SHARE

CATALUNYA, Hispania

HALI inazidi kuwa tete kwa kiungo mshambuliaji wa zamani wa timu ya taifa ya Brazil, Ronaldinho, katika kesi yake ya kuingia Paraguay kwa kutumia hati feki ya kusafiria.

Ronaldinho na kaka yake, Roberto de Assis, wanaendelea kusota gerezani wakisubiri uchunguzi si tu wa kesi hiyo bali nyingine ya utakatishaji fedha iliyoibuka hivi karibuni.

Endapo watakutwa na hatia kwa makosa hayo, sheria za Paraguay ziko wazi kuwa Ronaldiho aliyesherehekea siku yake ya kuzaliwa jana na kaka yake watatumikia kifungo cha gerezani kwa miezi sita.

Sasa, klabu ya Barcelona aliyowahi kuichezea kwa mafanikio makubwa, ikiwamo kuipa mataji mawili ya La Liga na moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya, imejiweka kando na kile kinachomkuta staa huyo.

Hatua ya Barca kumkwepa Gaucho imeripotiwa na gazeti la SunSport, ikiongeza kuwa klabu hiyo haitahusika kwa chochote juu ya majanga yake, licha ya kwamba aliondoka Catalunya akiwa amewapachikia mabao 94 katika mechi 207.

Uamuzi huo unakuja wiki chache tangu nyota wa timu hiyo, Lionel Messi, naye alipokanusha taarifa zilizodai kwamba angezama mfukoni na kutoa kiasi cha fedha kumsaidia mchezaji mwenzake huyo wa zamani.

Taarifa alizokanusha Messi, nahodha wa Barca na timu ya taifa ya Argentina, ni zile za kutaka kutuma Pauni milioni tatu (zaidi ya Sh bil. 8 za Tanzania) nchini Paraguay ili Ronaldinho aachiwe huru.

Hata hivyo, hilo halikuwa la kushangaza sana kutokana na ukweli kwamba mwaka jana Ronaldinho alikataa madai kuwa Messi ndiye mchezaji bora wa muda wote na badala yake aliwataka wakongwe Diego Maradona, Pele na Ronaldo (De Lima).

Juu ya kesi ya utakatishaji fedha, imeelezwa kuwa Ronaldinho alikwenda Paraguay kumfuata mwanamama aitwaye Dalia Lopez, ambaye kwa pamoja wanafanya biashara hiyo.

Awali, bibiye huyo ambaye ni mfanyabiashara alitarajiwa kwenda mahakamani kuzungumzia hilo ili walau kumpa afueni Ronaldinho lakini hakutokea kwa kile kilichoelezwa na madaktari wake kuwa ni afya yake kutokuwa sawa.

Huku akisubiri uchunguzi unaoendelea, ambao unaweza kumsweka gerezani kwa miezi sita endapo utakamilika na kumkuta na hatia, Ronaldinho anatajwa na vyombo vya habari vya Paraguay kuwa ni mtu asiye na furaha, licha ya kwamba hajapoteza tabasamu lake.

Jaribio lake lililogonga mwamba ni lile la kuwa nje kwa dhamana, ambalo lilitupiliwa mbali, hivyo kuendelea kuishi kwenye gereza lenye wafungwa na mahabusu 200, wakiwamo wauza ‘unga’ na wahalifu wengine.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here