SHARE
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta

LONDON, England

UNAWEZA kusema mambo ni mazuri kwa kocha mpya wa Arsenal, Mikel Arteta, kutokana na mabadiliko ambayo vijana wake wameyaonyesha kwenye michezo miwili ya mwisho ambayo yote alipata ushindi.

Arteta anataka kuiona Arsenal ikicheza soka la kiwango cha hali ya juu na hilo litafanikiwa ikiwa wachezaji wa timu hiyo wataamua kukaza buti na kuonyesha ubora wao msimu huu.

Lakini bado kuna maeneo ya kurekebisha kwenye kikosi hicho hasa safu ya ulinzi ambayo imekuwa kama pakacha lililotoboka halafu na majeruhi kadhaa ambao wanaiweka Arsenal kwenye ulazima wa kufanya usajili.

Tuko mwezi Januari, je ni wachezaji gani ambao huenda tukawaona katika viunga vya Arsenal kabla ya kuingia Februari?

Jerome Boateng

Asikudanganye mtu, Boateng ni aina ya mchezaji ambaye kwa wanaoelewa soka watakueleza wazi ndiye mchezaji anayetakiwa pale Arsenal na hata klabu yenyewe iko radhi kumsajili.

Tetesi zinasema kuwa beki huyo wa kati mwenye umri wa miaka 31 anapatikana bila dau lolote la usajili, maana yake ni kwamba Arsenal inatakiwa kulipa tu mshahara wake wa wiki ili wamchukue bure. 

Boateng si yule wa zamani, lakini ni mashabiki wachache wa Arsenal watakaoweza kupinga uhamisho wake kutokana na kwamba atakaposimama na David Luiz ni lazima kuna uimara ambao utaongezeka kwenye safu ya ulinzi ya timu yao hiyo. 

Kitu pekee ambacho Arsenal watafaidika kwa Boateng ni kwa beki huyo kutoumia mara kwa mara.

Thomas Lemar

Kama utakumbuka, Arsenal iliwahi kuhusishwa na Lemar kipindi hicho akiwa Monaco na ilidaiwa kwamba walikuwa tayari kulipa kiasi cha pauni milioni 92 ili waipate saini yake.

Bahati mbaya kwa Arsenal, kiungo huyo raia wa Ufaransa aliishia kutua Atletico Madrid ambako hana maisha mazuri ambayo pengine aliyatarajia kwa wabishi hao wa La Liga. 

Licha ya hivyo, Atletico hawatoshawishika kumuuza Lemar na huenda wakakubali dili la kumtoa kwa mkopo. 

Hapo ndipo Arsenal watatakiwa kutumia fursa kwani ni aina ya mchezaji ambaye atacheza vizuri tu kwenye mfumo wa Arteta. Ni mchezaji bora, ingawa si ambaye anahitajika zaidi pale Emirates.

Ukiachana na ubora wake wa kucheza eneo la pembeni la safu ya viungo watatu, Lemar ni kiungo mchapakazi na Arteta hupenda wachezaji wanaozingatia nidhamu kubwa pindi wanapocheza bila mpira katika himaya yao. 

Hakem Ziyech

Ripoti za Arsenal kuvutiwa na Ziyech na kuwa tayari kumsajili zilianza kutikisa katika vyombo vya habari tangu majira yaliyopita ya kiangazi, lakini kwa sasa ndio imezidi na timu yake ya Ajax ipo tayari kumuuza.

Pauni milioni 40 zitatosha kuishawishi Ajax imuachie kiungo mshambuliaji huyo raia wa Morocco ambaye ubora wake mkubwa ni pale anapotumika kama mchezaji huru. Ziyech ni mrithi sahihi wa Mesut Ozil. 

Anao pia uwezo wa kucheza kama mshambuliaji wa pembeni, kuna uwezekano Arsenal ikamtumia hivyo kwa sababu ya ishu za mkataba zinazoendelea kwa Pierre-Emerick Aubameyang na Alexandre Lacazette.

Mmoja kati ya mastraika hao huenda akaondoka, lakini itakuwa ni fursa kwa Arteta kumsajili Ziyech na kumtumia pembeni hasa upande wa kushoto.

Dayot Upamecano

Majira yajayo ya kiangazi Arsenal itaanza kumtumia beki wake raia wa Ufaransa, William Saliba ambaye amerudishwa St. Etienne kwa mkopo, lakini katika orodha ya usajili ya klabu hiyo kuna jina la Upamecano.

Pengine dau kubwa la uhamisho wake ambalo ni pauni milioni 70 ndilo lililosababisha Upamecano asitue Emirates majira yaliyopita ya kiangazi, lakini bado Arsenal ina matumaini makubwa ya kuinasa saini yake. 

Beki huyo mwenye umri wa miaka 19 ni tegemeo la RB Leipzig chini ya kocha mbunifu, Julian Nagelsmann, kutokana na uimara wake kwenye ulinzi na uwezo wa kuuchezea mpira.

Max Aarons

Tangu Arteta atangazwe kuwa kocha mpya wa Arsenal, kiwango cha Ainsley Maitland-Niles kwenye upande wa kulia wa safu ya ulinzi kimerudi kwa kasi kubwa mno.

Ni tishio kwa Hector Bellerin ambaye amekuwa akiumia mara kwa mara msimu huu na ametabiriwa kuuzwa siku sio nyingi.

Kuna jina jipya ambalo linasubiriwa pale Arsenal ambalo ni la kinda wa Norwich, Max Aarons. Pauni milioni 30 zitampa Arteta mchezaji bora kiufundi katika mfumo wake anaotaka Arsenal icheze. 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here