SHARE

MUNICH, Ujerumani

MWANZONI ilionekana Borussia Dortmund wamemaliza kazi mapema baada ya kuanza vizuri katika Ligi Kuu ya Ujerumani, Bundesliga, huku wapinzani wao Bayern Munich wakichechemea kwa matokeo mabaya.

Kuelekea katika michezo ya mwisho ya Ligi Kuu ya Ujerumani wikiendi hii, wababe wawili wa ligi hiyo wamekuwa katika moto mkali huku ikiwa ni mara ya kwanza kwenye historia mshindi kupatikana siku ya mwisho.

Matokeo ya wikiendi iliyopita yalichochea kasi hiyo baada ya vinara Bayern Munich kupata suluhu dhidi ya RB Leipzig huku wapinzani wao, Borussia Dortmund wakishinda kwa tabu mabao 3-2 dhidi ya Fortuna Dusseldorf.

Ilikuwa rahisi kwa kila mmoja kuamini kuwa Bayern Munich wamepoteza nguvu katika ligi hiyo ya kibabe na nafasi yao inachukuliwa na Borussia Dortmund ambao tangu kuanza kwa ligi hiyo wapo kileleni.

Lakini baada ya michezo ya wikiendi iliyopita mambo yanaonekana kubadilika kwenye ligi hiyo, hivi sasa Bayern Munich wanaongoza kwa tofauti ya pointi mbili, yaani wanazo 75 na Borussia Dortmund wamekusanya 73.

Machi 1 mwaka huu, ilikuwa rahisi kwa Bayern Munich kuwafikia Borussia Dortmund ambao walifungwa mabao 2-1 na Augsburg huku Munich wakishinda mabao 5-1 dhidi ya Borussia Monchengladbach.

Lakini Borussia Dortmund waliendeleza moto wao wa ushindi tofauti na Bayern Munich ambao walishindwa kupata ushindi michezo mingi mfululizo na kuwapisha vijana wa Lucien Favre kileleni baada ya kuongoza kwa muda.

Desemba mwaka jana, Borussia Dortmund waliwazidi Bayern Munich pointi tisa, baadaye zilibaki sita baada ya vinara hao kufungwa na Fortuna Dusseldorf.

Safari ilionekana kuwa ngumu kwa Bayern Munich kupunguza pengo la pointi na kujikuta wakiachwa saba baada ya mabingwa hao kufungwa mabao 3-1 na Bayer Leverkusen huku Borussia Dortmund wakitoa sare ya bao 1-1 na Eintracht Frankfurt.

Haijawahi kutokea kwenye historia ya Bundesliga kwa timu kupitwa pointi saba na kuweza kutwaa taji hata kama watakuwa sawa kwa pointi na vinara, je, Bayern Munich ataweza kutetea ubingwa wake?

MAJERUHI

Mwanzoni mwa ligi hiyo, kikosi cha Bayern Munich kilikuwa na wachezaji majeruhi wengi ambao walipelekea timu hiyo kuanza taratibu na kukosa matokeo mazuri kila walipoingia uwanjani.

Baadaye baadhi ya wachezaji nyota kurejea kikosi hicho cha mabingwa mara tano mfululizo kilianza kufanya vizuri na kuwafukuzia waliokuwa vinara wa ligi hiyo, Borussia Dortmund kwa kasi kubwa.

Lakini mambo yanaonekana kubadilika hivi karibuni, Borussia Dortmund wanakabiliwa na majeruhi ya baadhi ya wachezaji wao nyota.

Inawezekana hilo linachangia kwa kiasi kikubwa klabu hiyo kuanza kufanya vibaya sababu kocha wao, Favre anakosa machaguo mengi ya wachezaji pindi anapowahitaji.

UZOEFU

Kwa kiasi kikubwa kikosi cha Bayern Munich kimezungukwa na wachezaji wazoefu ambao wametwaa mataji mengi ndani ya timu hiyo.

Inawezekana kwa hali ilipofika wakawa wajanja zaidi ya damu changa za Borussia Dortmund ambao kwa kiasi kikubwa hawajawahi kushinda mataji hata wazoefu ambao wapo walitwaa ubingwa misimu saba iliyopita.

Uzoefu unaweza kuwa chachu ya kuzitenganisha timu hizo zilizopo kileleni huku wakitofautiana kwa pointi mbili tu.

Hivi karibuni, Borussia Dortmund walipata pointi tatu tu kutoka kwenye timu zilizopo katika hatari ya kushuka daraja msimu huu.

Bayern Munich wakichukua pointi tisa kwenye michezo minne dhidi ya klabu hizo zinazoshika mkia kwenye Bundesliga.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here