Home Makala ARSENE WENGER ANAPAMBANA NA HALI YAKE, WALA SI WA KUMLAUMU

ARSENE WENGER ANAPAMBANA NA HALI YAKE, WALA SI WA KUMLAUMU

317
0
SHARE

NA EZEKIEL TENDWA

UKISHAUMBWA mwanamume lazima uwe na roho ngumu, kwani kama isingekuwa hivyo leo hii tungesikia Arsene Wenger, yule Kocha Mkuu wa Arsenal, kwamba ameshazira na kuwatupia makabrasha wenye timu yao kisha akasepa zake.

Ndiyo! Lazima angefanya hivyo kama angekuwa na roho nyepesi, kwani kila kukicha ni maneno tu kwake, kila mtu akizungumza lake, anasimangwa kila kona lakini anajua yeye ni mwanamume hivyo lazima akomae.

Wenye roho za kwanini wameanza kumrushia Wenger maneno kisa kufungwa mchezo mmoja uliopita wa Ligi Kuu nchini England, huku wanaomlaumu wakisahau kuwa katika mchezo wao wa kwanza Mfaransa huyo aliiongoza timu yake kushinda mabao 4-3.

Timu iliposhinda mabao 4-3 dhidi ya Leicester City, mchezo wa ufunguzi, mtaa ulikuwa kimya lakini walipofungwa na bao 1-0 na Stock City, mwishoni mwa wiki iliyopita, basi maneno tu kwa mzee wa watu kana kwamba anapenda hali hiyo itokee.

Licha ya kwamba kuna baadhi ya timu kubwa kama Chelsea, nao walipata matokeo kama hayo ya Arsenal ya kushinda mchezo mmoja na kupoteza mmoja, lawama zimekuwa nyingi kwa Wenger hiyo ikimaanisha kwamba kuna jambo nyuma ya pazia.

Hapa ngoja nimtetee mzee wa watu kwamba anapambana na hali yake, kwani katika misimu kadhaa iliyopita alianza hivyo hivyo na mwisho wa siku akamaliza vizuri kwa kushika nafasi nne za juu japo msimu uliopita waliteleza kidogo.

Hapa tunajiweka pembeni kidogo na habari ya ubingwa, bila shaka wanaolalamika sana wanafikiria imepita misimu mingapi bila Wenger kupeleka furaha hiyo ya kombe, ila kuhusu kushiriki michuano ya Uefa, Mfaransa huyo amejitahidi sana.

Wakati baadhi ya watu wakilalamika kwamba timu imeanza vibaya msimu huu kwa kushinda mchezo mmoja na kupoteza mmoja, wanasahau kwamba ndani ya misimu ya hivi karibuni ndivyo ilivyokuwa.

Mfano mzuri ni msimu uliopita ambapo walianza kwa kichapo cha mabao 4-3, kutoka kwa Liverpool na baadaye kutoka suluhu ya 0-0 dhidi ya Leicester City, wakapata matokeo mazuri katika michezo karibuni mitano mfululizo ikiwapo ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Chelsea, sema bahati mbaya ni kwamba walimaliza wakiwa nafasi ya tano na kukosa kushiriki michuano ya Uefa.

Kwa msimu huo uliopita wanachotakiwa kumlaumu Wenger ni kukosa tu nafasi yao ya nne kama ilivyo kawaida yao na kushiriki michuano hiyo ya Uefa, vinginevyo wamwache mzee wa watu aendelee kufanya kazi yake na mwisho wa siku astaafu vizuri.

Kama hiyo haitoshi, msimu wa 2015/16, walianza vibaya wakifungwa na West Ham mabao 2-0 wakiwa nyumbani, wakaifunga Cristal Palace 2-1 na suluhu ya 0-0 dhidi ya Liverpool na mwisho wa msimu wakamaliza nafasi ya pili sasa hapo dhambi ya Wenger iko wapi?

Ili kudhihirisha kwamba Wenger anapambana na hali yake, msimu wa 2014/15 walianza kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Cristal Palace na kutoka sare michezo mitatu mfululizo, ikiwamo ile ya 2-2 dhidi ya Manchester City kabla ya kuzinduka mchezo wa nne wakishinda mabao 3-0 dhidi ya Aston Villa. Waliendelea kushiriki michuano ya Uefa.

Hata msimu wa 2013/14, hali ilikuwa hivyo hivyo na mwisho wa siku wakamaliza nafasi ya nne. Hapa labda kuwekana sawa ni kwamba, Wenger amekuwa na matokeo hayo hivyo wanaoona msimu huu ameanza vibaya, watakuwa hawajafuatilia sana mwacheni mzee Wenger apambane na hali yake, wala asilaumiwe.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here