Home Habari AZAM KUFA NA MTIBWA J’TANO

AZAM KUFA NA MTIBWA J’TANO

1192
0
SHARE

NA EZEKIEL TENDWA

AZAM FC wanajua kwamba hawawezi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu kutokana na nafasi waliyopo lakini wamejiandaa kuwashushia kipigo kitakatifu Mtibwa Sugar, Jumatano ya wiki ijayo.

Azam ambao wapo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi, watakuwa wenyeji wa Mtibwa Sugar, mchezo utakaochezwa Uwanja wa Azam Complex uliopo nje kidogo mwa Jiji la Dar es Salaam.

Katika msimamo huo, Azam wamejikusanyia pointi 69 wakicheza michezo 36 na kubakiwa na michezo miwili mkononi ambayo hata wakishinda hawawezi kufikia pointi 83 walizonazo Yanga inayoshika nafasi ya pili.

Hata Azam pia wakifungwa michezo miwili iliyobakia ikiwamo huo dhidi ya Mtibwa Sugar, haitawaathiri chochote kwani nao hawawezi kuondolewa nafasi ya tatu wala hawawezi kupiga hatua mbele.

Licha ya hali kuwa hivyo lakini wenyewe Azam wamejiapiza kuwa hawawezi kukubali kupata matokeo mabaya kwenye michezo hiyo na lazima washinde ili kulinda heshima yao.

Kocha wa kikosi hicho, Idd Nassor ‘Cheche’, alisema watahakikisha wanapata matokeo mazuri kwenye mchezo huo licha ya kwamba utakuwa mgumu kwa pande zote.

“Utakuwa mchezo mgumu kwani kila timu inahitaji ushindi lakini kwa upande wetu tumejipanga vizuri kuhakikisha tunapata matokeo mazuri licha ya kuwa hatupo kwenye mbio za ubingwa,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here