SHARE

NA MAREGES NYAMAKA,

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, Azam wanatarajia kushuka dimbani leo kukipiga na Mbabane Swallows ya Swaziland, huku wakiahidi kufia uwanjani ikibidi ilimradi waondoke na ushindi.

Wanalambalamba hao jana mchana waliondoka rasmi katika kambi ya muda mjini Pretoria, Afrika Kusini kwenda Swaziland, wakifikia Lugogo sun Hotel, kabla ya kushuka dimbani kuwavaa wenyeji wao hao katika mechi ya michuano hiyo.

Meneja wa kikosi hicho, Philipo Alando, aliliambia DIMBA kwa njia ya simu kuwa ndani ya siku tatu walizoweka kambi Pretoria walifanya mazoezi ya nguvu huku akikazia zaidi safu ya ushambuliaji.

“Kila kitu kinakwenda sawa, wachezaji wako kwenye morali ya hali ya juu kupambana, kocha Cioaba (Aristica) ndani ya siku chache tulizokuwa Pretoria alifanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika mchezo wa awali.

“Kwa upande wa nahodha John Bocco, bado ni nusu nusu kucheza lakini tunaamini wachezaji waliopo katika nafasi hiyo watafanya vizuri zaidi,” alisema Alando.

Katika mtanange huo wa leo, Azam watatakiwa kupata ushindi au sare yoyote ili waweze kuvuka hatua ya mtoano.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here