Home Michezo Afrika BAHATI MBAYA TSHISHIMBI KAMKUTA MAGUFULI, IKULU

BAHATI MBAYA TSHISHIMBI KAMKUTA MAGUFULI, IKULU

1646
0
SHARE

ILIWAHI kumtokea Fally Ipupa. Mshahara wa mwaka wa mwandishi wa habari wa Tanzania, aliupata ndani ya dakika moja tu, akiwa juu ya jukwaa hapa Dar es salaam.

Ilimtokea pia Christian Bella. Dakika tano alizotumia kwenye jukwaa la Bongo Star Search, zilitosha kumpatia ada aliyotumia mzee Kamwe kunisomesha mpaka nilipoyachoka madaftari. Nani alijali? Bongo ilikuwa Bongo kweli!

Wabongo tulicheza sana na pesa, tuliizoea mno. Haikuwa ajabu kutunzana hadi milioni 5 kwa burudani unayoweza kuipata sebuleni kwako ukipata juisi fresh ya parachichi.

Fally alivuna pesa ya kutosha. Mpaka leo Bella hakumbuki ni lini tena alipata pesa nyingi akiwa jukwaani kama ile aliyopata mbele ya mboni za Salama Jabir na Madam Ritta. Ilikuwa kawaida mno kucheza na pesa.

Ikawa hivyo kwenye majukwaa ya burudani, mpaka viwanjani. Kila aliyejitolea kuziburudisha nyoyo za mashabiki, alirudi nyumbani kwake akiwa milionea.

Mrisho Ngassa kavuna sana kwenye shamba hili. Juma Kaseja kavuna sana. Jerry Tegete kabeba sana posho hizi. Haikuwa ajabu tena.

Hata wachezaji nao walijiandaa na kuzoea utamaduni huu. Zilipokosekana pesa, ungepewa kiroba cha mchele kama alivyopewa Simon Msuva kipindi kile. Wabongo tulikuwa jeuri mno wa mifuko.

Bahati mbaya kwa Papy Kabamba Tshishimbi. Baada ya kufanya zaidi ya vile vilivyozoeleka vikifanywa na Frank Domayo, ametoka katika geti la uwanja wa Taifa, mikono mitupu.

Ameishia kupata heshima ya kulisikia jina lake likiimbwa majukwaani. Hakuna pesa tena za kuchezea. Bahati mbaya sana Tshishimbi amekuja Bongo, pale Magogoni tukiwa na Dk. John Pombe Magufuli.

Yale maisha ya kifalme waliyoishi kina Okwi na Niyonzima, ataishia kuyasoma tu kwenye magazeti. Pesa imekata!

Najaribu kuwaza nje ya boksi, kwa uwezo ule ulionyeshwa na Tshishimbi. Kuutawala mchezo atakavyo, angetoa na utajiri gani baada ya zile dakika 90?

Alitupa kila kitu tunachopenda kukiona uwanjani. Alihimili mchezo, alipotakiwa kutoa pasi alitoa, alipotakiwa kukokota, alifanya hivyo, nini Tshishimbi hakukifanya?

Kanzu? Alimvisha Okwi mapema sana kwenye kipindi cha kwanza. Nini tena? Tobo? Nenda kamuulize kilichomtokea Muzamiru Yassin. Hakuna alichobakiza Tshishimbi, alitupatia kila kitu.

Tulitakiwa kumlipa zaidi kwa burudani ile, kumlipa zaidi ya tulivyomlipa Bella nyakati zile. Lakini tatizo ni lile lile nililolisema hapo juu. Ikulu iko chini ya John Pombe Magufuli.

Amenyimwa pesa za mapedeshee, amepewa heshima inayotakiwa kwenye soka. Heshima ya kulisikia jina lake jukwaani likitajwa kwa furaha.

Ni lini tena unakumbuka Wabongo waliliimba jina la mchezaji jukwaani? Miaka mitano ya ufalme wa Niyonzima, pale Jangwani, hakupata heshima hiyo. Imetokea kwa Tshishimbi kama zawadi ya burudani aliyowapa Watanzania. Ahsante Papy!

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here