SHARE

MILAN, Italia

WAKATI Li Yonghong anainunua AC Milan mwaka 2017, mashabiki wengi wa kikosi hicho walikuwa na matumaini makubwa ya timu yao kurudi kuwa kama zamani enzi hizo wakitawala soka la Italia.

Timu hiyo ilifanikiwa kufanya usajili uliokaribia kufika pauni milioni 200, ambao wengi wao waliishia kuwa kichekesho tu, kwa kushindwa kuonyesha viwango vilivyotarajiwa na wengi.

Tajari huyo aliishia kushuhudia timu hiyo ikifungiwa kucheza michuano ya Ligi ya Europa kutokana na kuvunja sheria za usajili za Shirikisho la Soka Kimataifa, FFP.

Achana na hilo, wakati ambao iliaminika kuwa Li Yonghong atairudisha timu hiyo katika ubora wake, walifanikiwa kusajili mastraika wengi ambao wote wameshindwa kuziba nafasi iliyoachwa na Zlatan Ibrahimovic. 

Japo, kidogo tangu kuingia kwa Krzysztof Piatek alionekana kufuata nyayo za mshambuliaji huyo wa Sweden ambaye sasa anacheza katika kikosi cha LA Galaxy huko Marekani.

Straika raia wa Ureno, Andre Silva ambaye amecheza kwa misimu miwili katika kikosi cha AC Milan anajiandaa kuondoka kwnda AS Monaco huku akiwa ametoka kwa mkopo wa muda mrefu Sevilla.

Hawa hapa mastraika walioshindwa kuwika katika kikosi cha AC Milan kipindi cha hivi karibuni kama ilivyokuwa kwa Silva.

Alessandro Matri

Amezalia karibu na Jiji la Milan lakini alifanikiwa zaidi akiwa Juventus, mashabiki wa AC Milan walifurahu kumwaona Matri katika kikosi chao mwaka 2013, alikuwa na rekodi ya kufunga mabao 27 ndani ya misimu miwili akiwa Juventus na Cagliari.

Lakini miezi minne aliyokuwa kwa mabingwa hao wa zamani wa Italia, aliishia kufunga bao moja tu, mwishowe alitolewa kwenda kucheza Fiorentina.

Hakufanya vizuri tena, alitolewa kwa mkopo kwenda Genoa ambako pia, alikuwa na msimu mbaya, pengine alidani kurejea kwake ndani ya Juventus kungerudisha makali yake, nako ilishindikana kabisa.

Matri alipelekwa Lazio, baadae, aliuzwa kwenda Sassuolo ambako aliishia kuwa mchezaji wa akiba tu akipasha misuli.

Luiz Adriano

Nani?, inawezekana umeshtuka kuliona jina lake katika orodha hii. Haraka kaangalie wasifu wake katika mtandao wa Wikipedia, utagundua kuwa muda mwingi aliutumikia nchini Ukraine.

Alifunga mabao kadri alivyojisikia akiwa na Shakhtar Donetsk, kiwango chake kiliwafanya Ac Milan walipe kiasi cha pauni milioni 8 kumsajili mwaka 2015.

Alihangaika kufanya vizuri, hakuwa na kiwango kizuri tena zaidia ya kuandamwa na mejaraha. Ndani ya San Siro, alifunga mabao sita katika michezo 36 aliyocheza akiwa na jezi ya AC Milan.

Mwishowe, mwaka juzi aliuzwa Spartak Moscow ya Urusi baada ya dili lake kuelekea China kushindwa kukamilika. 

Nikola Kalinić 

​Baada ya kuwa na misimu kadhaa bora ndani ya kikosi cha Fiorentina, Kalinic alikamilisha usajili wa kwenda San Siro uliotajwa kuwa na thamani ya pauni milioni 25, mwaka 2017.

Bado mashabiki wa AC Milan hawakukata tamaa na kikosi chao, ukizingatia walitoka kulipa kiasi kikubwa cha pesa kwa ajili ya Andre Silva.

Mabao yake yalifanikiwa kurejea ndani ya Jiji la Milan? Aliishia kufunga mabao sita tu, katika michezo 41. Hakufanya vizuri, kiasi cha mashabiki wa timu yake kumzomea kila alipokuwa uwanjani.

Mwishowe alisajiliwa na Atletico Madrid, ilikuwa nafuu zaidia kwa mashabiki wa Ac Milan kuliko Kalinic ambaye bado anapambana kurejea katika kiwango chake.

Andriy Shevchenko

Moja ya wakongwe wa AC Milan ambao huwezi kukosoa pindi wanapokuwa uwanjani, badoa anakamata nafasi ya pili katika orodha ya wafungaji wa muda wote akiwa na mabao 175.

Lakini straika huyo raia wa Ukraine, alisajiliwa Chelsea, Shevchenko alishindwa kufanya vizuri katika kikosi chenye maskani yake Stmaford Bridge.

Kufanya kwake vibaya kulifanya arudishwe AC Milan kwa mkopo, lakini haikumsaidia kurejea kwenye ubora wake wa kupachika mabao.

Hakufunga bao lolote katika michezo 18 ya Ligi Kuu aliyocheza akiwa AC Milan, aliishia benchi tu, aliporejea Chelsea aliuzwa moja kwa moja Dynamo Kyiv, ambako miaka mitatu baadae alistaafu kucheza soka.

Mario Balotelli 

Kama ilivyokuwa kwa Shevchenko, straika Mario Balotelli alirejea AC Milan baada ya kuondoka Liverpool, alifunga mabao 30 katika michezo 54 ndani ya kikosi hicho cha Italia, matumaini yalikuwa makubwa angerejea katika kiwango chake.

Balotelli alihangaika ndani ya Ac Milan, alifunga bao moja tu katika mechi 20 huku muda mwingi akiishia kuwa majeruhi.

AC Milan walimrejesha Liverpool, aliishia kuuzwa Nice ya Ufaransa ambako kwa kiasi kidogo alifunga mabao 23 katika michezo 49 aliyocheza na timu hiyo iliyopo Ligue 1.

Sasa ni mchezaji huru baada ya kuondoka Marseille, Balotelli anahusishwa kuhitajika na timu za Italia na England lakini bado mpaka sasa hajaamua pa kwenda.

Gianluca Lapadula 

Mwaka 2016 alijiunga na AC Milan, je, wasifu wake ukoje? Ndani ya miaka tisa alikuwa amecheza katika timu zisizopungua 12, ambazo kwa kiasi kikubwa zilikuwa za madaraja ya chini.

Kilichofanya AC Milan kutoa pauni milioni 9 kumsajili straika huyo ni kiwango alichokionyesha alipokuwa na timu ya Pescara ya Daraja la Pili Italia. 

Alifunga mabao nane katika michezo 27, AC Milan iliponunuliwa na Li Yonghong alikuwa mmoja wa wachezaji ambao walitemwa na kikosi hicho. 

Lapadula alisajiliwa Genoa msimu uliofuata, alifunga idadi ya mabao sawa na alipokuwa AC Milan, aliandamwa sana na majeraha ambayo yalipelekea kutolewa kwa mkopo kwenda Lecce. 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here