Home Habari BOCCO MNYAMA

BOCCO MNYAMA

7505
0
SHARE

 

NA WINFRIDA MTOI, NJOMBE

KUBALI ama kataa lakini straika wa Simba, John Raphael Bocco anatisha. Huo ndio ukweli wenyewe.

Na hii imezidi kujidhihirisha jana baada ya straika huyo kutupia bao zote mbili na kuibeba timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Njombe Mji, katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sabasaba mjini hapa.

Ushindi huo umeifanya Simba kuzidi kujichimbia vizuri kileleni kwa kufikisha pointi 49 na kuwaacha mahasimu wao Yanga wakiwa na pointi zao 46, timu zote mbili zikiwa zimecheza michezo 21.

Bocco alifunga mabao hayo kila kipindi, akianza na la kwanza dakika ya 17 ya kipindi cha kwanza, huku la pili akilifunga dakika ya 64 katika kipindi cha pili.

Katika kipindi hicho cha kwanza, Simba wangekwenda mapumziko wakiwa na zaidi ya bao hilo 1-0 kama wangetumia nafasi kadhaa za wazi, ikiwamo ile aliyoipata Emmanuel Okwi dakika ya pili, akiwa yeye na kipa lakini akashindwa kufunga.

Simba walikosa tena nafasi ya wazi katika dakika ya tano baada ya Bocco na Okwi kushindwa kumalizia krosi ya Shiza Kichuya aliyoichonga kutoka winga ya kushoto.

Kama hiyo haitoshi, dakika ya 11 Bocco akiwa yeye na kipa, alishindwa kumalizia krosi ya Okwi, kwani badala ya kutumbukiza mpira nyavuni, akapiga kichwa cha kuokoa.

Dakika ya 17 ndiyo iliyowafanya Simba kwenda mapumziko wakiwa na bao 1-0 la Bocco ambaye alipokea mpira mrefu wa faulo uliopigwa na Yusuph Mlipili, akaruka yeye na beki wa Njombe Mji, kisha mpira ukatua chini na yeye bila ajizi akaachia shuti kali lililojaa wavuni.

Katika mwendelezo wa Simba kukosa nafasi kipindi hicho cha kwanza, Kichuya alishindwa kufunga bao dakika ya 27, baada ya kupokea pasi ndefu kutoka kwa Nicholaus Gyan, lakini akapiga shuti hafifu likatoka nje.

Katika kipindi hicho cha kwanza, mabeki wa Simba wakiongozwa na Jjuuko Murushid, walihakikisha washambuliaji wa Njombe Mji chini ya Ditram Nchimbi, hawatengenezi nafasi za kuonana na kipa Aishi Manula na ndivyo ilivyokuwa.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Njombe Mji wakitaka kusawazisha bao hilo, lakini wakajikuta wakiongezwa bao la pili dakika ya 64, likifungwa tena na Bocco akimalizia krosi ya Shomari Kapombe aliyoichonga kutoka winga ya kulia.

Katika dakika ya 74, Njombe Mji walishindwa kuwa watulivu na kupoteza nafasi ya wazi huku Simba nao wakishindwa kupata bao la tatu dakika ya 77 na mpaka mpira unamalizika, Wekundu hao wa Msimbazi waliondoka na pointi zote tatu kwa ushindi huo wa mabao 2-0.

Kwa sasa Bocco amefikisha jumla ya mabao 12 sawa na Obrey Chirwa wa Yanga, huku Emmanuel Okwi akiendelea kuwa juu na mabao yake 16.

Katika hatua nyingine, mama mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Ever Michael, alisema yeye ni shabiki mkubwa wa Simba na alilazimika kufunga safari kutoka Chimara jijini Mbeya mpaka Njombe ili kumuona Asante Kwasi ambaye ni beki wa kushoto wa Wekundu wa Msimbazi hao.

Njombe Mji ambao walikuwa wenyeji, waliwakilishwa na David Kisu, Christopher Kasewa, Stephen Mwanjala, Hussein Akilimali, Peter Mwangosi, Jimmy Mwasandola, Awadh Salum, Mustapha Bakari, Ethiene Ngladjoe, David Obash pamoja na Ditram Nchimbi.

Kikosi cha Simba kilikuwa; Aishi Manula, Nicholas Gyan, Asante Kwasi, Yusuph Mlipili, Jjuuko Murshid, Erasto Nyoni, James Kotei/Salim Mbonde, Shomari Kapombe, John Bocco, Emmanuel Okwi/Laudit Mavugo pamoja na Shiza Kichuya/Haruna Niyonzima.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here