SHARE

Mwamuzi, rekodi balaa zito Liver ikiita City

MERSEYSIDE, England

NI wikiendi nyingine tamu kwa mashabiki wa Ligi Kuu ya England (EPL). Liverpool watakuwa Anfield kuumana na mabingwa watetezi, Manchester City.

Tofauti ni pointi sita kati ya timu hizo, Liverpool wakiwa wamejichimbia kileleni mwa msimamo, wakifuatiwa na vijana wa ‘bishoo’ wa Kihispania, Pep Guardiola.

Baada ya kila moja kushuka dimbani mara 11, Liverpool wameweka kibindoni pointi 31, wakati Man City wao wamejikusanyia 25 kuelekea mchezo huo.

Hii unaweza kuiita mechi ya kisasi kwani timu hizo zilipokutana kwa mara ya kwanza msimu huu, mchezo wa Ngao ya Jamii uliochezwa Wembley, Man City walishinda kwa ‘matuta’ baada ya sare ya bao 1-1.

Kama ulivyo huu, mchezo wa raundi ya kwanza EPL msimu uliopita ulimalizika kwa timu hizo kutofungana.

Kasi ya timu zote

Katika mechi 11, kila moja imepata sare moja, lakini Liverpool wameshinda 10, wakati Man City wameibuka na ushindi mara tisa na kuchezea vichapo viwili.

Man City wamefungwa moja (2-0 dhidi ya Everton), wameshinda nane na kutoa sare moja (1-1 dhidi ya Atalanta) katika mechi 10 zilizopita za mashindano mbalimbali.

Ukiwatazama Liverpool, unaona wao wametoa sare moja tu (1-1 dhidi ya Man United) katika mechi 10 zilizopita.

Rekodi

Mechi 44 za Ligi Kuu zilizowahi kuvikutanisha vigogo zimewashuhudia Liverpool wakishinda 19, Man City wakitamba mara tisa, huku zikiwapo sare 16.

Katika michezo 16 ya Ligi Kuu kati ya timu hizo pale Anfield, Liverpool hawajafungwa na mara ya mwisho kwa Man City kushinda katika uwanja huo ikiwa ni mwaka 2003.

Pia, Klopp ndiye aliyemfunga mara nyingi Guardiola kuliko kocha yeyote. Guardiola amefungwa mechi saba kati ya 17 za mashindano mbalimbali.

Nyota watakaoikosa mechi

Kwa Man City, Ederson hatasimama langoni kwani ni majeruhi, wakati pia kikosi hicho kitawakosa David Silva, Rodri, Oleksandr Zinchenko, Aymeric Laporte na Leroy Sane.

Liverpool watashuka dimbani wakiwa bila beki wao wa kati, Joel Matip, kama ilivyo kwa Xherdan Shaqiri na Nathaniel Clyne.

Mwamuzi

Michael Oliver ndiye atayekuwa katikati ya uwanja kuamua vita hiyo. Tangu kuanza kwa msimu huu, ameamua mechi mbili za Liverpool, kama alivyofanya kwa Man City.

Katika michezo hiyo, Liverpool imeshinda yote (Norwich na Chelsea), wakati Man City wametamba moja (Tottenham) na kutoa sare mwingine (Everton).

Ukichukua takwimu za jumla, Oliver ameichezesha Liverpool mara 40, ikishinda 23, wakati Man City wamekutana naye katika michezo 32, wakiondoka na ushindi mara 31.

Liverpool; Alisson, Alexander-Arnold, Lovren, Van Dijk, Robertson, Henderson, Fabinho, Wijnaldum, Salah, Firmino na Mane.

Man City; Bravo, Walker, Otamendi, Fernandinho, Mendy, De Bruyne, Gundogan, Bernardo, Mahrez, Aguero na Sterling.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here