Home Michezo Kimataifa ATAONDOKA.. CARRAGHER AMTAJA CONTE KWENYE REKODI YA CHELSEA KUFUKUZA MAKOCHA

ATAONDOKA.. CARRAGHER AMTAJA CONTE KWENYE REKODI YA CHELSEA KUFUKUZA MAKOCHA

381
0
SHARE

LONDON, England

MCHAMBUZI wa soka wa Sky Sports, Jamie Carragher, amesema litakuwa jambo la kushangaza kama Antonio Conte atadumu Chelsea kwa mwaka mwingine.

Conte aliiongoza Chelsea kunyakua taji la EPL katika msimu wake wa kwanza kuifundisha timu hiyo, lakini Carragher anayaona malalamiko yake kuhusu vibopa wa klabu hiyo ni dalili mbaya ya Muitaliano huyo kutodumu.

Carragher, mchezaji wa zamani wa Liverpool, alidai kuwa suala la mabosi wa Chelsea kusimamia wenyewe dili za usajili ndilo linalomkosesha raha Conte.

“Nitashangazwa kama atadumu hata kwa miezi 12. Conte si kocha wa kukubali kuingiliwa majukumu yake, hasa ikiwa ni muda mfupi tu tangu ashinde taji EPL.

“Kiuhalisia hataweza kunyamaza na ni kitu kibaya kwa kocha kutoa maneno kama ya Conte,” alisema.

Tangu bilionea wa Kirusi, Roman Abramovich, ainunue Chelsea mwaka 2003, Jose Mourinho alishatimuliwa mara mbili huku wengine kama Carlo Ancelotti, Luiz Felipe Scolari na Claudio Ranieri wakidumu kwa muda usiozidi miaka miwili.

Aidha, Carragher alisema Abramovich pamoja na mkurugenzi wa ufundi wa Chelsea, Michael Emenalo, si watu wa kusitasita linapokuja suala la kutimua kocha hata kama aliwapa taji msimu mmoja kabla.

“Chelsea ni klabu iliyoundwa kibiashara, ina hasira kali na mafanikio. Ni kama vile Real Madrid ilivyo. Kwao suala la kumthamini kocha kama zilivyo timu nyingine ni mtihani sana.

“Hawaogopi kutimua kocha mwenye hadhi yake baada ya miezi 12, lakini si jambo la kulalama sana, ukitazama hata mafanikio ya Chelsea kwa kiasi kikubwa yamechangiwa na uwepo wa Abramovich,” aliongeza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here