Home Habari BATA LA UBINGWA SIMBA NI KUFURU

BATA LA UBINGWA SIMBA NI KUFURU

8564
0
SHARE
NA CLARA ALPHONCE, SINGIDA    |  

SIMBA jana walicheza na Singida United na kuibuka na ushindi wa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Namfua, mkoani Singida, ikiwa ni mwendelezo wa sherehe za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, walioutwaa tangu Alhamisi, wiki hii.

Wekundu hao wa Msimbazi walitangazwa rasmi kuwa mabingwa wapya wa msimu huu wa 2017/2018, baada ya watani wao wa jadi, Yanga, kufungwa na Prisons mabao 2-0, Uwanja wa Sokoine, mjini Mbeya.

Hiyo iliwafanya Simba kufikisha pointi 65, walizokuwa wamepata katika michezo 27, ambazo hazitafikiwa na timu nyingine yoyote kabla hata ya kucheza mechi yao ya 28 jana, ambapo walifikisha pointi 68 baada ya ushindi dhidi ya Singida United.

Yanga, yenye pointi 48 sasa na ambayo ina mechi tano mkononi, kabla ya kushuka dimbani leo Jumapili kukipiga na Mtibwa Sugar, inaweza kuishia pointi 63 tu hata ikishinda mechi zote, wakati Azam FC, inayoshika nafasi ya pili nyuma ya Simba, inaweza kufikisha pointi 57.

Kilichobaki sasa ni kwa Simba kula bata tu, baada ya kutwaa ubingwa na Wekundu hao wa Msimbazi wameamua kusherehekea katika mikoa mitatu kudhihirisha kuwa, wamepania kuwapa raha mashabiki wao ambao wameusubiri kwa miaka mitano mfululizo.

Mabingwa hao wapya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, walizianza sherehe hizo jana mkoani Singida, kikosi chao kilipocheza na Singida United, mchezo uliokuwa kama wa kutafuta tu heshima, kwani hawakuwa na chakupoteza.

Leo Jumapili mashabiki wa Mkoa wa Dodoma itakuwa zamu yao, kwani jeshi zima la Wekundu hao litakuwa hapo kwa ajili ya kucheza mechi moja dhidi ya wenyeji Dodoma Combine Area C.

Baada ya hapo wachezaji na viongozi wao watapata chakula safi ambacho wameandaliwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, ambaye huwa hafichi furaha yake timu hiyo inapopata matokeo mazuri.

 

Na kesho Jumatatu, timu hiyo itaibukia Bungeni Dodoma kwa mwaliko aalumu kutoka kwa wabunge ambao ni mashabiki wa kutupwa wa Wekundu hao wa Msimbazi, wakiongozwa na Spika Ndugai.

Kaimu Rais wa Simba, Abdallah Salim ‘Try Again’, amelithibitishia DIMBA kuwa, baada ya hapo watarejea jijini Dar es Salaam, na hapo watafanya sherehe kubwa kuwapongeza wachezaji wao na pia kutoa shukrani kwa mashabiki kwa jinsi walivyotoa ushirikiano mkubwa tangu Ligi ilipoanza.

“Ratiba yetu ipo kama hivyo nilivyokwambia na tunatarajia tukiwa Dar es Salaam, tutaungana na mwenzetu, Mohamed Dewji (Mo Dewji), ambaye kwakweli amekuwa bega kwa bega na sisi kwa kila hali.

“Tunawashukuru sana wachezaji wetu kwa jinsi walivyopambana mpaka kupata ubingwa huu, lakini pia mashabiki wetu ambao tangu kuanza kwa Ligi wameonyesha umoja na mshikamano wa hali ya juu,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here