Home Habari BADO SAA 120 OKWI KUTUA MSIMBAZI

BADO SAA 120 OKWI KUTUA MSIMBAZI

452
0
SHARE

NA SAADA SALIM,

HAIJALISHI kwamba atakuja kwa kificho au kwa kujionyesha, lakini taarifa njema kwa mashabiki wa Simba ni kwamba, Emmanuel Okwi atatinga jijini Dar es Salaam ndani ya siku tano kuanzia leo Jumapili kumalizana nao moja kwa moja.

Straika huyo kwa sasa yupo Cape Verde, katika majukumu yake ya timu ya Taifa ya Uganda ‘The Cranes’ kwa ajili ya michuano ya kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2019, na taarifa kutoka Simba zinadai kuwa akirudi tu moja kwa moja atakuja nchini kumalizana na uongozi.

Okwi ni miongoni mwa wachezaji ambao huwa wanapokuja nchini wanakuja kwa kificho, mfano mzuri ni kipindi kile alivyosaini Yanga, ambapo alikuja na kusaini kisha akaondoka kwa kificho na sasa anatarajiwa kutua Dar es Salaam kumalizana na Simba.

Awali DIMBA liliripoti kwamba, mchezaji huyo ameingia makubaliano ya miaka miwili kutumikia timu hiyo baada kufanya mazungumzo na viongozi wa Simba na sasa kilichobakia ni kumalizana kwa mambo machache yaliyobakia, zoezi ambalo litakamilika siku hizi chache.

Kigogo mmoja ameliambia DIMBA kwamba, straika huyo atakapomaliza majukumu yake na timu yake ya Taifa, atakuja moja kwa moja Tanzania na atapokelewa na uongozi ambapo pande zote mbili zitamalizia makubaliano yao ili waendelee na mambo mengine.

“Yeye yupo na timu yake huko Cape Verde, lakini wakishamaliza tu mchezo wao, yeye atakwenda kwao Uganda labda kuweka tu mabegi yake na baada ya hapo anakuja Dar es Salaam kwa ajili ya kumalizia mazungumzo yetu.

“Unajua Okwi ni kijana wetu, hawezi kusahau tulipotoka na sisi hatuwezi kumsahau kutokana na kazi aliyoifanya, ndiyo maana baada ya kujiridhisha kwamba bado anacho kiwango kikubwa, tumeamua kumrejesha,” alisema kigogo huyo.

Kigogo huyo alisema Kamati ya Usajili na Kamati nzima ya utendaji wanafanya usajili kulingana na matakwa ya benchi lao la ufundi, ikizingatiwa kuwa wanataka kufanya makubwa michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika mwakani.

“Msimu ujao tunahitaji kufanya vizuri katika ligi pamoja na michuano ya kimataifa, tumeshindwa kushiriki michuano hiyo kwa miaka minne na sasa tumeipata nafasi hii, lazima tuitumie vizuri, huu usajili tunaoufanya ni kutokana na mapendekezo ya benchi la ufundi,” alisema.

DIMBA lilimtafuta Okwi, ambaye alikiri kwamba amefanya mazungumzo na Simba kwa muda mrefu na kwamba atakuja Tanzania muda wowote kumaliza zoezi hilo.

“Kwa sasa siwezi kusema mengi, ila kwa ujumla nilishafanya mazungumzo na Simba, hivyo tusubiri muda utazungumza, nadhani siku chache zijazo nitakuja Tanzania,” alisema.

SHARE
Previous articleKIJIWE CHETU
Next articleNGOMA ATULIZA MZUKA YANGA SC

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here