoni kusaka kocha mwingine.

Amunike anaondoka Tanzania, nyuma akiacha historia aliyoiandika kwa wino wa moto. Haitafutika milele. Vizazi na viazi itakuja kusoma alichokifanya.

Kama nchi tulikaa miaka 39 bila kushiriki Mataifa Afrika, lakini Amunike alikuja kuiwezesha Stars kushiriki michuano hiyo. Ametuachia kumbukumbu nzuri. Kwake ni mafanikio makubwa kama kocha.

Muda huu ambao Amunike anafunga mabegi yake ili arudi Hispania anakoishi, tujiulize swali la msingi kupeana nae mkono wa kwaheri tumetatua tatizo?

Soka la Tanzania lina matatizo mengi yanayopaswa utatuzi, kuliko tunavyofikiri. Kumfukuza Amunike ni kumtoa sadaka ni kujisafisha machoni mwa watu, lakini ukweli ni kwamba soka letu lina matatizo.

Tumewahi kutimua na kuajiri makocha mbalimbali kwa ajili ya timu yetu ya taifa. Lakini makocha wengi tunaachana nao kwa sababu zile zile.

Kubwa tunalokosea hawa makocha hawarahisishiwi kazi zao ili kile wanachokifundisha kionekane kina nguvu. Tuna ligi ambayo ni dhaifu. Tuna ligi ambayo wachezaji hawana viwango vya kupambana na wachezaji wengine walioandaliwa vyema. Tulitaka Amunike afanye miujiza gani kwa wachezaji wa namna hii?

Tunachokiamini ukiwa na Amunike atafanya kila kitu kwa wachezaji wetu. Mchango wa kocha ni mdogo kama mambo yakiwa yamewekwa vyema, lakini katika nchi ambayo haizalishi wachezaji wenye viwango vikubwa, haina kundi kubwa la wachezaji wanaocheza nje, tulitaka Amunike afanye makubwa gani zaidi? Bila aibu tumeamua kujificha katika kivuli chake.

Kabla ya Amunike kama nchi tulipaswa kufanya kazi kubwa kwanza, Amunike akija anaingiza vitu vidogo jambo linaenda, lakini Amunike ambaye kocha wa Stars aanze kumfundisha mchezaji jinsi ya kuupokea mpira, kuuficha na mwisho kutoa pasi. Jamani hili ni jukumu la Amunike? Hili si jukumu lake kama kocha wa Stars.

Kabla ya kuajiri makocha wa nje hata wa ndani tunapaswa kuutazama mfumo wetu wa soka una mchango gani kwa kocha ambaye atakuwa na jukumu la kuinoa Stars? Tuna mfumo mbovu unaofanya kazi ya kocha wa Stars ionekane ngumu.

Hatuna mfumo rafiki ambao kocha wa Stars hatotumia nguvu kubwa kufundisha. Lakini yote haya tumeyaweka kando, badala yake tumemgeuza Amunike mbuzi wa kafara. Presha ilikuwa kubwa mtaani, mabosi wameamua kuishusha presha kwa kumfuta kazi Amunike.

Ninachokiamini akija kocha mwingine nae tutamuona hafai. Tutawasukuma mabosi wetu wamfukuze kama tulivyowasukuma wamfukuze Amunike. Mabosi wetu nao wanaishi kwa presha, wanaamini kumfukuza kocha wametibu tatizo.

Kumbe tatizo letu la msingi halijawahi kuwa kocha, tatizo letu la msingi ni mfumo mbovu soka tulionao ambao hauna msaada kwa kila kocha aliyekuja na kuondoka kuinoa Stars.

Amunike ameondoka kama walivyoondoka wakina Kim Poulsen, Mart Nooij na wengine, lakini tumeendelea kubaki kama tulivyo. Kubwa tusilolijua ni matatizo yetu ni makubwa kuliko tunavyofikiri.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here