Home Makala BUSWITA HURU, VIPI RAFIKI YANGU MKOPI?

BUSWITA HURU, VIPI RAFIKI YANGU MKOPI?

691
0
SHARE

NA ABDUL MKEYENGE

SHETANI amemuachia Pius Buswita sasa ni huru kukipiga Yanga. Soka letu kwenye sintofahamu nyingine iliyozua maswali mengi yaliyokosa majibu.

Kutoka Agosti 12 katika Ukumbi ule wa St. Gaspel mjini Dodoma mpaka leo Septemba 12 ni mwezi mmoja sasa wa viongozi wapya wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwepo madarakani.

Ndani ya mwezi huo mmoja kumeshakuja sintofahamu zinazotuchanganya sisi maamuma. Kama masihara vile ndani ya mwezi huo tumejionea kukosewa kutengenezwa kwa Ngao ya Hisani na medali zake. Sasa tumejionea suala la Buswita lilivyoamuliwa kishetani kwa mujibu wa Buswita mwenyewe aliyepitiwa na shetani.

Buswita alisaini mikataba na timu mbili. Alisaini mkataba na Simba kisha akasaini na Yanga. Mwisho kabisa akatokeza Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji, Elias Mwanjala na kusema klabu hizo zimezungumza na kuafikiana juu ya mchezaji huyo ambapo Yanga ikikamilisha kile walichozungumza Buswita atakuwa wao. Ndani ya mwezi huu mmoja tumejionea haya!

Kanuni za TFF ziko wazi kwa mchezaji aliyesaini timu mbili ndani ya msimu mmoja. Kanuni inamtaka mchezaji kusimama kucheza msimu mmoja bila pingamizi wala malalamiko. Kamati ilihitaji nini cha ziada ili kumwadhibu Buswita?

Suala la Buswita halikuhitaji huruma yoyote ile kwa mujibu wa kanuni zilizotungwa na wavunja kanuni, lakini kutokana na shetani aliyempitia Mwanjala na kamati yake wamepitisha huruma sehemu ambayo nao walipaswa kuweka roho ya kishetani, si vinginevyo.

Wachezaji wengi wamewahi kukumbana na adhabu ya kusimamishwa msimu mzima, mmoja wao ni rafiki yangu Mohamed Mkopi. Huyu ni rafiki yangu kabisa ninayekaa naye mtaa mmoja Mwananyamala.

Rafiki yangu Mkopi msimu wa ligi iliyomalizika nilikuwa nikienda naye uwanjani kama shabiki kutazama wenzake wakicheza na hakukuwa na iliyokuja kwa ajili ya kumhurumia.

Mkopi alilia na nafsi yake, hajalia na mtu mwingine ili kuipata huruma ya kamati. Adhabu yake imeisha hivi sasa ni mchezaji wa Mbeya City na moja ya mambo anayoyajutia katika maisha yake ya soka ni kusaini timu mbili.

Kama kuna shetani la huruma, inakuwaje shetani hilo linaishia kwa baadhi ya wachezaji? Sisi ‘maamuma’ tulihitaji kuona meno ya kamati ya Mwanjala kwenye suala la Buswita, lakini si kwa ilivyofanyika.

Kanuni zinazotungwa zisimamiwe ili kuondoa ukakasi unaoupa sura mbaya mchezo wa soka. Ni uvunjaji wa kanuni kwa baadhi ya wachezaji kuadhibiwa na wengiwe kusamehewa kwa kosa moja kwa kila mmoja. Haki hakuna tena! Haki imesiginwa.

Muda huu ambao soka letu linahitaji dira mpya ya maendeleo mambo kama haya ya Buswita yanahitaji kutiliwa mkazo kwa kanuni zake kufuatwa.

Kama kamati ya Mwanjala itafanya kazi zake kwa kufuata usuluhishi wa pande mbili ni ngumu suala hili kumalizika. Litaendelea kuwepo siku hadi siku.

Siku kamati ya Mwanjala itakapoamua kubadilika ndiyo masuala ya namna hii yataisha, lakini kwa namna hii sioni lini matatizo haya yakiondoka.

Ni ngumu kutamka kama kuna upendeleo ambao uko kwa baadhi ya wachezaji na timu. Ni ngumu kulitamka hili kutokana na kukosa uthibitisho, lakini tunakoendea siku moja watu watalitamka hili bila wasiwasi wowote ndani ya vinywa vyao.

Watalitamka hilo kupitia marejeo ya baadhi ya wachezaji Athuman Iddy (Chuji), Kelvin Yondan. Watatamka hivi watu hawa. Kwanini tufike kote huko?

Ni wakati wa kamati hii kujitazama kwa macho matatu na kujipima kama wanatosha, kisha wajiulize wanawatendea haki Watanzania waliowaamini?

Kwa muundo wa soka letu ni ngumu kuwa na kamati inayoweza kukosa malalamiko kutoka sehemu mbalimbali, lakini kuna baadhi ya mambo yanasababishwa na kamati yenyewe na mengine yako nje ya uwezo wa kamati.

Kwenye hili la Buswita kamati haikwepi lawama, licha ya baadhi ya malalamiko mengine ya watu kukosa mashiko.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here