Home Habari CAF YAMRUDISHA LWANDAMINA ZAMBIA

CAF YAMRUDISHA LWANDAMINA ZAMBIA

744
0
SHARE

SAADA SALIM NA MAREGESI NYAMAKA,

NI kama bahati ya mtende kwa  mabingwa watetezi wa Ligi Kuu nchini, Yanga, chini ya kocha Mzambia, George Lwandamina, kucheza hatua ya pili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kukipiga na Zanaco ya Zambia.

Zanaco ilipata nafasi hiyo kufuatia ushindi wa bao 1-0, dhidi ya APR ya Rwanda jana, ambapo mechi ya awali timu hizo zilitoka suluhu na hivyo kupata nafasi ya kusonga mbele.

Zanaco na Yanga sasa zitavaana kati ya Machi 10 hadi 12, katika mechi itakayopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kisha mechi ya marudiano itachezwa nchini Zambia wiki moja baadaye.

Yanga wanaamini kwamba kocha Lwandamina aliyejiunga Yanga akitokea timu ya Shirika la Umeme nchini humo (Zesco), analifahamu vizuri soka la Zambia na hivyo itakuwa ni rahisi kuipa timu yake hiyo mpya mikakati ya kupata ushindi.

Yanga imefanikiwa kusonga mbele licha ya kupata matokeo ya sare ya bao 1-1 dhidi Ngaya de Mbe ya nchini Comoro, katika mchezo wa marudiano uliopigwa jana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, katika mchezo wa ugenini uliochezwa Jumapili iliyopita Yanga ilishinda jumla ya mabao 5-1 na hivyo kuitoa nje ya michuano timu hiyo kwa ushindi wa mabao 6-2.

Katika mchezo huo, Ngaya waliokuwa wakipewa nafasi ndogo ya kushinda, ndio walioanza kuwashtua mashabiki wa Yanga na Watanzania kwa ujumla baada ya kupata bao la mapema dakika ya 19 ya kipindi cha kwanza ambalo lilifungwa na Zahir Mohamed kwa shuti kali lililomshinda kipa Deogratius Munishi na mpira kujaa wavuni.

Bao hilo liliwafanya wachezaji wa Yanga kutulia na kuanza kupanga mashambulizi ambapo katika dakika ya 43, beki wa kushoto, Mwinyi Haji, alifunga bao kwa shuti kali kutokana na pasi nzuri aliyopigiwa na Kelvin Yondani na kuzifanya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa zimefungana bao 1-1.

Katika kipindi hicho cha kwanza mpira ulikuwa mkali kila timu ikokosa nafasi kadhaa za wazi, Ngaya wakiwa wamekosa nafasi nyingi katika dakika ya tisa, Pakotoarimanana Falinirino, akikosa nafasi ya wazi huku Said Anfane, naye akishindwa kutumia nafasi alizozipata dakika ya 12 na 18.

Kwa upande wa Yanga licha ya kujitahidi sana kupata mabao ya mapema ngome ya Ngaya ilikaa imara huku Obrey Chirwa, akishindwa kuipatia bao dakika ya 18 ambapo licha ya kuwa kwenye nafasi nzuri aliachia shuti kali likapaa juu ya lango.

Kipindi cha pili timu zote zilionekana kukamiana ambapo Yanga walikuwa wakitaka kupata mabao ya haraka ili kudhihirisha kuwa hawakuwafunga wapinzani wao hao kwa bahati mbaya huko kwao, lakini hali ikawa tofauti na walivyotarajia kwani Ngaya nao walionekana kujifunza kutokana na makosa.

Baada ya kuona mambo yanakuwa magumu, Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina, alimtoa Juma Abdul na nafasi yake kuchukuliwa na Hassan Ramadhan ‘Kessy’ huku Deus Kaseke naye akitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Juma Said ‘Makapu’, lakini hadi dakika 90 zinamalizika timu hizo zilitoka uwanjani zikiwa zimefungana bao 1-1.

Katika mchezo huo, Yanga waliwakilishwa na Deogratius Munishi, Juma Abdul, Haji Mwinyi, Vicent Bossou, Kelvin Yondani, Justine Zulu, Simoni Msuva, Thabani Kamusoko, Obrey Chirwa, Deusi Kaseke pamoja na Emanuel Martin.

Kwa upande wa Ngaya kikosi kilikuwa, Said Mmadi, Said Hachim, Chadhuili Mradabi, Said Anfane, Franck Said Abderemane, Youssouf Ibrahim Moidjie, Rakotoarimanana Falinirino, Berthe Akpha, Zamir Mohamed, Mounir Mousa na Said Toihir.

Katika mechi nyingine ya michuano hiyo, Zanaco ilipata ushindi wa bao 1-0, dhidi ya APR ya Rwanda, mechi ya awali timu hizo zilitoka suluhu ya 0-0.

Katika hatua nyingine straika wa Yanga, Amissi Tambwe, amewaambia mashabiki wao kuwa wajitokeze kwa wingi Februari 25, mwaka huu Uwanja wa Taifa kushuhudia wakiwaadabisha Simba.

“Leo (jana) sijacheza kutokana na majeraha, lakini naamini nitakuwepo dhidi ya Simba Mungu akipenda, naamini kuwa utakuwa mchezo mgumu lakini nawaambia mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi kwani kwa jinsi mambo yalivyo nina imani tutashinda,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here