Home Makala BARCELONA VS ATLETICO MADRID NI VITA YA MSN VS GGT

BARCELONA VS ATLETICO MADRID NI VITA YA MSN VS GGT

676
0
SHARE

NA NIHZRATH NTANI

NI kaskazini mashariki mwa Hispania, umbali wa kilomita 623.9. Unatumia saa 5 na dakika 45 kwa gari kutoka katika jiji la Madrid na kulikuta jiji la Barcelona.

Ni katika jiji hilo la Barcelona lenye wakazi wasiopungua milioni 1.6 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2015, ndiko kunakosemekana kuwa ndio kitovu cha bahari ya Mediterranean.

Usiku wa Jumatano ya leo Septemba 21, saa 5:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki na Kati, macho na masikio ya wapenzi wa soka kote ulimwenguni yataelekezwa kunako katika dimba la Camp Nou. Huko kutakuwa na vita ya wanaume watupu. Shauku iliyoje!
Barcelona watawakaribisha wababe wa jiji la Madrid, Klabu ya Atletico Madrid, katika mechi ngumu kabisa kwa pande zote mbili na inayosubiriwa kwa hamu kubwa. Kwa kifupi mtoto hatumwi dukani leo.

Timu zote mbili zitakuwa mikononi mwa mwamuzi David Fernandez Borbalan. Mmoja wa waamuzi bora kwa sasa nchini Hispania. Ni mwamuzi huyu ambaye amepewa nafasi ya kuwa ‘hakimu’ katika mechi hii inayochukuliwa kuwa bora na yenye upinzani mkubwa kwa wakati huu. Baada ya dakika 90 atatupa majibu.

NI LUIS ENRIQUE VS DIEGO SIMEONE

Katika watu watakaokuwa na nyakati ngumu usiku wa leo, ni wanaume hawa wawili. Tangu amewasili Barcelona Juni 2014, Luis Enrique ameiongoza Barcelona katika mechi 8 dhidi ya Atletico Madrid ya Diego Simeone kwa mashindano yote.

Takwimu dhidi yao hazidanganyi. Katika mechi hizo 8, Enrique ameibuka kidedea katika mechi 7, huku akipoteza mechi moja tu dhidi ya mpinzani wake huyo. Kwa takwimu hizi Enrique anaonekana mbabe dhidi ya mwenzake.

Enrique, anayependelea mfumo wa 4-3-3, usiku wa leo anaweza kukutana na wakati mgumu mbele ya Diego Simeone, anayependelea mfumo wa 4-4-2 ama 3-4-3. Mechi yao inaweza kuwa tofauti leo.

NI VITA YA MSN V GGT

Miaka michache iliyopita nchini Hispania kuliibuka kombinesheni iliyobatizwa jina la BBC, ikiwa ni mjumuiko wa Galeth Bale, Benzema na Cristiano Ronaldo klabuni Real Madrid.

Mwaka mmoja baadaye Barcelona nao waliwajibu kwa MSN ikiwa kifupisho cha Messi, Suarez na Neymar. Ni kombinesheni inayochukuliwa kuwa kali zaidi ya ile ya BBC.

Mambo hubadilika, wahenga walinena. Msimu huu baada ya BBC kuonekana imepoteza makali yake imeibuka kombinesheni mpya kabisa kunako klabu ya Atletico Madrid iliyopewa jina la GGT, ikiwa ni kifupi cha washambuliaji wake Griezmann, Gameiro na Torres.

Timu hizi mbili tayari zimekwishacheza jumla ya mechi nne hadi hivi sasa, huku MSN wakitupia jumla ya mabao tisa, Messi na Suarez kila mmoja akiwa na mabao manne, huku moja likifungwa na Neymar.

Kwa upande wao GGT, wao wana mabao 8, ambapo Antonie Griezmann yuko kileleni akiwa na mabao manne, huku Torres na Gameiro wakiwa na mabao mawili kila mmoja. Ni usiku wa leo Nou Camp utatupa majibu ipi bora kati ya hizo kombinesheni mbili.

UBORA NA UDHAIFU WAO

Barcelona inatisha katika ushambuliaji. Ni ngumu mno kuuzuia ‘utatu’ wa washambuliaji wao. Uwezo wao wa kupiga pasi fupi fupi na za haraka unawafanya wawe imara zaidi kwenye kiungo. Wana viungo wabunifu mno na wanaoendana na staili yao ya ‘tiki taka.’
Udhaifu wao ni sehemu ya ulinzi. Kuondoka kwa Dan Alves kumepelekea mpaka sasa washindwe kumfahamu mrithi wake sahihi.

Wameweza kuwatumia Alex Vidal, Rafinha na Sergio Roberto katika nafasi ya beki wa kulia, lakini bado inaonekana kuna tatizo.
Pia beki yao haipo makini sana. Inafanya makosa mengi ambayo kwa safu kali ya ushambuliaji inaweza kujikuta ikitabasamu kila mara.

Ni wabovu zaidi kwa mipira ya kushtukiza (counter attack).
Wakati Atletico Madrid ikisifiwa na safu ngumu za ulinzi kwa miaka yote, msimu huu wamekamilika.

Wana wachezaji bora na imara mno kuanzia golini hadi mbele. Wanajituma kwa muda wote wa mchezo. Ni wazuri sana kwa kuwatumia viungo wa pembeni. Barcelona wanapaswa kuwachunga sana akina Koke, Saul Niguez na Yannick Ferreira Carraso.

Udhaifu wa Atletico Madrid ni kukosa umakini wa kucheza na mipira ya kuotea (Offside), wamekuwa wakifungwa mabao mengi ya aina hiyo. Pia si wazuri sana kwa mipira ya krosi kwa walinzi wao. Bila shaka utamu wa La Liga unaanza usiku huu.

Kwingineko katika dimba la Santiago Bernabeu, Zinedine Zidane usiku huu atakuwa anajaribu kuweka rekodi ya kushinda mechi 17 mfululizo kwenye La Liga. Ni baada ya Jumapili iliyopita kuivunja rekodi ya Pep Guardiola aliyoiweka katika msimu wa 2010/2011 kwa kushinda mechi 16 mfululizo akiwa na Barcelona.

Real Madrid watakuwa wenyeji wa Villareal, katika mechi nyingine ya kukata na shoka nchini Hispania. Kila shabiki wa Barcelona, Atletico na Real Madrid macho yatakuwa yakimuombea mwenzake mabaya.

Real Madrid wakiwa kileleni mwa La Liga kwa pointi 12, ni ushindi wao mbele ya Villareal utakuwa na maana kubwa kwao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here