Home Habari BUSWITA AANIKA KILICHOMSAINISHA SIMBA, YANGA

BUSWITA AANIKA KILICHOMSAINISHA SIMBA, YANGA

1086
0
SHARE

NA CLARA ALPHONCE

SIKU chache baada ya kupigwa umeme wa mwaka mmoja kukaa nje ya soka kutokana na kudaiwa kusaini katika timu mbili tofauti, kiungo Pius Buswita amefunguka sababu zilizomfanya kuingia kwenye mtego huo.

Hivi karibuni Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) inayoongozwa na Mwenyekiti Richard Sinamtwa, ilimfungia mwaka mmoja baada ya kubaini kuwa mchezaji huyo amesaini mikataba miwili ndani ya msimu mmoja wa 2017/18 yaani Yanga na Simba.

Kitendo hicho ni uvunjwaji wa kanuni ya 66 ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo inaelekeza kufungiwa mwaka mmoja kwa mchezaji yeyote atakayekiuka kanuni hiyo.

Akizungumzia sakata hilo, Buswita alisema haikuwa dhamira yake kusaini mikataba hiyo lakini imetokea kutokana na shinikizo ambalo alilipata kutoka kwa Simba.

“Simba ndio walikuwa wa kwanza kunitumia tiketi ya ndege kutoka Mwanza kuja Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya nao mazungumzo, lakini tulishindwana, Yanga nao wakaonyesha nia nikafanya nao mzungumzo na kusaini mkataba wa miaka miwili.

“Lakini baada ya kusikia nimesaini nilishangaa familia yangu ikipokea vitisho vikilazimisha nisaini mkataba au kurejesha pesa za tiketi ya ndege pamoja hela ya usumbufu,” alisema Buswita.

Alisema kutokana na vitisho hivyo, mama yake mzazi akamshauri asaini tu kuwaridhisha Simba ili ajiepushe na vitisho hivyo japo haikuwa kwa hiari yake.

Hata hivyo, DIMBA lilimtafuta Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspoppe, ili kuzungumzia sakata hilo ambapo alisema mchezaji huyo ni mwongo kwa kuwa klabu aliyoanza kusaini ni Simba na si Yanga.

“Ni jambo la kushangaza kuona mchezaji analalamika kuwa analazimishwa kusaini, kwa umri wake analazimishwaje? Aache kusema uongo tarehe aliyosaini Simba inajulikana na ya Yanga inajulikana waangalie wataona wapi alianza,” alisema Hanspoppe.

Kwa upande wa Yanga, Katibu Mkuu wake Boniface Mkwasa, alisema  wamepata barua rasmi ya kufungiwa kwa mchezaji huyo, lakini alisema wapo katika kujadili ili kuangalia kama wanaweza kukata rufaa.

Buswita msimu uliopita aling’ara akiwa katika timu ya Mbao FC na kusababisha klabu za Simba na Yanga kumnyatia saini yake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here