Home Michezo Kimataifa Kasi ya Bale kwa mshahara yawatisha Messi, Ronaldo

Kasi ya Bale kwa mshahara yawatisha Messi, Ronaldo

630
0
SHARE

MADRID, Hispania

AISEE! Kwa mshahara huu mpya ambao winga Gareth Bale atakuwa anaupata kila wiki pale Real Madrid, ni wazi atakuwa na uwezo wa kugeuza majira haya ya kipupwe na kuwa kiangazi tena.

Mapema wiki hii, Bale alisaini mkataba mpya ambapo kipengele cha mshahara kiliongezwa zaidi, sasa atakuwa anakusanya pauni 346,000 kwa wiki.

Lakini bado raia huyo wa Wales hakuweza kuongoza kwenye orodha ya wanasoka matajiri zaidi, licha ya kutia saini kwenye mkataba utakaomwingizia pauni milioni 108 ndani ya miaka sita ijayo.

Ataweka mfukoni kiasi chote hicho cha fedha, lakini bado ataendelea kutembea kwenye vivuli vya Cristiano Ronaldo na Lionel Messi ambao wanatesa viwanjani na upande wa uchumi.

Mastaa hao wawili wanachota mshahara unaoaminika kufikia pauni 365,000 kwa wiki, ni jumla ya pauni milioni 19 kwa kila mmoja wao na kila mwaka baada ya makato ya kodi.

Madrid na Barcelona zinafanya malipo yao ya mishahara kwa kiasi kinachobaki baada ya chombo cha kushughulika na kodi Hispania kukata kiasi chake, ikiwa na maana kwamba Ronaldo na Messi wanaongoza orodha ya wachezaji matajiri kwa kiasi kikubwa zaidi.

Iwapo mishahara ya wachezaji wa Barca na Madrid ingekuwa inajadiliwa kama ya wale wa Ligi Kuu England, hiyo ni kabla ya makato ya kodi  kutoka kwenye mishahara yao hiyo, mkataba mpya wa Bale ungekuwa ni wa thamani mno. Mapato yanayoingia Hispania kutokana na kodi za wachezaji ni asilimia 45 na hapo Real wangeonekana kumlipa Bale mshahara wa pauni milioni 32.7 kwa mwaka au pauni 629,000 kwa wiki.

Kwa mfumo huo huo, Madrid na Barca wangekuwa wanawalipa Ronaldo na Messi pauni 664,000 kwa wiki, sawa na pauni milioni 34.5 kwa mwaka.

Madrid wamesisitiza kuwa, kipato anachokipata Bale kwenye mkataba wake ni pauni milioni 18 kwa mwaka, ingawa mtandao wa Daily Mail unaelewa kwamba kiwango ni kikubwa zaidi kutokana na jumla ya kiasi kinacholipwa kwenye kodi.

Mchezaji anayechukua mshahara mwingi Ligi Kuu England ni Paul Pogba aliyerudi Manchester United kwa ada ya uhamisho pauni milioni 89 kutoka Juventus. Kwa wiki anakusanya pauni 290,000  na pauni milioni 15 kwa mwaka.

Licha ya United kuwa na mwenendo usioridhisha tangu alipostaafu Sir Alex Ferguson, bado ina wachezaji watatu waliopo kwenye orodha ya wachezaji 10 bora wanaoongoza kwa mshahara mkubwa duniani, wakiongozwa na Pogba, Wayne Rooney (pauni 260,000 kwa wiki, pauni mil.13.5 kwa mwaka) na Zlatan Ibrahimovic (pauni 250,000 na pauni mil.13 kwa mwaka).

Majirani zao, Manchester City wana wachezaji wawili waliopo kwenye orodha hiyo; Sergio Aguero na Yaya Toure, wote wakichukua pauni 240,000 kwa wiki.

Aguero hajapata nafasi ya kutosha ya kucheza chini ya uongozi wa Pep Guardiola msimu huu, bado anachukua pauni milioni 12.5 kwa mwaka.

Kwa kuliwekwa sawa suala hili, wastani wa mishahara barani Ulaya mwaka huu 2016 ni pauni 27,500 kwa wiki, wakati huo Waziri Mkuu wa England, Theresa May anaweza kukamata mshahara wa pauni 143,462 kwa kuiongoza nchi hiyo zaidi ya miezi 12 ijayo, ikiwa ni nusu ya kiasi anachokikamata Pogba katika mshahara wake kila wiki.

Ligi nyingine ambazo zinalipa mishahara minono, hapa haitatajwa Serie A au Bundesliga, lakini ni Chinese Super League (Ligi Kuu ya China).

Kama ukisimama mbele za watu na ukataja jina la Graziano Pelle miongoni mwa wachezaji bora duniani, utachekwa aisee!

Lakini Muitaliano huyo naye anapokea mshahara mnono zaidi duniani kwa sasa.

Uhamisho wa Pele kutoka Southampton kwenda Shandong Luneng ya huko China uligharimu pauni milioni 13, lakini atakusanya mshahara mkubwa zaidi ya ule aliokuwa akiupata ambao ni pauni 260,000 kwa wiki.

Anayekamilisha orodha ya wachezaji 10 wanaolipwa mshahara mkubwa zaidi ni mshambuliaji wa Brazil, Hulk, anayekipiga katika klabu ya Shanghai SIPG.

Licha ya kutocheza kwenye moja ya ligi kubwa zaidi za Ulaya, Hulk, mwenye umri wa miaka 30, ni mchezaji wa nne kulipwa mshahara mkubwa wa pauni 317,000 kwa wiki.

Rekodi ya mabao ya kimataifa, Hulk amefunga mabao 12 ndani ya michezo 48, halafu analipwa mshahara wa pauni milioni 16.5 kwa mwaka. Cha kushangaza ni kwamba rekodi yake ya mabao ya kimataifa imeizidi ile ya mshambuliaji wa zamani wa England, Emile Heskey.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here