SHARE

LYON, Ufaransa

ISHU ipo hivi, klabu ya Arsenal ipo kwenye mazungumzo ya kumsajili Alexandre Lacazette ambaye alikaribia kutua Atletico Madrid kama si timu hiyo ya Hispania kufungiwa usajili.

Na Lyon wao hawaoneshi ugumu wa kumwachia straika wao huyo, ni makubaliano tu ya kibiashara ambayo yatakamilisha uhamisho wake.

Lyon inataka straika mzuri atakayeweza kurithi nafasi ya Lacazette, kwa kuwa licha ya kumnasa Bertrand Traore na kumfukuzia straika wa Real Madrid, Mariano Diaz, bado hawaoni kama wanafaa kuchukua mikoba ya Lacazette.

Olivier Giroud kwa sasa ni mguu ndani mguu nje Emirates na kocha wa Arsenal, Arsene Wenger, ameonesha kutokuwa mgumu pia kumwachia straika wake huyo, hiyo ikiwa na maana anao uwezo wa kubadilishana na Lyon.

Awape Giroud, wampe Lacazette.

Lyon wenyewe kupitia kwa rais wao, Jean-Michel Aulas, wameshaweka wazi kuwa Lacazette hataondoka kama hawajapata mrithi wake sahihi.

“Alishatuambia kuwa anataka kuondoka na tukampa ruhusa aende sehemu anayoipenda, lakini kuna vitu vinatakiwa kuwekwa sawa kabla ya kuondoka kwake.”

Aulas ambaye anataka pauni milioni 57 kwa Lacazette, alisema straika huyo hana nia ya kubaki na wiki ijayo hatima yake itazungumziwa.

Rais huyo pia alishanukuliwa kuvutiwa na Giroud, lakini pia yupo tayari kwa niaba ya timu kusikiliza ofa za Lacazette.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here