Home Habari APR: Hatutaisahau Yanga

APR: Hatutaisahau Yanga

737
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU

WIKI yote hii imeendelea kuwa ya majonzi kwa wachezaji wa timu ya APR ya Rwanda, kufuatia kipigo cha mabao 2-1 walichokipata kutoka kwa Yanga Jumamosi iliyopita.

Licha ya kukosa amani kwa uongozi wa timu hiyo pamoja na mashabiki wake, lakini bado wanaendelea kupigwa na butwaa kutokana na kampeni walizofanya wapinzani wao hao kutoka Tanzania ya kuteka mashabiki lukuki katika ardhi yao.

10-74Yanga licha ya kushinda mchezo huo wa awali wa michuano ya Klabu Bingwa Barani Afrika, lakini iliweka historia ya kupokelewa na umati wa mashabiki, wengi wao wakitokea katika timu zinazoshiriki ligi kuu ya nchi hiyo.

Miongoni mwa mashabiki waliojitokeza kwa wingi kuilaki Yanga tangu ilipotua Rwanda Alhamisi na kisha kuishangilia katika mchezo uliopigwa Jumamosi ni kutoka timu ya Rayon Sports na Kiyovu.

Nahodha wa APR, Jean Cloud Iranzi, ni miongoni mwa wachezaji waandamizi wa timu hiyo ambaye hadi sasa bado hajaelewa kampeni za Yanga ziliyofanyika kiasi cha kulitetemesha jiji la Kigali na kisha kupata ushindi ule.

“Japokuwa Yanga ina wachezaji kutoka hapa nymbani (Rwanda), lakini haijulikani walitumia muda gani kuandaa mapokezi ya halaiki ya wapenzi wa hapa Kigali,”

alisema Iranzi.

Hata hivyo, nahodha huyo anaamini kwamba mechi ya marudiano itakayochezwa jijini Dar Machi 18 inaweza kuwa na mabadiliko kwa vile wataingia Dar wakifahamu wanakwenda kupambana na timu yenye mipango ya ndani na nje ya uwanja.

Kwa upande wake Haruna Niyonzima, aliyecheza katika mechi ile kama nahodha wa Yanga, aliwataka mashabiki waendelee kuwaunga mkono katika mechi hiyo kwa kile alichodai inaweza kuwa ngumu kutokana na jinsi APR watakavyojipanga.

“APR ni timu kubwa na yenye mipango, itatupasa tujipange vizuri ili tupate matokeo mazuri,”  alisema Niyonzima.

Kocha Mkuu wa Yanga, Hans Pluijm, ameanza kukinoa upya kikosi chake katika mazoezi yanayoendelea kufanyika katika Uwanja wa Chuo cha Maafisa wa Polisi Kilwa Road na kudai kwamba kuna baadhi ya mapungufu yaliyojitokeza katika mechi ile ya awali ambayo anaendelea kuyafanyia kazi.

Juu ya mechi ya marudiano, alisema kamwe hawezi kudharau mechi yoyote inayokuja mbele yao.

“Sijawahi kudharau mechi hata moja ya Ligi, siwezi nikadharau hii ya kimataifa, nia ni kupata ushindi ili tusonge mbele,”  alisema.

Pluijm amewaagiza wachezaji wake kujituma na kuhakikisha inapata mabao kama 20 hivi katika michezo ya ligi iliyobaki.

Hadi sasa timu hiyo imefikisha idadi ya mabao 51 iliyokwishafunga katika michuano ya Ligi Kuu na kushika nafasi ya pili, ikitanguliwa na Simba iliyokwishapachika mabao 54.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here