Home Uchambuzi BOCCO ALA SAHANI MOJA NA MAPROO WANAOTESA TUZO ZA MWEZI ZA...

BOCCO ALA SAHANI MOJA NA MAPROO WANAOTESA TUZO ZA MWEZI ZA VPL

5387
0
SHARE

NA MAREGES NYAMAKA


KIUNGO wa Yanga, Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara, Papy Kabamba Tshishimbi, katikati ya wiki alitangazwa na Shirikisho la Soka nchini (TFF), kuwa mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa mwezi Januari wa ligi hiyo.

Tuzo hiyo inatolewa kwa kuzingatia vigezo vinavyohitajika namna ambavyo mchezaji anakuwa ameisadia timu yake ndani ya huo mwezi hasa kukusanya pointi nyingi zaidi.

Kazi hiyo inafanywa kupitia Kamati maalumu ya tuzo inayoundwa na wataalamu mbalimbali miongoni mwao wakiwemo makocha wanaozunguka katika viwanja mbalimbali wakati mechi zikichezwa.

Mshindi anakabidhiwa Ngao na Kingamzi cha Azam FC, ikiwa ni kumbukumbu yake ya kudumu, ikiambatana na zawadi ya fedha taslimu sh milioni moja kutoka kwa mdhamini mkuu wa ligi hiyo,  Kampuni ya Simu za mkononi ya Vodacom.

Hata hivyo kitendo cha tuzo ya mwisho kukabidhiwa kwa Tshishimbi, kimetoa taswira mpya msimu huu tofauti na ilivyokuwa msimu uliyopita, kwani Mcongoman huyo anakuwa mchezaji wa tatu wa kigeni ‘proo’ kuinyakua, tofauti na msimu mzima uliopita ambapo mgeni pekee aliyefanikiwa kuinyakua alikuwa ni beki wa Simba Method Mwanjale pekee, aliyefanya hivyo mwezi Desemba.

Ifuatayo ni orodha ya wachezaji wa kigeni waliotwaa tuzo hiyo msimu huu sambamba na vigezo kadhaa vilivyowabeba ndani ya miezi tofauti kwa straika wa Simba John Bocco, kuweka rekodi, lakini pia wachezaji wa Simba, Yanga na Singida United, kung’ara kwa ujumla.

OKWI (Simba, Agosti)

Straika Emmanuel Okwi, ndiye aliyekuwa mchezaji wa kwanza msimu huu kutwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili, Mohamed Issa wa Mtibwa Sugar  na Boiniface Maganga wa Mbao FC.

Katika kinyanganyiro hicho, Okwi alifanikiwa kuibuka kinara kutokana na kutoa mchango mkubwa ndani ya kikosi chake kuibuka na ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting, akiingia wavuni mara nne.

Ndani ya mwezi kila timu ikicheza mechi moja pekee, Mganda huyo alikuwa ni mchezaji pekee aliyefunga hat-trick, tena ndani ya  kipindi cha kwanza, kabla ya kufunga la nne kipindi cha pili.

Kwa upande wa wapinzani wake, Issa wa Mtibwa Sugar alifunga bao pekee lililoiwezesha timu yake hiyo kuibuka na ushinda wa 1-0 dhidi ya Stand United kama ilivyokuwa kwa Maganga mbele ya Kagera Sugar.

BATAMBUZE (Singida United, Septemba)

Baada ya Okwi kuanza kwa kishindo kutwaa tuzo hiyo, mwezi uliyofuata ilikwenda kwa beki wa kushoto wa Singida United, Shafik Batambuze, aliyewashinda akina Ibrahim Ajib wa Yanga na Mohamed Issa ‘Banka’ anayekipiga Mtibwa Sugar, ambao aliingia nao hatua ya fainali.

Batambuze alifanikiwa kutokana na kuisaidia timu yake kuvuna pointi 10 katika michezo minne aliyoshuka dimbani mwezi huo, akionekana kuwa nyota tegemezi zaidi kuifanya Singida United kukusanya alama nyingi zaidi mwezi huo, tofauti na timu nyingine 15.

Ajib wa Yanga aliyekuwa kwenye kinyanganyro hicho hadi hatua ya mwisho alikuwa ameisaidia timu yake kupata pointi nne akiing’arishinda kushinda mechi mbili, huku Issa Mohamed akiwa kwenye ubora wake kuifanya Mtibwa Sugar kukusanya pointi nane ndani ya michezo minne.

CHIRWA (Yanga, Oktoba)

Mfululuzo wa wachezaji wa kigeni uliendelea kuchukua nafasi mwezi Oktoba ikiwa ni zamu ya straika wa Yanga, Mzambia Obrey Chirwa, aliyeitwaa mwezi Oktoba, akiwagalagaza nyota wa kikosi chake Ibrahim Ajib na beki wa Simba, Erasto Nyoni.

Mabao mawili na pasi mbili ndani ya mechi mbili tofauti ilikuwa chachu ya Yanga kuvuna alama sita, katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Katiba, kabla ya kuwatungua Stand United mabao 4-0 na kuwafanya Wanajangwani hao kuondoka kidedea Kanda ya Ziwa.

Kama hiyo haitoshi, Mzambia huyo aliifungia timu yake bao la kuzawazisha dhidi ya Simba Oktoba 28, mchezo uliyopigwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya bao 1-1 na kuwafanya Yanga kupanda katika msimamo wa ligi kutoka nafasi ya sita hadi ya pili.

Kwa upande wa Nyoni alikuwa ameiwezesha timu yake kupata pointi nane katika michezo minne aliyocheza, akitoa pasi za mabao manne, Simba ikishinda mechi mbili kama ilivyokuwa upande wa sare, huku Ajibu akifunga mabao matatu na pasi moja ya mwisho.

REKODI YA BOCCO

Wakati wachezaji wa kigeni wakionekana kuwa msaada kwa vikosi vyao hivyo, mzawa na nahodha wa Simba Bocco ameonekana kutokuwa mbali kwani amefanikiwa kuweka rekodi ya tuzo hizo, zilizoanza kutolewa msimu uliopita.

Bocco anakuwa ni mchezaji pekee aliyetwaa tuzo hiyo mara mbili kabla ya kutwaa mwezi Januari msimu huu, akiitumikia Simba. Aliwahi kuichukua alipokuwa Azam mwezi Agosti msimu uliopita, akiwashinda Mzamirru Yassin wa Simba na Said Kipao wa JKT Ruvu.

Mbali ya kasi hiyo ya maproo pamoja na rekodi ya Bocco, wazawa waliyotwaa tuzo hiyo hadi sasa ni Mudathir Yahya (Singida United-Novemba) na Habibu Kiyombo (Mbao -Desemba).

Wachezaji nyota wa mwezi msimu uliopita (2016/17)

John Bocco(Azam, Agosti)

Shiza Kichuya (Simba, Septemba)

Simon Msuva (Yanga, Oktoba)

Riphat Hamis (Ndanda, Novemba)

Method Mwanjale (Simba,Desemba)

Juma Kaseja (Kagera Sugar, Januari)

Hassan Kabunda(Mwadui, Febururi)

Mbaraka Yusuph (Kagera Sugar, Machi)

Abdulrahaman Mussa (Ruvu Shooting, April)

Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ (Simba, Mei)

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here