Home Michezo Kimataifa ATAKAYEPIGWA ANFIELD APAMBANE NA HALI YAKE

ATAKAYEPIGWA ANFIELD APAMBANE NA HALI YAKE

621
0
SHARE

LONDON, England

JIONI ya leo, klabu ya Liverpool itavaana na Arsenal katika mtanange wa Premier League utakaopigwa kwenye dimba la Anfield, ambapo miamba hao wanatarajiwa kuchuana vikali kuwania alama tatu muhimu.

Kikubwa kinachosubiriwa katika mchezo huo wa leo ni kama Liverpool wataendeleza kilio cha Arsenal ndani ya hizi wiki mbili.

Lakini, tegemea mabao ya kutosha kwenye pambano hilo, kwani rekodi yao iko wazi kabisa juu ya suala hilo.

Mchezo huo ni mmoja wa mitanange mikubwa England, kutokana na mafanikio makubwa yaliyopo kwenye historia ya klabu hizo mbili.

Bila shaka, klabu hizo zina matumaini ya kutwaa taji la Premier League msimu huu, lakini dalili za awali kabisa zinaonesha wazi wawili hao wana lengo la kuhakikisha wanamaliza ‘top four’.

Katika mechi zote mbili za awali katika msimu huu wa 2017/18, tumeona jinsi gani timu hizo mbili zilivyo na nguvu ya kushambulia, tofauti na safu zao za ulinzi zisizoridhisha.

Kwa sababu hiyo, mchezo wa leo unaonekana kuwa mgumu sana kutabirika kadiri muda unavyozidi kusonga, kwani kila timu ina nafasi ya kushinda au sare ya mabao mengi.

Tukirudi nyuma kwenye ushindi wa bao 1-0 walioupata Liverpool wikiendi iliyopita dhidi ya Crystal Palace, ni wazi Liver kwa sasa wana uwezo wa kusaka alama tatu muhimu kwa nguvu zote. Ikizingatiwa mchezo wa kwanza walilazimishwa sare na Watford ugenini.

Wakati huo huo, Arsenal wao wakapokea kichapo kutoka kwa Stoke City. Safu yao ya ulinzi ilionesha mabadiliko finyu sana, walaini na umaliziaji ulikuwa butu. Siku yao ikawa yenye nuksi tupu.

Leo sasa inabidi vijana hao wa kocha Arsene Wenger waamke kutoka usingizini na kupata ushindi, bila ya hivyo, yale mabango na hashtags za Twitter: #WengerOut, zitaibuliwa upya.

Ni wazi kabisa mchezo huo utaamuliwa moja kwa moja na safu za ushambuliaji kuliko walinzi wa timu zote mbili, hivyo itakuwa ni burudani tosha kuona mafowadi wakifanya yao leo.

Alexis Sanchez huenda akaanza leo sambamba na nyota wengine wa Arsenal, Mesut Ozil na Alezandre Lacazette. Imani kubwa iliyopo kwa washika mitutu hao wa London ni kuisasambua safu ya ulinzi ya Liver inayoishi kwa mashaka.

Lakini, hakuna mdau wa soka asiyefahamu balaa walilonalo Liverpool pindi wanapofika langoni mwa mpinzani kupitia miguu na akili nyingi za washambuliaji wao watatu, Mohamed Salah, Sadio Mane na tozi la Kibrazil, Roberto Firmino.

Aidha, viungo wa pande hizo mbili kwa leo wanatarajiwa kuwa wachapakazi zaidi ya wabunifu hasa Liverpool ambayo itawakosa mafundi wao, Philippe Coutinho na Adam Lallana, hivyo Granit Xhaka na Aaron Ramsey watarajie mchuano mkali katikati dhidi ya Jordan Henderson, Emre Can na Gini Wijnaldum.

Leo itakuwa ni balaa baina ya timu hizo mbili zenye soka la kupendeza mno. Tegemea mabao ya kutosha sana, maana ni rahisi kwa Luis Suarez kurudi Liver kuliko mchezo huo uishe kwa sare ya 0-0!

TAARIFA NA MAJERUHI

Katikati ya wiki, Liverpool ilicheza mechi ya Champions League dhidi ya Hoffenheim, hivyo huenda kocha Jurgen Klopp akakifanyia mabadiliko kidogo kikosi chake, hivyo ni ngumu kutabiri nani ataanza kwa upande wao.

Tunachokifahamu ni kwamba Coutinho hatacheza, ambapo anatarajiwa kuungana na wenzake mara baada ya mapumziko ya kupisha mechi za kimataifa kumalizika.

Lallana na Nathaniel Clyne bado watakosekana kutokana na kuuguza majeraha, huku Trent Alexander-Arnold na Joe Gomez wakiwa kwenye mchuano mkali wa kuanza leo upande wa beki ya kulia.

Kama ilivyoelezwa mwanzoni, Sanchez huenda akaanzishwa leo kwa upande wa Arsenal, ingawa Wenger pia huenda akahofia kumwanzisha kwenye mchezo ambao una presha sana.

Kurudi kwa nahodha, Laurent Koscielny, ni taarifa njema sana kwa Wenger, kwani ni beki tegemeo wa kati katika muda wa miaka saba Emirates.

Huenda akaanza kuchukua nafasi ya Nacho Monreal, lakini Hector Bellerin anategemewa kupigwa benchi kutokana na fomu yake kutokuwa vizuri kwenye kipindi hiki cha mwanzo wa ligi, na upande wake wa ‘left wing-back’ akakabidhiwa Monreal.

NYOTA WA KUOGOPWA

Sadio Mane. Huyu jamaa leo anaweza akapeleka kilio kwa Arsenal.

Wakati dunia ya soka ikiwa bize kusema Coutinho ndiye mchezaji bora wa Liverpool, upande wa pili unakataa na kusema Mane ni habari nyingine.

Mane (25) tayari ameshaonesha umuhimu wake katika mechi iliyopita dhidi ya Palace. Kasi, mizunguko yake uwanjani na uwezo wa kujitenga kwenye maeneo muhimu unamfanya awe mmoja wa wachezaji bora wa Premier League.

Kama Arsenal haitamchunga vyema Mane, atawaliza sana tu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here