SHARE

UONGOZI wa timu ya soka ya Azam FC, inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, umeeleza nia yake ya kusitisha mchakato wa kutafuta kocha kutoka nje na badala yake itawatumia wazawa waliopo.

Awali klabu hiyo yenye maskani yake Chamazi jijini Dar es Salaam, ilisitisha mkataba wa Kocha Mkuu, Hans Pluijm na msaidizi wake, Juma Mwambusi, kwa kile walichodai ni timu hiyo kutofanya vizuri.

Badala yake, makocha waliopo katika klabu hiyo, Iddi Cheche na Abdul Mingange, wamepewa jukumu la kuinoa timu hiyo.

Hilo ni jambo muhimu na ni nafasi adhimu kwa makocha hao kujitathmini kwa kuiwezesha timu hiyo kufanya vizuri katika michuano hiyo, lakini pia kuwapa imani viongozi juu ya uwezo wao.

Sisi Dimba mara zote tumekuwa tukiamini kwamba makocha wazawa wana uwezo mkubwa wa kufanya mabadiliko katika soka la Tanzania, kutokana na ufahamu wao juu ya wachezaji wetu na soka lenyewe kwa jumla.

Tumekuwa tukitoa ushauri mara nyingi, tukitaka kuona makocha hawa wazawa wanapewa nafasi ili kuepusha dhana kwamba timu haiwezi kufanya vizuri mpaka iwe na kocha wa kigeni.

Kwa muda mrefu sasa tumekuwa tukishuhudia timu zinazonolewa na wazawa kama vile Mtibwa, Lipuli na nyingine kadhaa zimekuwa zikitoa ushindani wa hali ya juu na wakati mwingine kuzipa wakati mgumu timu zinazofundishwa na makocha kutoka nje.

Tanzania tuna makocha wengi wenye uwezo, hivyo ni vizuri sasa tukafanya tathmini kuona kama ujio wa makocha wa kigeni umetufikisha wapi na faida yake nini.

Hii itatubadilisha na kuanza kuthamini vyetu kwa kuwaendeleza wakufunzi wetu wa soka na hapo baadaye nchi nyingine nazo zitahitaji kupata makocha kutoka kwetu.

Tunawapongeza makocha Cheche na Mingange kwa kupewa heshima pale Azam, tunaamini wataipokea heshima hiyo kwa kuisimamia vizuri timu yao ili iweze kufikia matarajio waliyojiwekea.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here