Home Michezo Kimataifa ANTOINE GRIEZMANN ZIGO LA MISUMARI LINAMSUBIRI OLD TRAFFORD

ANTOINE GRIEZMANN ZIGO LA MISUMARI LINAMSUBIRI OLD TRAFFORD

514
0
SHARE

NA EZEKIEL TENDWA, 

MANCHESTER United ni timu kubwa duniani, hilo upende usipende habari ndivyo ilivyo, kwani mafanikio waliyonayo hapana shaka kwamba yanatambulisha ukubwa walionao.

Katika Ligi Kuu nchini England, timu hii ambayo kwa sasa inashika nafasi ya sita ikiwa na pointi 41, ndiyo ambayo imeutwaa ubingwa huo mara nyingi kuliko timu nyingine yoyote.

Timu hiyo ambayo kwa sasa ipo chini ya kocha mwenye maneno mengi ya shombo, imetwaa ubingwa huo mara 20 wakifuatiwa kwa ukaribu na Liverpool walioutwaa mara 18 hiyo ikimaanisha kuwa mashetani hao wekundu wapo imara.

Na katika kikosi hicho jezi namba saba (7) ndiyo ambayo imepitia katika mikono ya mastaa wengi waliong’ara ndani ya kikosi hicho na ndivyo inavyoonekana kuheshimiwa zaidi.

Jezi hiyo ilishawahi kuvaliwa na gwiji wa kikosi hicho, George Best na shughuli yake kila mmoja anaijua, kwani licha ya kwamba alikuwa winga lakini alifanikiwa kufunga jumla ya mabao 137 katika michezo 361 aliyocheza ndani ya kikosi hicho.

Nani mwanamichezo ambaye ukilitaja jina la Eric Cantona atakwambia hamjui?  Huyo naye aling’ara na jezi hiyo na alimaliza kazi yake kwa mashetani hao wekundu akiwa na mabao 64 katika michezo 143 na anakumbukwa mpaka leo.

Vipi kuhusu David Bekham? Nani hajui kitu alichokifanya winga huyo wa kulia katika kikosi hicho cha Manchester United?  Nani hakumbuki krosi alizokuwa akizichonga.

Vipi kuhusu mabao ya faulo aliyokuwa akiyafunga kwa mashuti yake makali yaliyowaacha makipa wakishangaa wasijue la kufanya? Bekham naye aliitendea haki jezi namba saba na aliiacha kwa heshima alipoamua kutimkia Real Madrid.

Angalia mwaka 2009 wakati Cristiano Ronaldo anapoondoka katika kikosi hicho kwenda nchini Hispania kujiunga na Real Madrid, mashabiki wa Manchester United walitokwa machozi kutokana na umuhimu aliokuwa nao.

Alifanya kila kilichowezekana ambapo baadhi ya timu zilipokuwa zinakutana na United mtu pekee aliyekuwa akiimarishiwa ulinzi alikuwa Ronaldo. Aliitumia vizuri jezi namba saba na aliondoka salama bila lawama.

Tangu kuondoka kwa Ronaldo jezi hiyo mpaka sasa haijapata mtu sasa anayeitendea haki, kwani akina Luis Nani waliojaribu kuivaa walikuwa wakirukaruka tu uwanjani na mwisho wa siku wakaamua kuivua.

Antonio Valencia, alipokuja Manchester United alijaribu kuvaa lakini akaona inampwelepweta na haraka sana akaivua akaamua kuchukua jezi namba 25 ambayo ndiyo anayoitumia mpaka sasa.

Alivyokuja Memphis Depay, aliona kama akina Valencia waliamua kuiacha jezi hiyo hawajui walitendalo kumbe yeye ndiye aliyeingia kichwakichwa akaivaa kwa mbwembwe nyingi na mwisho wa siku leo hii ameshapigwa bei Lyon ya nchini Ufaransa.

Sasa sikia hii. Kocha Mkuu wa Manchester United, Jose Mourinho, anataka kufanya usajili ambapo mtu ambaye amemtupia jicho ni straika wa Atletico Madrid ya nchini Hispania, Antoine Griezmann na hii ni kutokana na uwezo mkubwa alionao ndani ya uwanja.

Na wakati Mourinho akimwinda Mfaransa huyo kwa kila namna, taarifa zinadai kuwa ameandaliwa zawadi nzuri sana na zawadi yenyewe ni kupewa jezi hiyo namba saba, ambayo kwa sasa imehifadhiwa tu baada ya Depay kutimka zake kutokana na kukosa nafasi.

Hata hivyo, swali muhimu linalobakia kwa mashabiki ni kwamba, je, ataweza kuitendea haki kama dili lake likitiki ndani ya mashetani hao wekundu au hadithi itakuwa ileile ya akina Depay?

Kilichopo ni kusubiri kama Mourinho atamsajili na endapo itakuwa hivyo uhakika ni kwamba, atapewa jezi namba saba kwani ndiyo anayoitumia huko aliko na hiyo itakuwa ni sawa na kutwishwa zigo la misumari kichwani. Ngoja tusubiri.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here