SHARE

LOS ANGELES, Marekani

KATI ya mastaa walioumaliza mwaka 2018 kwa machungu hutaacha kulitaja jina la mwigizaji mwenye jina kubwa kwenye filamu, Bill Cosby.

Ikiwa imebaki takribani miezi mitatu kabla ya mwaka 2019 kuingia, yeye alikuwa mahakamani na mwishowe hakimu akaamua Cosby akatumikie kifungo cha miaka mitatu gerezani.

Kilichomponza babu huyo mwenye umri wa miaka 81, ni kesi ya muda mrefu iliyokuwa ikimkabili ya kumfanyia vitendo vya udhalilishaji mwanadada Andrea Constand, tukio ambalo hata hivyo ni la miaka 14 iliyopita.

Katika maelezo yake, Constand alisema siku moja ndani ya mwaka 2014, Cosby alimwalika nyumbani kwake na alipokwenda alimpa vidonge vilivyompa usingizi na kisha kumbaka.

“Nilidhani (vidonge) vingeniondolea uchovu kama alivyoniambia. Lakini baada ya nusu saa tu, nilianza kushindwa kuongea na sikuweza tena kuongea,” alisema Constand kuiambia mahakama.

Licha ya wanasheria wake kuomba mwigizaji huyo apewe dhamana, mahakama iligoma na kumtaka Cosby mzaliwa wa Philadelphia, aende gerezani tu.

Alitaka soka akawa mchekeshaji

Katika miaka ya 1960, Cosby hakuwa na mpango wa kuwa mwigizaji na badala yake akili yake ilikuwa kwenye mchezo wa kandanda. Mara nyingi alikuwa akionekana viwanjani ingawa hakuwahi kuzichezea timu kubwa wala kujiunga na ‘academy’ zao.

Kipaji chake cha kuimba kilibainika pia kwani moja kati ya ngoma zake ilishika nafasi ya kwanza katika orodha ya 40 bora mwaka 1969.

Alianza kuchekesha akiwa chuo

Ni kweli Cosby aliwahi kuacha shule akiwa sekondari, lakini baadaye alituliza akili na kufika chuo na huko ndiko kipaji chake cha kuvunja mbavu kilipoonekana. Mara nyingi alikuwa kivutio kwa wafanyakazi wa chuoni.

Hata katika hafla mbalimbali zilizofanyika chuoni, alikuwa akipewa nafasi ya kupanda jukwaani kufanya yake hivyo kujizolea umaarufu mkubwa.

Hapo awali, ifahamike kuwa aliwahi kujishughulisha na kazi za kuuza viatu ili tu aweze kuwasaidia wazazi wake waliokuwa hoi kiuchumi.

 ‘Shoo ilimpa mke msomi

Kwa wafuatiliaji wa filamu za vichekesho, Camille Olivia, si jina geni kwao. Ndiye mke wa kwanza wa Cosby. Wawili hao walikutana wakati Cosby akiwa kwenye shoo mjini Washington na hiyo ilikuwa katika miaka ya 1960.

Kipindi hicho, bibiye Camille alikuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Maryland. Cosby ilifunga ndoa na mwanamke huyo mwaka 1964 na walidumu kwa miaka 15.

Kesi zake kuwatesa mademu

Si tu Constand, Cosby ana kesi nyingi za wanawake waliodai kufanyiwa unyanyasaji na staa huyo. Mwaka 2015, mwigizaji wa kike, Louisa Moritz, aliibua shutuma hizo akisema alifanyiwa hivyo mwaka 1969.

Moja ya aibu kubwa alizoibua mwanamke huyo ni kwamba, Cosby alimlazimisha kunyonya sehemu zake za siri wakati wakiwa nyuma ya jukwaa katika moja ya ‘show’ zake.

 Orodha ya wanawake walioteswa na mzee huyo pia inawahusisha Donna Barrett, Sharon Van Ert, Pamela Abeyta, Lisa Christie, Heidi Thomas, Colleen Hughes, Eden Tirl na weingine kibao.

Amekwenda jela akiwa na bil 900/-

Cosby ni miongoni mwa wasanii waliokuwa wakifurahia maisha kutokana na vipato vikubwa vitokanavyo na kazi zao. Ukiacha filamu zake, alikuwa  akiingiza mkwanja mrefu kutokana na dili zake za matangazo.

Hadi anakwenda zake gerezani mwishoni mwa mwaka jana, mzee huyo alikuwa na utajiri Dola za Marekani milioni 400 (zaidi ya Sh bil 900 za Tanzania).

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here