Home Makala Amunike vitani na makocha waliokichafua Ulaya

Amunike vitani na makocha waliokichafua Ulaya

1489
0
SHARE

NA HASSAN DAUDI

SIKU zinazidi kukatika tu na hadi leo hii, umebaki mwezi mmoja kabla ya kuanza kwa fainali za Afcon 2019 huko Misri.

Presha ya michuano hiyo ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), ambayo ndiyo mikubwa zaidi kwa ngazi ya timu za taifa barani humu, imekolezwa na makocha kuanza kutaja vikosi vyao ya awali.

Taifa Stars nayo itakuwapo na tayari kocha wake raia wa Nigeria, Emmanuel Amunike, ameshalianika jeshi lake litakalopitia mchujo, kabla ya wale watakaokwea pipa kwenda nchini Misri.

Ukiacha kuwa Amunike anakuwa kocha wa kwanza kuipeleka Stars katika michuano hiyo tangu mwaka 1980, CV yake inapambwa na klabu ya Barcelona.

Ndiyo, alicheza Camp Nou kwa misimu minne, ikielezwa kuwa Barca walitumia Dola za Marekani milioni 3.4 kumng’oa Albacete Balompie, klabu ambayo pia ni ya Hispania.


Lakini je, ni makocha gani atakaokabiliana nao Afcon 2019, ambao nao waliwahi kutamba Ulaya wakiwa na klabu mbalimbali?

Djamel Belmadi (Algeria-PSG/Man City)

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 43, aliipeleka Algeria katika fainali za mwaka huu, amepoteza mechi moja tu kati ya sita, akishinda tatu na kutoa sare mbili.

Akiwa mchezaji, mzaliwa huyo wa Ufaransa alipita PSG, Gueugnon, Marseille, Cannes, kabla ya kwenda Celta Vigo ambako alimkuta staa mwingine aliyekuwa na jina kubwa katika soka la Afrika Kusini, Benni McCarthy.

Mwanzoni mwa mwaka 2003, Belmadi, aliyekuwa kiungo, alisajiliwa na Manchester City, iliyokuwa chini ya kocha Kevin Keegan.

Southampton walimchukua mwaka 2005, lakini majeraha ya mara kwa mara yalimzuia kung’ara na haikushangaza kuona akirejea Ufaransa kujiunga na Valenciennes, kabla ya kustaafu miaka minne baadaye

Michel Dussuyer (Benin-Cannes/Nice)

Katika kundi lilikuwa na Algeria na Togo, ilionekana wazi Benin na Gambia zisingefuzu, ikizingatiwa kuwa ni mbili tu zilizokuwa zikitakiwa kukata tiketi ya kwenda Afcon 2019.

Hata hivyo, Dussuyer aliiongoza Benin kuipiku Togo, akishinda mechi mbili, sare tatu na kufungwa moja.

Enzi za uchezaji soka, Mfaransa huyo alikuwa mmoja kati ya makipa mahiri Ligi Kuu ya Ufaransa, akiidakia Cannes na kisha kuajiriwa na Nice.
Clarence Seedorf (Cameroon-Ajax/AC Milan)

Katika mechi za kufuzu, Cameroon yake ilipangwa Kundi B na ilishika nafasi ya pili, nyuma ya Morocco, ikishinda mechi tatu, sare mbili na kupoteza moja.

Kabla ya kuwa mmoja kati ya viungo bora wa ulinzi kuwahi kutokea barani Ulaya, aliibuliwa na Ajax na baadaye Sampdoria, Real Madrid, Inter Milan na AC Milan.

Corentin Martins (Mauritania- Auxerre/Deportivo)

Kwa mashabiki wa soka huko Mauritania, jina la Mfaransa huyo litabaki kwenye kumbukumbu zao, kwani ndiye kocha aliyewapeleka Afcon kwa mara ya kwanza katika historia ya mchezo huo nchini humo.

Wakiwa Kundi I, walifuzu wakiwa nafasi ya pili nyuma ya Angola, ambapo katika ya mechi sita walizoshuka dimbani, walishinda mechi nne na kupoteza mbili, wakizizuia Burkina Faso na Botswana kwenda Misri.

Tukirejea kwa Martins, kocha mwenye umri wa miaka 49, aliwahi kutamba barani Ulaya, kwani kwa nyakati tofauti alikuwa kiungo mshambuliaji wa Auxerre, akiwa sehemu ya kikosi kilichofika nusu fainali ya Kombe la UEFA mwaka 1991.

Usajili wake kwenda Deportivo La Coruna haukuwa wa mafanikio kutokana na majeraha ya mara kwa mara na ndipo aliporejea Ufaransa kuzichezea Strasbourg Bordeaux, kabla ya kustaafu mwaka 2004.Herve Renard (Morocco- AS Cannes)

Ana historia kubwa katika soka la Afrika, akikumbukwa kwa mafanikio yake akiwa na timu za taifa za Zambia, Ivory Coast na sasa Morocco, aliyoipeleka Misri akiwa kileleni mwa Kundi B baada ya kushinda mechi tatu na kutoa sare mbili.

Mzaliwa huyo wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 50, naye aliwahi kukichafua barani Ulaya, akitamba Ligi Kuu nchini humo kwa nafasi yake ya beki katika klabu za AS Cannes, Stade de Vallauris na SC Draguignan.

Aliou Cisse (Senegal-Lille/PSG)

Akiwa ndiye kocha, Cisse aliihakikishia Senegal nafasi yao kule Misri baada ya kushinda mara tano na kutoa sare moja katika michezo sita ya kufuzu.

Kwa upande wa enzi zake za kucheza soka barani Ulaya, Cisse (43) alikuwa akicheza nafasi ya beki au kiungo. Klabu iliyotambulisha kipaji chake ni Lille, kabla ya baadaye kutua PSG.

Baada ya kuifikisha Senegal robo fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2002, alisajiliwa na Birmingham City, akitolewa kwa kadi nyekundu katika mchezo wake wa kwanza dhidi ya Arsenal.

Portsmouth walimchukua, kabla ya kurejea Ufaransa ambako alizichezea CS Sedan, Nimes Olympique na alistaafu mwaka 2009.

Alain Giresse (Tunisia- Bordeaux/Marseille)

Kikosi chake cha Tunisia kilifuzu Afcon 2019 kikiwa Kundi J, baada ya kushinda mechi tano na kufungwa moja kati ya zile sita za hatua ya makundi.

Enzi zake za uwanjani, Giresse (66) alikuwa kiungo, akizichezea Bordeaux na Marseille, ikikumbukwa pia alikwenda na kikosi cha Ufaransa katika fainali za Kombe la Dunia za mwaka 1982, ambapo walishika nafasi ya tatu.

Aidha, alikuwa kikosini sambamba na wakali Michel Platini, Luis Fernandez na Jean Tigana, wakati Ufaransa ilipotwaa ubingwa wa fainali za Euro mwaka 1984.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here