Home Habari CAF YAISOGEZEA YANGA MAMILIONI

CAF YAISOGEZEA YANGA MAMILIONI

2483
0
SHARE

 NA MWANDISHI WETU              |               


KAMA wachezaji wa Yanga watazitumia vyema dakika 90 za mchezo wa leo dhidi ya Gor Mahia ya Kenya, basi watakuwa wamejiweka kwenye mazingira mazuri ya kupata milioni 170 kutoka Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF).

Ndio, hili ni fungu tofauti na ile milioni 625 ambayo Wanajangwani hao watapokea kutoka CAF kama zawadi ya kufanikiwa kucheza hatua ya makundi Kombe la Shirikisho.

Kwa mujibu wa CAF, timu mbili zitakazomaliza kwenye nafasi mbili za mwisho kwenye kundi lao, zitazawadiwa dola za Marekani 275,000 (sawa na milioni 625 za Tanzania).

Lakini kwa timu mbili za juu katika makundi hayo zitakazofuzu hatua ya robo fainali zitapata zawadi ya dola za Marekani 350,000 (sawa na Shilingi milioni 795).

Mpaka sasa Yanga wanashika mkia katika Kundi D wakiwa na pointi moja, hivyo wana uhakika wa kupata milioni 625, lakini kama wataichapa Gor Mahia, watakuwa na pointi nne zitakazofufua matumaini yao ya kufuzu robo fainali na kupata nyongeza hiyo ya dola za Marekani 75,000.

Kiasi hicho watakachovuna kwa kufuzu robo fainali pia kinaweza kutumika kulipa mishahara ya wachezaji wote wa Yanga kwa mwezi.

Kwa sasa bajeti ya Yanga kwenye mishahara ya mwezi mmoja ni Shilingi milioni 135, hivyo dola za Marekani 75,000 zinaweza kutatua shida hiyo na chenji ikabaki.

Akizungumza na DIMBA, msemaji wa Yanga, Dismas Ten alisema wanatambua umuhimu wa mchezo wao dhidi ya Gor Mahia hivyo wamejipanga kuhakikisha wanabeba pointi tatu.

“Tulipoteza mchezo wa kwanza ugenini kwa mabao 4-0, lakini kama unavyofahamu hii ni hatua ya makundi kwa hiyo kila mchezo una umuhimu wake. Kwa leo lengo letu ni kupata pointi tatu,” alisema Dismas.

Akieleza kuhusu fedha za CAF, Dismas aliongeza: “Hii ni michuano mikubwa na mbali na heshima ya klabu kufuzu hatua ya robo fainali kuna pesa nyingi huwa zinatolewa kila hatua. Tunafahamu tayari tunaweza kupata Shilingi milioni 625 lakini hilo halitufanyi tukaridhika na kuacha kuzipambania Shilingi milioni 795 kama tutafuzu robo fainali.”

Kwa upande wake kocha mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, amewataka mashabiki wamiminike kwa wingi uwanjani leo na kuwahakikishia kwamba amewaandaa vijana wake kushinda dhidi ya Gor Mahia.

“Tumefanya maandalizi mazuri, nina uhakika yatatupa matokeao mazuri, najua utakuwa mchezo mgumu lakini tutapambana kuhakikisha tunaondoka uwanjani kifua mbele,” alisema.

Kocha huyo amesema anafurahi kuona baadhi ya wachezaji walikosekana mchezo uliopita kikosini na sasa anaweza kuwatumia katika mchezo wa leo wakiwemo Deus Kaseke na Matheo Anthony.

Mbali na hao huenda kocha huyo akaimarisha zaidi safu yake ya ulinzi kwa kumtumia Kelvin Yondani, ambaye naye alikosa mchezo uliopita kutokana na suala la mkataba ambalo sasa limekwisha.

Katika michezo yao mitatu waliyocheza, Wanajangwani hao hawajafanikiwa kufunga bao lolote huku wakiruhusu nyavu zao kufungwa mabao nane, lakini mazoezi ya nguvu waliyoyachukua huenda leo wakawapatia mabao na ushindi.

Yanga walianza kwa kipigo cha mabao 4-0 ugenini dhidi ya USM Alger ya Algeria kabla ya kulazimishwa sare ya kutofungana nyumbani na Rayon Sport ya Rwanda kisha hivi karibuni kuchezea tena kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa Gor Mahia ugenini.

Baada ya leo, Yanga watawakaribisha tena USM Alger, Agosti 19 mwaka huu na baadaye kumalizia mchezo wao wa mwisho ugenini dhidi ya Rayon Sports Agosti 29.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here